Mgombea urais TLP: Puuzeni maneno ya mitandao jitokezeni kupigakura

Moshi. Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha Tanzania Labour Party (TLP), Yustas Rwamugira, amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura Oktoba 29, 2025, akisisitiza kuwa uchaguzi upo kwa mujibu wa Katiba ya nchi na kwamba kila Mtanzania ana wajibu wa kushiriki katika mchakato huo muhimu wa kidemokrasia.

Rwamugira ametoa wito huo leo Jumatatu, Oktoba 27, 2025, wakati akizungumza kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika Kata ya Marangu Mashariki, Jimbo la Vunjo, mkoani Kilimanjaro, ambapo amewataka wananchi kupuuza maneno ya mtandaoni na kila mmoja ajitokeze kupiga kura.

“Nendeni mpige kura, mmalize muende nyumbani. Najua kumekuwa na maneno kwenye mitandao ya kijamii wakidai hakuna uchaguzi, hayo ni maneno yasiyo na kichwa wala miguu. Uchaguzi upo na unafanyika kwa mujibu wa Katiba,” amesema Rwamugira.

Amefafanua kuwa muda wa uongozi wa Serikali iliyopo madarakani umeisha kikatiba, hivyo ni haki ya wananchi kuchagua viongozi wapya.

Ameeleza kuwa mfumo wa vyama vingi upo kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hivyo wananchi wasirubuniwe na taarifa za upotoshaji.

“Tulikuwa na utawala wa chama kimoja cha TANU, baadaye CCM, kisha tukaingia kwenye mfumo wa vyama vingi. Sasa tuna wagombea 17 wa urais, nami ni mmoja wao kupitia TLP,” amesema.

“Jitokezeni mkapige kura, vituo vya kupigia kura haviko mbali. Hata kama kitambulisho cha mpigakura kimepotea, njoo na kitambulisho cha uraia au leseni, majina yako yatahakikiwa kituoni,” ameongeza.

Amesema; “Uchaguzi upo kwa mujibu wa Katiba. Oktoba 29, kila mmoja atoke akapige kura. Puuzeni maneno ya mitandao siku hiyo ni yenu, siku ya kufanya maamuzi kwa mustakabali wa nchi.”

Rwamugira ametumia nafasi hiyo kuwataka wananchi wasiogope wala wasiwe na hofu, bali watumie siku hiyo kufanya maamuzi ya busara kwa kuchagua viongozi wanaostahili kuongoza taifa, wabunge na madiwani wanaojua shida za wananchi.

Rwamugira amewaomba wananchi kumchagua Richard Lyimo awe Mbunge wa Vunjo  aendelee na dira ya marehemu Augustino Lyatonga Mrema, aliyewahi kuwa mbunge wa Vunjo, kwa kupigania maendeleo ya wananchi.

“Mpeni nafasi Lyimo, mzaliwa wa hapa, anayejua changamoto zenu. Tufanye kazi pale alipoishia Mrema,” amehimiza Rwamugira.

Katika mkutano huo, mgombea ubunge wa Jimbo la Vunjo kupitia TLP, Richard Lyimo, ameahidi kuunda kamati shirikishi ya ubunge itakayoshirikiana na wananchi kutambua na kutatua changamoto za jimbo hilo.

“Tunayo changamoto ya miundombinu ya barabara, masoko, shule, vituo vya afya na hospitali. Nipeni nafasi ya ubunge niwe sauti yenu bungeni kuhakikisha changamoto hizi zinapata suluhisho,” amesema Lyimo.

Kwa upande wake, mgombea ubunge wa Moshi Vijijini kupitia TLP, Dominic Macha, naye amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi siku ya uchaguzi kutimiza haki yao ya kikatiba.

“Tuhakikishe Oktoba 29 tunatoka mapema kupiga kura. Tunahitaji amani na utulivu, tusipotoshwe na taarifa za mitandao. Tuchague viongozi makini watakaotuletea maendeleo,” amesema Macha.