Camara ashtua Simba, mabosi waingia sokoni mapema

KUWEPO kwa taarifa za kipa wa Simba, Moussa Camara kutarajia kufanyiwa upasuaji wa goti, imefichuka ndiyo chanzo cha vigogo wa klabu hiyo kujihami mapema kuingia sokoni kuanza kusaka mbadala aliye na kiwango cha juu.

Chanzo kutoka katika klabu hiyo kilisema Camara alipata changamoto ya goti mechi dhidi ya Gaborone United iliyomalizika kwa sare ya bao 1-1 na hakumaliza, nafasi yake ikachukuliwa na Yakoub Suleiman aliyetua Simba msimu huu akitokea JKT Tanzania.

Kuanzia hapo, Yakoub amecheza mechi tatu, moja ya ligi dhidi ya Namungo Simba ikishinda 3-0, kisha mbili za Ligi ya Mabingwa dhidi ya Nsingizini Hotspurs na Simba ilishinda ugenini 1-0, nyumbani ikatoka 0-0 na kufuzu makundi Ligi ya Mabingwa Afrika.

CAMA 01

Endapo Camara akifanyiwa upasuaji, kuna uwezekano wa kukaa nje siyo chini ya miezi sita na anaweza akazikosa mechi za Ligi Kuu Bara dhidi ya JKT Tanzania, Azam na Yanga, pia mechi za mwanzo za CAF katika hatua ya makundi msimu huu.

Siyo taarifa ngeni kwa Camara aliyezaliwa Novemba 27, 1998 nchini Guinea kutajwa kuachwa Simba, kwani ni tangu usajili wa dirisha lililopita na hivi karibuni alipoitwa katika majukumu ya taifa, ilielezwa baada ya kupimwa goti alionekana kuwa na jeraha kubwa.

Chanzo hicho kilisema: “Baada ya kurejea Simba, alipelekwa hospitali, bado daktari alisisitiza majeraha yake ya goti ni kubwa, lazima afanyiwe upasuaji.”

CAMA 02

Kwa taarifa za ndani zinasema kipa ambaye viongozi wa Simba wanazungumza naye ni yule aliyeng’ara katika michuano ya CHAN akiwa na timu ya taifa ya Madagascar, Michel Ramandimbisoa na kama atasajiliwa itakuwa ni mwaka mmoja kutokana na umri wake kuwa mkubwa, kwani amezaliwa Februari 11 mwaka 1986, ana miaka 39.

“Ni kipa mzuri na mwenye uwezo mkubwa, lakini atapewa mwaka mmoja, umri wake ni mkubwa, hatuwezi kuwa na malengo naye ya muda mrefu,” kilisema chanzo hicho.

Chanzo hicho kilisisitiza ulazima wa kusajili kipa mwingine, huku wakiwa wanamwangalia Yakoub kama kiwango chake kitapanda na akiumia apate msaidizi wake.

Hivi sasa ambapo Yakoub amekuwa akianza katika kikosi cha Simba, mbadala wake ni Hussein Abel, kipa ambaye yupo katika kikosi hicho kwa msimu wa pili.

CAMA 03

Msimu uliopita, Camara ndiye aliyeibuka kinara upande wa makipa waliocheza mechi nyingi bila ya kuruhusu bao ambapo zilikuwa 19 kati ya 28 alizokaa langoni.

Akizungumza na Mwanaspoti, Dokta Samweli Shita anayeandikia Mwanaspoti, alisema, jeraha la goti (knee injury) linaweza kumfanya mchezaji akae nje kwa muda tofauti, kutegemea ukubwa wa jeraha na eneo lililoathirika.

“Jeraha dogo (Minor sprain/strain), hapa ni misuli au mishipa (ligaments) inakuwa imevutika au kupata maumivu bila kupasuka, muda wa kuwa nje unaweza kuwa, wiki 1-3.

“Jeraha la kati (Moderate ligament injury/meniscus tear ndogo), hapa ni mishipa kama meniscus inachanika, muda wa kuwa nje ni wiki 4-8 (mwezi 1 hadi 2).

“Jeraha kubwa (ACL tear, meniscus tear kubwa, fracture), hapa mishipa mikubwa kama ACL (Anterior Cruciate Ligament) au PCL ikipasuka, au kukatika kwa cartilage, muda wa kuwa nje huwa inategemea kama utafanyiwa upasuaji basi ni kuanzia miezi 3-6.”