:::::::
Chama cha NCCR-Mageuzi kimeiomba jamii kuendelea kudumisha amani na mshikamano, kikiwataka wananchi kuepuka kuchochewa na watu wachache wanaolenga kuvuruga utulivu wa nchi kuelekea uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 29, mwaka huu.
Kauli hiyo imetolewa leo Oktoba 27, 2025 na Katibu Mkuu wa chama hicho, ambaye pia ni mgombea mwenza wa urais, Dkt. Evaline Wilbard Munisi, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika makao makuu ya chama hicho jijini Dar es Salaam.
Dkt. Munisi amesema kuwa amani na mshikamano ni hazina kubwa kuliko mali yoyote, hivyo kila Mtanzania ana wajibu wa kuvilinda kwa nguvu zote bila kujali tofauti za dini, kabila au itikadi za kisiasa. Alisisitiza kuwa uchaguzi ni tukio muhimu la kihistoria na linapaswa kufanyika kwa utulivu.
Aidha, amesema kampeni za uchaguzi zimekuwa zikifanyika kwa amani kote nchini, jambo linalodhihirisha uwepo wa misingi imara ya kisiasa na kijamii. Alitaja utulivu huo kuwa matokeo ya ushirikiano kati ya vyama vya siasa, Ofisi ya Msajili wa Vyama na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC).
Katika maelezo yake, Dkt. Munisi alibainisha kuwa moja ya ajenda kuu katika Ilani ya NCCR-Mageuzi ya mwaka 2025 ni Muafaka wa Kitaifa, inayolenga kujenga maridhiano na kuimarisha misingi ya amani kama nguzo ya maendeleo ya Taifa.
Amesema kuwa mabadiliko madogo yaliyofanyika katika sheria na kanuni za uchaguzi ni matokeo ya ushirikiano wa vyama vya siasa na serikali, hatua iliyowezesha kampeni kufanyika kwa amani na uwazi bila pingamizi lolote hadi sasa.
Akihitimisha, Dkt. Munisi alisema NCCR-Mageuzi haitaki kuona vurugu au taharuki siku ya uchaguzi, akisisitiza kuwa chama hicho kinapinga maandamano ya aina yoyote na badala yake kinawahamasisha Watanzania kujitokeza kwa wingi kupiga kura kama njia sahihi ya kuleta mabadiliko wanayoyataka.

