Mwanza. Katibu Mkuu wa zamani wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Bashiru Ally, amemuombea kura kwa Watanzania mgombea urais kwa tiketi ya chama hicho, Samia Suluhu Hassan huku akitaja vigezo sita vinavyombeba mgombea huyo, ikiwemo ustahimilivu na usimamizi makini wa rasilimali za nchi.
Vigezo vingine ni Samia kuwa kiongozi mwenye msimamo usioyumba hasa masuala yanayohusu masilahi ya nchi na usalama wa nchi na kuwa amesimamia vema Muungano.
Dk Bashiru ameyasema hayo leo Jumanne Oktoba 28, 2025 katika viwanja vya CCM Kirumba, jijini Mwanza wakati wa mkutano wa kufunga kampeni ya chama hicho.
“Samia ni kiongozi mwenye msimamo usioyumba hasa masuala yanayohusu masilahi na usalama wa nchi, majaribio yalikuwepo tangu alipoingia ofisini nimeyaona, lakini amesimama kidete kwa ujasiri kutetea Muungano wetu na leo Muungano ni imara,” amesema na kuongeza;
“Ni msimamizi makini rasilimali za nchi, ambazo zinahitaji mifumo na umakini zaidi kuliko watu kusimamia kwa mabavu, chini ya uongozi wake amesimamia mifumo ya kodi na uwezekano wa watu kudokoa mali za umma kwa mifumo, akikabidhiwa dhamana rasilimali za nchi utakuwa salama, matumizi ya rasilimali za umma yataelekezwa maeneo yanayohusu maendeleo ya watu.”
Amesema kuwa Samia anafaa kuaminiwa na kupewa dhamana kuongoza nchi kwa sababu ni kiongozi anayejipambanua kama kiongozi bora na kuwaomba Watanzania wamchague mgombea huyo.
Ametaja vigezo hivyo kuwa ni Samia ni kiongozi anayefahamu na kujali shida na kero za anaowaongoza na katika kipindi cha miaka minne alitambua mahitaji ya wananchi wake na akayafanyia kazi ili yawe na matokeo bora.
“Kigezo cha pili mgombea wetu ni mchapakazi na mbunifu hata namna umeongoza mpangilio wa kuendesha kampeni miezi miwili ni uthibitisho wa uchapakazi, kabla na baada ya kuwa Katibu Mkuu wa CCM, sijawahi kuona maandalizi ya chama na nchi kuingia katika uchaguzi kama ilivyotokea mwaka huu.
“Samia ana kila sababu ya kuomba mumchague na sisi tuna kila sababu ya kumnadi ili achaguliwe, niko hapa mimi kumsemea sifa na vigezo alivyonavyo vya uongozi bora. Jamhuri ya mitandaoni ilisema iliyoyasema nadhani sasa wameshika adabu kwa sababu ametufundisha namna ya kunyamaza na kutochokozeka,” amesema.
Amefafanua kuwa Samia ndiye kiongozi ambaye walipokuwa bungeni alipeleka mpango wa Serikali wa namna ya kutumia fedha za mkopo kukabiliana na madhara ya Uviko -19, ambapo alielekeza fedha hizo kwenye sekta ya maji na zimebadilisha sekta hiyo kwa kiwango ambacho hakijawahi kutokea pamoja na ujenzi wa madarasa na miradi mingine.
“Samia ni mstahimilivu na mtulivu, uchaguzi wa mwaka huu na kampeni zake ulikuwa uchaguzi kujadili masuala sio watu, hata pale alipotukanwa yeye binafsi na familia yake, chama chake na Serikali anayoongoza alisimama na kuwaasa na kuwasihi Watanzania akasema msichokozeke na kwa maelekezo hayo nchi nzima wananchi wamesikiliza sera, hawakusikiliza masuala binafsi ya wagombea.
“Rais ni binadamu kama wengine anafurahi anachukizwa, anasononeka lakini kwa nafasi yake ukipata mtikisiko na presha kubwa ukashindwa kusimama bila kujibu mapigo hicho ni kigezo muhimu sana cha kiongozi bora. Ni mtu asiyeyumba, asiyetolewa kwenye mstari kutokana na dhihaka au dharau ni sifa muhimu anastahili kuitwa kiongozi bora,” amesema.
Kwa upande wake aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Ziwa Victoria, Ezekiah Wenje, amewataka Watanzania kutambua kuwa kupiga kura ni haki yao ya kikatiba, hivyo wajitokeze kwa wingi kesho kwenda kuchagua viongozi wanaowataka watakaowawakilisha katika ngazi mbalimbali za maamuzi.
“Kiongozi bora ni yule anayejali watu wake, anayewapa matumaini kuwa kesho yake itakuwa bora kuliko leo, kiongozi bora anakuwa mfariji mkuu kwa watu anaowaongoza hadi anaopingana nao na yuko tayari kuwasikiliza. Suala la kura ni haki yako ya kikatiba, usikubali akili yako kushikiwa na mtu,” amesema.
