Fountain Gate yashtua Ligi Kuu

KITENDO cha kukusanya pointi saba katika mechi tatu mfululizo za Ligi Kuu Bara ilizocheza Fountain Gate, imeonekana kurejesha ari, morali na matumaini kwa mastaa wa timu hiyo, huku wakitamba kuwa kazi ndio imeanza.

Timu hiyo iliyoweka makazi yake mkoani Manyara, haikuwa na mwanzo mzuri ilipochezea vichapo kwenye mechi tatu za kwanza na kujikuta ikiwapa presha ndani na nje ya uwanja.

Katika mechi tatu za awali, timu hiyo ilianza kupoteza kwa bao 1-0 dhidi ya Mbeya City, ikakwaa kisiki tena kwa kufa 3-0 mbele ya Simba, kisha kulala 2-0 kwa Mtibwa Sugar na kuifanya kuwa mkiani mwa msimamo wa ligi.

Hata hivyo, kwa sasa kikosi hicho kimeonekana kubadilika na kuimarika kwa kushinda mechi mbili dhidi ya Dodoma Jiji 1-0, matokeo sawa na KMC, huku ikitoa sare na Coastal Union 1-1 na kuchumpa nafasi ya nne kwa pointi saba, ikizidiwa pointi moja na kinara Mbeya City.

FOUN 01

Mshambuliaji wa timu hiyo, Joshua Ibrahim, amesema matokeo waliyoanza nayo ilitokana na changamoto ya baadhi ya mastaa kutokuwapo, akieleza kuwa kwa sasa kazi ndio imeanza.

Amesema baada ya kuvuna pointi tatu kwenye mechi iliyopita dhidi ya KMC, kwa sasa akili ipo kwa Pamba Jiji watakaowafuata jijini Mwanza, kuhakikisha wanaendeleza ubabe na kurejesha heshima yao.

“Kwa sasa tumeanza upya ligi, hatukuwa na mwanzo mzuri ila nadhani kila mmoja ameona tunachofanya, mkakati wetu ni kuona mechi yoyote tunapata ushindi ili kufidia tulizopoteza,” amesema nyota huyo.

FOUN 02

Staa huyo wa zamani wa KenGold, ameongeza kuwa kama ilivyokuwa katika kikosi alichotoka kufuatia uhakika wa namba, bado anazidi kupambana kujihakikishia namba licha ya ushindani ulivyo.

“Vita ya namba ni kubwa lakini kama ambavyo nimeaminiwa na benchi la ufundi naendelea kupambana kuhakikisha nalinda heshima hii, kikubwa ni kupambania timu,” amesema nyota hiyo.

Fountain Gate katika mechi hizo tatu za kwanza, ilicheza ikiwa na wachezaji 14 tu waliofanikiwa kuingizwa kwenye mfumo wa usajili, huku wengine wakikumbana na changamoto hadi baadaye hali ilipokaa sawa.