Mwenyekiti wa Kamati ya ulinzi na usalama wilaya ya Chato, ambaye pia ni mkuu wa wilaya hiyo, Louis Peter Bura.
::::::
MWENYEKITI wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Chato mkoani Geita, Louis Peter Bura, amewahakikishia wananchi kuwa watakuwa salama wakati wote wa mchakato wa kupiga kura kwa madai vyombo vya dola vimejipanga kuimalisha hali ya usalama wakati wote.
Amesema hali itakuwa shwari na hakuna yeyote atakayebughudhiwa au kutishwa wakati wa mchakato wa upigaji kura, hivyo wananchi wajitokeze kwa wingi.
Akizungumza na vyombo vya habari ofsini kwake, Bura amesema kamati ya ulinzi na usalama imeweka mikakati madhubuti na ina taarifa za kina kuhusu hali ya kila eneo la wilaya hiyo, na kwamba wananchi wanapaswa kuwa watulivu na kutoingiwa na hofu.
Kauli hiyo ameitoa leo Oktoba 28, 2025 ikiwa imebaki siku moja kuelekea uchaguzi mkuu wa Rais,Wabunge na Madiwani nchini, huku akitoa onyo, na anasisitiza kuwa hakuna mwananchi atakayenyimwa haki yake ya kikatiba ya kushiriki katika uchaguzi.
Bura, ambaye pia ni Mkuu wa wilaya ya Chato amesema maandalizi ya uchaguzi yamekamilika kwa kiwango cha kuridhisha, na Tume Huru ya taifa ya Uchaguzi imeweka vituo 820 vya kupigia kura kwenye vijiji vyote 115 vilivyo kwenye Kata 23 ili kusogeza huduma hiyo karibu zaidi na wananchi.
“Nawaomba wananchi mjitokeze kwa wingi kupiga kura,” amesema Bura.
“Chagueni viongozi watakaoweza kutatua changamoto zenu na kuwaletea maendeleo, kulingana na sera zilizowasilishwa na vyama vyao.”
Amesema serikali imefanya maandalizi ya kutosha, ikiwemo kutoa elimu kwa wananchi na makundi mbalimbali kuhusu umuhimu wa kushiriki katika uchaguzi kwa amani.
Bura amesema kuwa vituo vya kupigia kura vitafunguliwa kuanzia saa 1:00 asubuhi hadi saa 10:00 jioni, na kwamba wananchi watakaokuwa bado kwenye foleni muda wa kufunga vituo utakapowadia, wataruhusiwa kupiga kura hadi wote watakapomaliza.
Vile vile amedai matarajio waliyonayo ni kuwa ifikapo saa tano usiku kura zitakuwa zimehesabiwa zote na kubandikwa kwenye mbao za matangazo na kwamba matokeo ya kila eneo yatatangazwa ndani ya saa 24.
Ikumbukwe kuwa upo usemi usemao “Hauwezi kumiliki uhuru wa maamuzi wa mtu yeyote, iwe ndugu, rafiki, wala mwenza, ila unaweza kumfundisha, kumuelimisha, kumpa tahadhari, au kumuonyesha mifano ya watu wengine walioharibikiwa, lakini mwisho wa siku atabaki na uhuru wa maamuzi juu ya hatima ya maisha yake bila kujali juhudi zako kwake”.
Hivyo suala la kupiga kura ni takwa la kikatiba ambalo uamuzi wa mtu yeyote haupaswi kuingiliwa ni vyema kuheshimu uamuzi huo hata kama wewe hupendi kutimiza haki hiyo ya kisheria.
Mwisho.
