WASIRA APIGA KURA , AWASIHI WANANCHI WASIPOTEZE NAFASI KUCHAGUA VIONGOZI WATAKAOONGOZA MIAKA MITANO IJAYO

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wasira ametimiza haki yake ya kikatiba kwa kupiga kura ya kuchagua rais, mbunge na madiwani mjini Bunda, mkoani Mara.

Wasira amepiga kura leo Oktoba 29, 2025 katika kituo cha kupigia kura Shule ya Msingi Kabalim, iliyopo Kata ya Majengo Wilaya ya Bunda na kusema kuwa amefanya hivyo kutekeleza takwa la kikatiba linalompa haki ya kuchagua viongozi anaowataka watakaoongoza nchi kwa miaka mitano ijayo.

“Mimi ni mpigakura wa hapa Kabalim Shule ya Msingi wa miaka yote, sikumbuki mara ya kwanza nilipiga lini lakini nimepiga miaka yote kama chaguzi tano zilizopita na uchaguzi wa mwaka huu nimekuja kutimiza haki yangu ya kupiga kura na nimeshapiga.

“Nimempigia mgombea urais, nimempigia mgombea ubunge na nimempigia mgombea udiwani kwa sababu kata hii ndiko mimi ninakoishi hapa Majengo,” ameeleza.

Ameeleza mwitikio mzuri wa wananchi waliojitokeza kupiga kituoni hapo na kuwataka ambao bado hawajajitokeza wafanye hivyo kabla ya saa 10 jioni upigaji kura utakapofungwa.

“Ninawaambia Watanzania hili ni zoezi la mara moja kwa miaka mitano na msingi wa zoezi hili ni kwamba kura yako inaamua nani awe rais wako, inaamua nani awe mbunge wako na nani awe diwani wako.

“Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 8, mamlaka yote ya nchi yapo mikononi mwa wananchi na wananchi wanayatoa mamlaka hayo kupitia sanduku la kura ndio wanaamua kwa miaka mitano, ikiisha tunarudisha mamlaka kwao halafu tunaomba ku-renew,” amesema.

Amewatakia heri waliofika kituoni kupiga kura na kuwataka wale ambao hawajafika wafanye hivyo wapate fursa ya kuamua nani awaongoze kwa miaka mitano ijayo.

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wasira akipiga kura katika Kituo cha Kupigia Kura Kabalim, Kata ya Majengo wilayani Bunda Mkoa wa Mara.