Usafiri mikoani, Dar-Zanzibar kusitishwa Oktoba 29

Dar/mikoani. Wakati Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa) ikieleza sababu za baadhi ya kampuni kusitisha safari zake kati ya kesho Jumanne Oktoba 28-30, 2025, Chama cha Kutetea Abiria kimeeleza sababu hizo hazina mashiko kwani kila mtu ana shida zake za kijamii na  kifamilia.

Baadhi ya kampuni za usafirishaji wa barabara na nyingine za majini zimetangaza kusitisha safari zake kati ya kesho Oktoba 28, hadi 29 na nyingine kwenda hadi Oktoba 30 ili kupisha shughuli ya upigaji kura katika uchaguzi mkuu utakaofanyia Oktoba 29, 2025.

Baadhi ya kampuni  za mabasi yanayofanya safari zake kutoka Dar es Salaam kwenda Mwanza, Tarime (Mara), Kilimanjaro, Arusha, Tabora, Mpanda (Katavi), Bukoba, Karagwe (Kagera), Kigoma na baadhi ya mikoa imetangaza kutosafirisha abiria Oktoba 29, siku ambayo Watanzania watapiga kura.

Kampuni ya Azam Marine  na Zan Fast Ferries nazo zimetoa taarifa kwa umma kwamba Oktoba 29, 2025 hazitatoa huduma ya usafiri majini iwe Dar es Salaam-Zanzibar au Zanzibar- Dar es Salaam hadi Oktoba 30.

Hata kwenye mitandao yao, ukitaka kukaa tiketi tarehe hiyo haikupi nafasi ya kuichagua.

Leo Jumatatu, Oktoba 27, 2025, Mwananchi limezungumza na viongozi wa Tabora, Chama cha Kutetea Abiria na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra) juu ya taarifa zinazotolewa mitandaoni na baadhi ya kampuni za mabasi na

Msemaji wa Taboa, Mustapha Mwalongo amesema huo si msimamo wa Taboa, isipokuwa ni kampuni mojamoja zimeamua kutofanya safari siku hiyo.

“Ni kweli baadhi ya kampuni zimeamua kusitisha safari zake hususani siku ya kupiga kura (Oktoba 29) baadhi ya kampuni zina hofu kwamba abiria watakuwa wachache, hivyo zikaona zisitishe.

“Kama nilivyosema huo si msimamo wa Taboa, ni kampuni moja moja, zipo baadhi zimepunguza ruti, mfano mtu anapeleka gari tano Mbeya, siku hiyo ana hofu kama abiria hawatokuwepo, hivyo anapunguza na kusalia na ruti moja,” amesema.

Amesema wamiliki wa mabasi wanaamini uchache wa abiria siku hiyo, hivyo wamelazimika kupunguza ruti na wengine kusitisha safari ili kutoa mwanya kwa Watanzania kushiriki kikamilifu kupiga kura.

Hata hivyo, Katibu wa Chama cha kutetea abiria, Hashim Omary amesema sababu za wamiliki wa mabasi ni za nidhamu ya woga ambazo hazina mashiko.

“Huko ni kukiuka sheria za usafirishaji, kwani unaweza usipeleke gari na watu wasipige kura, zingekuwa na mashiko kama Serikali ndiyo ingekuwa imewambia wasitishe, lakini kama ni uamuzi binafsi, hizo ni sababu ambazo hazina mashiko,” amesema.

Amesema kila mtu anaposafiri huwa na sababu zake za msingi, wengine ni za ugonjwa, mwingine anawahi sehemu ambayo hawezi kuacha kwenda.

“Sasa unaachaje kumpeleka kwa sababu ya kupiga kura? sidhani hata Serikali inaunga mkono hili, hayo ni mawazo yao ya uoga kwamba wataunguza mafuta.

“Kama chama cha kutetea abiria tunaamini siku hiyo abiria wapo kama kawaida, kwani kila mtu ana shida zake za kijamii,kifamilia, misiba wagonjwa, kusitisha safari hakuna mashiko,” amesema.

Kwa upande wake,Mkurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra), Johansen Kahatano alipoulizwa juu ya baadhi ya mabasi kusitisha huduma za usafiri, amesema amezungumza na baadhi ya wamiliki na kujua sababu.

“Mmoja kasema ni sababu ya usalama, lakini tayari polisi walishatoa taarifa kuhakikisha hali ya usalama nchini siku ya uchaguzi hilo sio tatizo, na tumewaambia viongozi wa chama chao kuhusu hilo.

“Baadhi ya wamiliki wamesema wao wataendelea kutoa huduma kama kawaida, hakuna shida, ni wachache sana ambao wamesitisha, lakini ni kwa sababu zao tu,” amesema.