Bosi TRC azungumzia uchunguzi ajali ya SGR

Dar es Salaam.  Ikiwa zimepita siku kadhaa tangu treni ya Electric Multiple Unit (EMU) maarufu treni ya mchongoko iliyokuwa ikitokea Dar es Salaam kuelekea Dodoma kupata ajali, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Machibya Shiwa amesema uchunguzi bado unaendelea.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na TRC ajali hiyo ilitokea saa 2 asubuhi ya Oktoba 23, 2025 katika kituo cha Ruvu huku sababu ikitajwa ni hitilafu za kiuendeshaji.

Taarifa hiyo pia ilieleza kutoripotiwa kwa kifo huku ikibainisha kuundwa kwa timu ya wataalamu kwa ajili ya kuchunguza kwa kina chanzo cha ajali hiyo.

Timu hiyo ya wataalamu inaongozwa na Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi, Profesa Godius Kahyarara, vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na menejimenti ya TRC.

Jana Jumatatu, Oktoba 27, 2025, Mwananchi lilimtafuta Shiwa kujua kinachoendelea ambapo alisema kamati hiyo imeundwa kwa mujibu wa sheria na miongozo inayoongoza utendaji wa TRC.

Shiwa alisema kamati hiyo bado inaendelea kufanya uchunguzi wa kina na utakapokamilika taarifa rasmi itatolewa kwa umma.

“Uchunguzi unafanyika kwa hatua kuangalia nini kilifanyika na nini hakikufanyika,” alisema na kuongeza:

“Baada ya kukamilika kwa uchunguzi, taarifa yake inapita katika hatua mbalimbali na kupitiwa na wataalamu ili kujiridhisha ndipo iweze kutolewa kwa umma.”

Treni ya mchongoko, ambayo imekuwa ikifanya safari zake kutoka Dar es Salaam, Morogoro hadi Dodoma ilianza kutoa huduma Novemba 1, mwaka 2024.

Baada ya kutokea kwa ajali hiyo safari za treni ya SGR zilisitishwa kwa muda na baadaye kurejea.