WAKATI Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) likitangaza Novemba 3, 2025 litachezesha droo ya upangaji wa makundi na ratiba ya Ligi ya Mabingwa Afrika, imefahamika wapinzani wanaoweza kukutana na wawakilishi wa Tanzania, Yanga na Simba.
Kwa mujibu wa viwango vya klabu vya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) mwaka 2025 na kanuni za michuano hiyo, timu zilizo katika chungu (POT) sawa haziwezi kupangwa pamoja katika hatua ya makundi.
Yanga imefuzu makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa msimu wa tatu mfululizo ikianza 2023-2024, 2024-2025 na sasa 2025-2025, kwa mujibu wa CAF itakuwa kwenye chungu (POT) namba mbili kutokana na nafasi ya 12 inayoshika kwenye viwango vya Klabu Bora Afrika vya Shirikisho hilo ikikusanya pointi 35.
Simba yenyewe imefuzu hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika, ikiwa ni mara ya tano ndani ya kipindi cha miaka nane sasa, hadi sasa ipo chungu (POT) namba mbili, lakini inaweza kupanda nakuwa namba moja endapo RS Berkane haitafuzu. Berkane inacheza na Al Ahli Tripoli kuwania kufuzu makundi, mechi ya kwanza imeisha kwa sare ya bao 1-1. Simba ipo nafasi ya tano viwango vya CAF ikiwa na pointi 48.
Kwa kuwa Yanga na Simba zote zipo POT 2, haziwezi kukutana zenyewe, lakini zitagawana vigogo mmojammoja kutoka POT 1 ambao ni Al Ahly (Misri) yenye pointi 78 za CAF, Mamelodi Sundowns (Afrika Kusini) yenye pointi 62, na Esperance de Tunis (Tunisia) yenye pointi 57. Timu ya nne inayotarajiwa kuungana nao ni RS Berkane (Morocco) yenye pointi 52 endapo itafuzu kwa kuiondoa Al Ahly Tripoli.
Hatari iliyopo kuwa Pot 2 ni kwamba, Simba na Yanga zitakuwa tayari kukukutana na aidha Al Ahly, Mamelodi Sundowns, Esperance, au RS Berkane na mashabiki lazima wajiandae kwenda Uwanja wa Benjamin Mkapa kutazama timu zao zikivaana na vigogo hao.
POT 2 inatarajiwa pia kuwa na Al Hilal (Sudan) na Pyramids FC (Misri) ikiwa itafuzu ikikabiliwa kucheza dhidi ya Ethiopian Insurance ya Ethiopia baada ya ugenini kutoka 1-1, na huenda Petro de Luanda (Angola) iwapo Pyramids haitafuzu, hivyo kama timu hizo zitakuwa kwenye poti hiyo hazitaweza kukutana.
POT 3 inaweza kuwa na AS FAR Rabat (Morocco), MC Alger (Algeria), Rivers United (Nigeria), JS Kabylie (Algeria), ambapo hapa pia timu moja itavaana na Simba na Yanga.
Pot 4 inaweza kujumuisha Saint Eloi Lupopo (DR Congo), Power Dynamos (Zambia), Petro de Luanda (Angola) na Stade Malien (Mali), huku ndiyo sehemu pekee ambayo timu nyingi kutoka kwenye POT zingine za juu zitakuwa na matumaini ya kuvunia pointi.
TIMU ZILIZOFUZU MAKUNDI
Al Ahly (Misri)
Power Dynamos (Zambia)
Al Hilal SC (Sudan)
St Eloi Lupopo (DR Congo)
Yanga (Tanzania)
Rivers United (Nigeria)
Petro Luanda (Angola)
JS Kabylie (Algeria)
AS FAR (Morocco)
Simba (Tanzania)
Mamelodi Sundowns (Afrika Kusini)
Esperance (Tunisia)
Stade Malien (Mali)
MC Alger (Algeria)
BADO ZINASAKA KUFUZU
Pyramids vs Ethiopian Insurance (mechi ya kwanza sare ya bao 1-1)
RS Berkane vs Al Ahli Tripoli (mechi ya kwanza sare ya bao 1-1)
