Kuelekea uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29 mwaka huu, Kituo cha Sheria cha Everlasting Legal Aid Foundation (ELAF) kimewataka Watanzania kujiepusha na vitendo vya ukiukwaji wa sheria, ikiwemo kufanya maandamano yasiyo rasmi katika kipindi cha uchaguzi, ili kuendelea kulinda amani ya Taifa.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa ELAF, Dk. Hamis Masoud, amesema uchaguzi ni takwa la kisheria, hivyo ni muhimu kwa wananchi kuzingatia taratibu zilizowekwa badala ya kujihusisha na vitendo vinavyoweza kuhatarisha amani.
“Uchaguzi ni sehemu ya haki za kikatiba, lakini unapaswa kufanyika kwa kuzingatia sheria. Vitendo vyovyote vinavyokiuka misingi ya sheria havina nafasi. Tunawahimiza Watanzania wote washiriki uchaguzi huu kwa amani na utulivu,” amesema Dk. Masoud.
Katika hatua nyingine, kituo hicho kimeibua mjadala kuhusu marekebisho ya Sheria ya Uchawi ya mwaka 1928, kikiiomba serikali kufanya mabadiliko ya sheria hiyo ili kuruhusu matumizi ya teknolojia za jadi kwenye masuala ya ulinzi wa taifa, maendeleo na urithishaji wa mila na desturi za Kitanzania.
Dk. Masoud amesema ingawa sheria hiyo iliundwa enzi za ukoloni kwa lengo la kudhibiti vitendo viovu vinavyohusishwa na uchawi, bado kuna mambo chanya ya kimila ambayo yanaweza kusaidia jamii katika kulinda maadili na kuimarisha mshikamano wa kitaifa.
“Sheria ya uchawi ililenga kudhibiti maovu, lakini yapo mambo mazuri ya kimila ambayo yalisaidia jamii kudumisha amani na maendeleo. Tunashauri yafanyiwe tathmini upya ili yaendane na wakati,” ameongeza.
Kwa upande wao, baadhi ya vijana wameunga mkono wito wa ELAF, wakisisitiza umuhimu wa kudumisha amani kipindi chote cha uchaguzi na kuelimisha jamii kuepuka vurugu. Wengine walitoa maoni yao kuhusu hoja ya marekebisho ya sheria ya uchawi, wakisema ipo haja ya kuenzi mila zinazochochea umoja na maadili mema katika jamii.



