Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limethibitisha kumkamata mfanyabiashara wa mtandaoni Jenifer Bilikwiza Jovin, maarufu kama Niffer, kwa tuhuma za kuhamasisha vurugu na kuharibu miundombinu kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025.
Akizungumza Jumatatu, Oktoba 27, 2025, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, amesema Niffer alikamatwa majira ya saa 9 alasiri katika eneo la Sinza Kumekucha, alipokuwa dukani kwake.
Taarifa hiyo imekuja kufuatia madai yaliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii kwamba mfanyabiashara huyo alikuwa ametekwa na watu wasiojulikana.
“Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam mnamo Oktoba 27, 2025, majira ya saa 9 mchana, eneo la Sinza Kumekucha, limemkamata na linamuhoji Jenifer Bilikwiza Jovin (26), mkazi wa Masaki Peninsula, Kinondoni,” ilisomeka sehemu ya taarifa hiyo ya Polisi.
Kamanda Muliro amesema uchunguzi unaendelea, na hatua zaidi za kisheria zitachukuliwa mara tu taratibu za awali zitakapokamilika.
Related
