Mkopo wa mfumo huo unaotarajia kuondoa changamoto zilizopo katika sekta ya ardhi hasa migogoro ya makundi tofauti, umetolewa kwa ushirikiano wa Benki ya CRDB itakayotoa Euro milioni 7.949 na Taasisi ya Fedha ya Ufaransa ya BPIFrance, itakayotoa Euro milioni 29.55.
Akizungumza kwenye hafla ya kusaini mkataba huo iliyofanyika ikulu visiwani Zanzibar, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar, Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema ardhi ni rasilimali muhimu kwa maendeleo ya wananchi hivyo serikali imeona ni vyema kuipa thamani inayostahili kwa kuimarisha usimamizi wake.
“Nawashukuru Benki ya CRDB kwa kutuunga mkono katika wazo letu hili. Inachokifanya Serikali ni kuweka mazingira rafiki ya kila mwananchi kunufaika na adrhi anayoimiliki. Tuna hakika baada ya kufunga mfumo huu wa LARIS taarifa zote za umiliki na usimamizi wa ardhi hapa Zanzibar zitapatikana kirahisi hivyo kuondoa migogoro ya mipaka na matumizi mengine ya ardhi,” amesema Rais Mwinyi.
Kumalizwa kwa migogoro ya ardhi kwa kutumia mifumo ya kidijitali, Mheshimiwa Dkt. Mwinyi amesema kutawapa nafasi wananchi kuitumia ardhi kuomba mikopo benki na taasisi nyingine za fedha ili kutekeleza miradi na biashara walizonao hivyo kuharakisha kasi ya kujiletea maendeleo.
“Mfumo huu utaongeza kasi ya kutoa leseni wa wananchi na kumaliza changamoto ya uvamizi wa maeneo ya wazi au yale ya serikali na wawekezaji. Nawasihi Wazanzibari wote kutambua fursa njema zitakazoletwa na mfumo huu na kujiandaa kwa manufaa ya kiuchumi yanayotokana na ardhi iliyorasmishwa,” amsisitiza Dk. Mwinyi.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Zanzibar, Mheshimiwa Khadija Kassim amebainisha kuwa mfumo huu pia utainufaisha serikali kwani itarahisisha utambuzi wa wamiliki wote wa ardhi visiwani humo jambo litakalowapa nafasi nzuri wasimamizi katika ngazi zote kukusanya kodi ya ardhi.
“Ninaamini pindi mfumo huu utakapoanza kufanya kazi, makusanyo ya kodi ya ardhi yataongezeka kuanzia ngazi ya halmashauri mpaka taifa. Wizara na watendaji wake wataweza kuwakumbusha kulipia ada wanazodaiwa wamiliki watakaokuwa wamechelewa kutekeleza wajibu wao hivyo kuyapata mapato yote ya serikali kama inavyotakiwa,” amesema Mheshimwa Rahma.
Akisaini mkataba huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela, amesema mfumo huo utakwenda kuleta mageuzi makubwa katika sekta ya ardhi visiwani Zanzibar, kwa kuweka misingi imara ya usimamizi na umilikishaji wa ardhi kwa njia ya kidigitali. Amesema utekelezaji wa mradi huo utafungua fursa mpya za kifedha na kiuchumi, kwani urasimishaji wa ardhi utajenga imani kwa taasisi za fedha, zikiwemo benki, katika kutoa mikopo na huduma nyingine za kifedha kwa wananchi.
Aidha, amebainisha kuwa hatua hii itachochea ustawi wa wananchi kupitia uboreshaji wa huduma, ukuaji wa uwekezaji, na ujenzi wa uchumi shirikishi unaowanufaisha Wazanzibari wote. Akizungumza kuhusu utayari wa taasisi za nje ya nchi kushirikiana na Benki ya ndani na Serikali katika mradi huo, Nsekela amesema hiyo inaonyesha imani ya wadau wa kimataifa kwa Serikali na Benki ya CRDB katika kuusimamia miradi mikubwa ya kimkakati.
Kwenye mkakati wake wa biashara wa muda wa kati wa 2023/27, Benki ya CRDB imeweka kipaumbele kikubwa katika ushirikiano wa kimkakati na wadau wa kimataifa ili kurahisisha ufanikishaji wa ufadhili wa miradi mikubwa ya maendeleo nchini na katika mataifa ambako benki inatoa huduma zake.
Nsekela amebainisha kuwa kutokana na ushirikiano huo, tayari Benki ya CRDB imeshiriki na kufanikisha ujenzi wa Bwawa la Umeme wa la Julius Nyerere (JNHPP) na ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR), na kwa upande wa Zanzibar Benki ya CRDB imewekeza zaidi ya shilingi bilioni 484 kwa ajili ya kusaidia ufadhili ujenzi wa miundombinu ya barabara, shule za kisasa, na Uwanja wa Ndege wa Pemba.
Katika kuchochea maendeleo nchini, Nsekela amesema pia Benki hiyo imekuwa ikiwekea katika ubunifu wa huduma na bidhaa akitolea mfano utoaji wa hatifungani za kijani na hatifungani ya miundombinu ya ‘Samia Infrastructure Bond’ ambazo kwa pamoja zilikusanya jumla ya zaidi ya shilingi bilioni 494 kwa ajili ya kusaidia miradi ya kijani, pamoja na ujenzi wa miundombinu kwa kushirikikana na TARURA.
“Hivi karibuni pia tumetoa hatifungani inayofuata misingi ya sharia ya dini ya kiislam ‘CRDB Al Barakah Sukuk’ iliyotuwezesha kukusanya shilingi bilioni 125.4 na dola milioni 32.3 za Marekani. Fedha hizi zote zinalenga kuchochea kasi ya maendeleo katika sekta mbalimbali ikiwamo ujasiriamali na biashara, kilimo na uvuvi, elimu, afya, utalii, pamoja na utekeleza miradi ya kimkakati kwa maendeleo ya taifa letu,” amesema Nsekela.
Akieleza namna BPIFrance ilivyojipanga kushirikiana na Afrika, Makamu wa Rais anayesimamia Mikopo ya Nje wa benki hiyo yenye makao makuu yake jijini Paris nchini Ufaransa, Alienor Daugreilh amesema wanao uzoefu wa kutosha na walipopokea ombi la kutoka SMZ walilitekeleza kwa haraka kwani wanafahamu jinsi uchumi wa visiwa hivyo ulivyo imara na unaoku akwa kasi nzuri.
“Huu ni mwanzo tu, BPIFrance tutaendelea kushirikiana na Seriklai ya Mapinduzi Zanzibar kufanikisha miradi yake ya maendeleo. Tukiwa na wadau wetu imara Benki ya CRDB, naamini tunaweza kufanya mambo mengi mazuri kwa manufaa ya wananchi wa Zanzaibar na Tanzania yote kwa ujumla,” amesema Daugreilh.







