NEC yatoa maelekezo 10 muhimu uchaguzi mkuu Oktoba 29

Dar es Salaam. Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imetoa maelekezo 10 kwa wapigakura na wadau wote wa uchaguzi kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 huku ikisisitiza maandalizi yote yamekamilika na Watanzania wanapaswa kujitokeza kutekeleza haki yao ya kikatiba kwa amani na utulivu.

Taarifa ya INEC imetolewa leo Oktoba 28,2025 na Mwenyekiti wa tume hiyo  Jaji Jacobs Mwambegele siku moja kabla ya uchaguzi mkuu huku akisisitiza watendaji wa vituo tayari wamepatiwa mafunzo, na taratibu zote za uchaguzi zimekamilika kwa mujibu wa sheria.

“INEC imekamilisha maandalizi yote ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, tunawaomba Watanzania wote wajitokeze kwa amani, kwa kufuata sheria na kanuni za uchaguzi, amani ya nchi yetu ni jukumu letu sote,” amesema Jaji Mwambegele.

Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo, uchaguzi wa mwaka huu unatarajiwa kuwa wa kipekee kutokana na maboresho makubwa ya kiutendaji na kiteknolojia yaliyofanywa na tume, ikiwemo usimamizi wa upigaji kura kwa uwazi na ushirikishwaji wa wadau wote.

“Tume imeweka mifumo ya kisasa kuhakikisha uchaguzi unakuwa huru, wa haki na wa kuaminika. Tunataka kila kura ihesabiwe, na matokeo yaakisi matakwa ya wananchi,” ameongeza Jaji Mwambegele.

Katika taarifa yake, Jaji Mwambegele ametoa maelekezo 10 muhimu ambayo wapigakura wote wanapaswa kuyazingatia siku ya uchaguzi.

Kwa wapigakura wasiokuwa na picha, Jaji Mwambegele amesema ambao majina yao yapo kwenye daftari la kudumu ka mpiga kura lakini picha zao hazionekani, wataruhusiwa kupiga kura endapo taarifa nyingine kwenye kadi zitakuwa sahihi.

“Kama kadi ya mpigakura ina namba tofauti na ile iliyo kwenye daftari lakini jina na taarifa nyingine zinalingana, mpiga kura huyo ataruhusiwa kupiga kura.

Kwa wapigakura waliopoteza au kuharibu kadi zao wataruhusiwa kutumia kitambulisho cha Taifa (Nida), leseni ya udereva, au pasi ya kusafiria kuthibitisha utambulisho wao,”taarifa hiyo imeeleza.

Mpigakura mwenye kadi ambayo taarifa zake hazipo kwenye daftari la kudumu hataruhusiwa kupiga kura, kwani uthibitisho wa taarifa kwenye daftari ndiyo unaotambulika kisheria.

Kwa wapigakura  wa kata zilizofutwa, zikiwemo Kanoge, Katumba, Mishamo na Milambo, tume imewahamishia kwenye vituo vipya vilivyoidhinishwa kuhakikisha kila mmoja anashiriki uchaguzi.

“Tume imesisitiza kuwa upigaji kura ni siri na hakuna mtu anayepewa ruhusa kueleza au kushinikizwa kueleza nani alimchagua, kura ni siri, ni haki ya mtu binafsi. Tunawasihi wananchi wote waheshimu utaratibu huu,” amesema Jaji Mwambegele.

Pia Jaji Mwambegele ameelekeza wapigakura kuondoka kituoni baada ya kupiga kura na kurejea nyumbani, mawakala wa vyama ndiyo watakaoshuhudia mchakato wa kuhesabu kura.

“Kila mpigakura anatakiwa kupiga kura katika kituo alichojiandikisha au alichopangiwa na INEC, hatua inayolenga kudhibiti msongamano na makosa ya kiutendaji.

Wale waliobadilisha vituo kwa ajili ya kupiga kura ya Rais pekee hawataruhusiwa kupiga kura kwenye kituo cha awali kwa sababu majina yao hayatakuwepo kwenye orodha ya wapigakura wa eneo hilo,”amesema.

Katika kuhesabu kura, Jaji Mwambegele amesema kutafanyika katika kituo cha kupigia kura, isipokuwa pale panapotokea changamoto maalumu, mawakala wa vyama vyote vitakavyoshiriki wataruhusiwa kushuhudia hatua zote hadi matokeo kutangazwa.

Vituo vya kupigia kura vitafunguliwa saa 1:00 asubuhi na kufungwa saa 10:00 jioni, huku vituo maalum vya magereza na vyuo vya mafunzo vikifunguliwa saa 2:00 asubuhi na kufungwa saa 9:00 alasiri.

Wapigakura wenye mahitaji maalumu kama wazee, wajawazito, watu wenye ulemavu na akina mama wanaonyonyesha watapewa kipaumbele kupiga kura mapema, huku wasioona lakini wanaojua nukta nundu wakitumia jalada maalumu la nukta nundu (Tactile Ballot Folder) kupiga kura kwa siri.

Jaji Mwambegele amesema pia kuwa ni kosa kisheria kuvaa mavazi ya chama, kufanya kampeni, au kukusanyika ndani ya mita 300 kutoka kituo cha kupigia kura, vyombo vya usalama vitakuwepo kuhakikisha taratibu zinazingatiwa.

Kwa mujibu wa takwimu za INEC, vyama 17 vitashiriki katika uchaguzi wa urais na makamu wa rais, huku zaidi ya wagombea 1,700 wakishindania ubunge katika majimbo 264.

“Tunawasihi Watanzania wote wajitokeze kupiga kura kwa amani. Kura yako ni sauti yako. Uamuzi wako ndio mustakabali wa Taifa letu,  tume iko tayari, uchaguzi wa mwaka huu utakuwa wa heshima, wa haki, huru na wa amani,”amesema.