Cheki Yanga ilivyoikimbiza Simba CAF

MASHABIKI wa Yanga wanalia timu yao haipo sawa, lakini kumbe takwimu zao zinawabeba vizuri ikionyesha umwamba mbele ya Simba.

Takwimu zinaonyesha kwenye mechi nne za hatua ya mtoano kwa kila timu katika Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu huku zote zikifuzu makundi, Yanga imeipiga bao Simba ikiwa na namba nzuri.

Yanga imeonyesha kuwa na ubora wa kufunga mabao ikiwa nayo saba, wakati Simba ikipata mabao matano, huku zote zikiruhusu bao moja.

Kwenye mabao hayo kwa timu zote mbili, vinara wa kufunga ni viungo wa Yanga, Pacome Zouzoua na Aziz Andabwile waliofunga mara mbili kila mmoja sawa na Kibu Denis wa Simba.

YANG 01

Wengine waliofunga bao moja ni beki Dickson Job, mshambuliaji Prince Dube na winga Edmund John wote wa Yanga, wakati Simba wakiwa beki Wilson Nangu, kiungo Jean Charles Ahoua na winga Ellie Mpanzu.

Yanga imekuwa bora kwenye kutengeneza nafasi ikiwa nazo 37 huku zile ambazo zilikuwa karibu kupatikana mabao ni 14.
Simba ilitengeneza jumla ya nafasi 25 kwenye mechi hizo nne lakini kubwa zikiwa saba pekee ambazo ni mara mbili ya zile walizotengeneza watani wao.

YANG 02

Simba imeipiga bao Yanga eneo moja tu la kutopoteza mechi, ikishinda mbili na kutoa sare mbili, huku Yanga ikishinda tatu na kupoteza moja ilipotibuliwa hesabu na Silver Strikers ugenini kwa kufungwa bao 1-0.

Kwa timu zote zilizofuzu hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu, Simba ndiyo pekee ambayo haijashinda mechi yoyote nyumbani ndani ya mechi nne za mtoano na wekundu hao mechi mbili za nyumbani zote zimeisha kwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Gaborone United, kisha 0-0 dhidi ya Nsingizini Hotspurs.

YANG 03

Yanga pia ndio timu iliyopiga mashuti mengi ambayo ni 42, lakini yaliyolenga lango yalikuwa 25 huku Simba ikipiga jumla ya mashuti 35 lakini yaliyolenga lango 17.

YANG 04

Timu hizo mbili hazitaweza kukutana hatua ya makundi baada ya kuwekwa kwenye chungu kimoja namba mbili kwenye droo itakayofanyika Novemba 3, 2025, jijini Johannesburg, Afrika Kusini.