TRA United kumrudisha Bongo Senzo anarudi Bongo

WALE TRA United ni kama wako siriazi sana na kama hufahamu ni kwamba wako kwenye hatua za mwisho  kumrudisha nchini bosi aliyewahi kufanya kazi bora na klabu za Simba na Yanga.

Inaelezwa kwamba TRA United imekuwa katika msako wa kutafuta Ofisa Mtendaji Mkuu mpya, na hesabu zimetua kumrudisha nchini Senzo Mazingiza.

Mwanaspoti linafahamu kwamba mabosi wa TRA United walikuwa na majina matatu, lakini katika mchujo huo Senzo ndiye aliyekubalika na wengi ili aje kufanya kazi ya kuijenga klabu hiyo kiutawala.

Taarifa za ndani zimeliambia gazeti hili kuwa uzoefu wa Senzo katika kusimamia mchakato wa mabadiliko ya klabu ya Yanga na uongozi wake wake ndani ya Simba, ambako kote alihudumu kama mtendaji mkuu ndivyo vimempa nafasi kubwa.

“Mbali na kufanya kazi ndani ya Simba na Yanga, Senzo pia amewahi kufanya kazi kwenye Bodi ya Ligi Kuu nchini Botswana, kabla ya kuachana nao na kurudi kufungua kampuni yake ya mambo ya utawala wa soka.

“Nadhani tutakwenda na Senzo, naona ni mtu ambaye amekubalika na wengi ukizingatia hapa nchini ana ufahamu wa mambo ya soka la Tanzania akifanya kazi hizi klabu kubwa.”

Aliongeza kuwa:  “Unajua tunataka sio tu kuwa timu inayoshiriki ligi, ila tunajipanga tuwe ndani ya nne bora hatutaki kuwa watu wa kujaribu. Tulipoinunua hii timu kutoka Tabora United ilimaliza nafasi ya tano, lazima na sisi tuende mbali zaidi.”