TULIKUTA VIROBA NANE VYENYE VIUNGO VYA BINADAMU: SHAHIDI

Na Karama Kenyunko Michuzi Tv

MKUU wa Upelelezi Kituo cha Polisi Kawe, Joram Magova (45) ameieleza Mahakama Kuu Masijala ndogo ya Dar es Salaam kwamba alikuta viungo vya binadamu ikiwemo kichwa na viganja vya mikono vilivyotenganishwa kwenye viroba nane tofauti na kutupwa maeneo ya Tegeta Ununio jijini humo.

Magova ambaye ni Mrakibu wa Polisi na shahidi wa pili katika kesi ya mauaji inayomkabili Abdallah Musa maarufu Mr Bluu, alitaja viungo vya binadamu alivyovikuta kwenye viroba hivyo vilivyofungwa kwa kamba ya katani kuwa ni viganja vya mikono viwili ambavyo kucha zake zilikuwa zimepakwa rangi , paja moja na kipande cha kalio.

Pia alikuta kipande cha kifua, utumbo wa ndani ambao ulikuwa umefungwa katika baibui ya rangi nyeusi na ndani ya mfuko kulikuwa na kilemba chekundu na nguo ya ndani (underskirt).

Akiongozwa na Wakili wa serikali Mwandamizi, Edith Mauya, mbele ya Jaji Awamu Mbagwa, shahidi huyo alidai alipata taarifa ya kuwepo kwa viroba vinane vikiwa vimefungwa kamba ya katani huku vikitoa harufu kutoka kwa msiri.

SP Magova amedai kuwa, Agosti 22, 2024 majira ya saa 10 jioni akiwa ofisini Mbweni, alipokea taarifa kutoka kwa msiri kuwa eneo la Kunduchi kulikuwa na mifuko ya salfeti minne ikiwa inatoa harufu kali na kuvuja damu.

Ameeleza baada ya kupata taarifa hiyo alichukua timu yake ya ukaguzi ambao ni ofisa uchunguzi wa kisayansi Inspekta Ally , askari Nickson na askari wengine wa upelelezi na kwenda eneo la karibu na hoteli ya Silver Sand Kunduchi, Dar es Salaam.

“Nilipofika niliona mifuko imefungwa na kamba ya katani salfeti ilikuwa na rangi ya kijani mpauko ambapo kulikuwa na mifuko miwili na baada ya umbali wa mita 200, kutoka mifuko hiyo miwili kukawa kuna mifuko mingine ya rangi hiyo hiyo ikiwa imefungwa.” amedai Sp Magova.

Amedai mara moja walianza ukaguzi wa kufungua mfuko mmoja baada ya mwingine akiwa na askari wenzake na kukuta vipande vya binadamu ambavyo vilishaanza kuoza.

“Nilipofungua niliona viganja vya mikono viwili ambavyo kucha zake zilikuwa zimepakwa rangi , paja moja na kipande cha kalio huku eneo lingine ilikuwa ni kipande cha kifua na utumbo wa ndani ambao ulikuwa umefungwa katika baibui ya rangi nyeusi na ndani ya mfuko kulikuwa na kilemba chekundu na pia tulikuta nguo ya ndani andasketi,” ameeleza.

Amedai baada ya kuona viungo hivyo alibaini kuwa ni vya binadamu mwenye jinsia ya kike.

Ameendelea kudai kuwa baada ya kukamilisha shughuli ya ukaguzi alivichukua viungo hivyo akaviweka pamoja ili kupelekwa hospitali kwa ajili ya kufanyiwa vipimo vya vina saba kufahamu ni nani.

SP Magova, ameieleza mahakama kwamba baada ya kukamilisha shughuli hiyo alifungua jalada la kukutwa na viungo vya binadamu katika kituo cha polisi Wazo Mbweni ambapo hivi sasa ni Mbweni.

Alidai kila askari alikuwa na jukumu lake ambapo wengine waliendelea kuangalia kama kuna viungo vingine huku askari Nickson akiwa na jukumu la kupiga picha za viungo hivyo.

“Baada ya hapo nilipeleka viungo hivyo hospitali ya rufaa Mwananyamala pia niliposti katika group (kundi) la mkoa ambalo ni group maalumu kwa watoa taarifa,” amedai.

Amedai baada ya kusambaza katika group hilo siku hiyo hiyo majira ya saa tatu usiku alipigiwa simu na RCO wa Temeke, ACP Kimu kuwa anawasiliana na ndugu ambao walitoa taarifa kuhusiana na kupotelewa na ndugu yao.

“ACP Kimu alikuja tukakutana Mwananyamala hospitali akiwa na ndugu ambao walitoa taarifa za kupotelewa ndugu yao ambapo baada ya kuona viungo vile walitambua nguo ambayo ni Baibui, mikono na zile rangi za kucha na kitambaa chekundu cha kichwani.” amedai.

Sp Magova ameendelea alidai kudai kuwa, Agosti 23, 2024, akiwa ofisini kwake alipigiwa simu na RCO Kimu kuwa yupo na na mtu aliyemtaja kwa jina la Abdalah Musa anayehusika na viungo vya binadamu na kumtaka waungane na mtuhumiwa huyo ili kumuonesha baadhi ya viungo vingine.

“Nilikwenda eneo lile la Ununio nilimkuta RCO Kimu akiwa na wapelelezi pamoja na mtuhumiwa akiwa anaelekeza eneo la awali ambapo tayari tulikuwa tumeshachukua viungo hivyo na eneo hilo lilikuwa linaonekana kwani majani yalikuwa yamelala na kuna damu,” amedai

Baada ya kuwaonesha maeneo hayo, ambayo walikuwa wamekwisha chukua mifuko mshitakiwa aliwapeleka eneo la Tegeta ambapo walikuta mfuko mmoja wa salfet ambao ndani yake kulikuwa na viganja vya miguu miwili vilivyopakwa rangi ya kucha na nyama zingine. Kesi hiyo imeahirishwa hadi itakapoangiwa session nyingine

“Alitelekeza pia eneo lingine tukasogea mtaa wa perenge tulikuta mifuko miwili, mmoja ulikuwa na paja moja na eneo la mikono na nyama zingine , baada ya hapo mtuhumiwa alitupeleka eneo la ununio Kipugwani tulikuta mfuko ukiwa na kichwa cha binadamu vyote vikiwa na uwiano wa mtu mmoja,” amedai.

SP Magova, alidai siku hiyo baada ya kumaliza shughuli hiyo alirudi ofisini kwake huku RCO Kimu alikwenda na vielelezo hivyo ofisini kwake Temeke, ikiwa ni jumla ya viroba vinane.

Katika kesi hiyo Mr. Bluu anadaiwa, alitenda kosa Agosti 19, mwaka jana, eneo la Chang’ombe wilaya ya Temeke, Dar es Salaam, ambapo alimuua kwa makusudi Ezenia Kamana, anayedaiwa alikuwa ni mpenzi wake.