CAF yamkutanisha Aziz Ki na Fei Toto, ikimrudisha Ramovic Bongo

DROO ya Kombe la Shirikisho la Afrika iliyochezeshwa Jumatatu Novemba 3, 2025 imekuwa na mambo mawili katika soka la Tanzania.

Droo hiyo iliyofanyika katika Studio za SuperSport jijini Johannesburg nchini Afrika Kusini ikiongozwa na Mkuu wa Idara ya Mashindano ya CAF, Khaled Nassar, akisaidiwa na wanasoka wa zamani Christopher Katongo kutoka Zambia na Alexander Song wa Cameroon, imekuja na majibu ya kuwakutanisha marafiki wawili, Stephane Aziz KI wa Wydad Athletic Club na Feisal Salum ‘Fei Toto’ wa Azam.

Jambo lingine ni CAF imemrudisha Bongo Kocha Mjerumani, Sead Ramovic aliyewahi kuinoa Yanga, anakuja na kikosi cha CR Belouizdad kucheza dhidi ya Singida Black Stars ambapo atakutana na nyota wake wa zamani, Khalid Aucho, Clatous Chama na Nickson Kibabage.

Katika droo hiyo ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu wa 2025-2026, Azam imepangwa Kundi B itakutana na majirani, Nairobi United FC ya Kenya wakati Singida Black Stars ikiangukia Kundi C.

Azam FC inayoongozwa na kocha mwenye uzoefu, Florent Ibenge, mbali na Nairobi United, pia imepangwa na Wydad AC ya Morocco na AS Maniema Union kutoka DR Congo.

Fei Toto na Aziz KI walikuwa pamoja ndani ya kikosi cha Yanga na ushirikiano wao uliipa mataji mbalimbali klabu hiyo kabla ya kila mmoja kuondoka kwa wakati wake.

Kwa upande wa Singida Black Stars inayofundishwa na Miguel Gamondi, imepangwa Kundi C lenye timu za CR Belouizdad (Algeria), Stellenbosch FC (Afrika Kusini) na AS Otoho (Congo Brazzaville).

Belouizdad inayofundishwa na Ramovic, kocha huyo anakuja kukutana na Aucho, Chama na Kibabage ambao waliwanoa wakati Yanga ikicheza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliopita 2024-2025.

Mabingwa mara tatu wa Ligi ya Mabingwa, Wydad Athletic Club, wanalazimika kushiriki kwenye Kombe la Shirikisho msimu huu baada ya kumaliza vibaya kwenye ligi ya Morocco. Kupangwa kwoa katika Kundi B pamoja na Azam, maana yake kiungo wa zamani wa Yanga anayeitumikia klabu hiyo kwa sasa, Stephane Aziz Ki anarudi tena Tanzania.

Kwa upande mwingine, Olympic Club Safi, ambao wamefuzu kwa mara ya kwanza katika michuano ya klabu barani Afrika baada ya kushinda Kombe la Mfalme (Moroccan Throne Cup) msimu wa 2024-2025, wamepangwa katika Kundi A wakiwa na USM Alger (Algeria), Djoliba AC (Mali), na FC San Pedro (Ivory Coast).

Mechi za hatua ya makundi zinatarajiwa kuchezwa kuanzia Novemba 23, 2025 hadi Februari 2026.

Makundi kamili ni haya hapa:

Kundi A: USM Alger (Algeria), Djoliba AC de Bamako (Mali), Olympique Club Safi (Morocco), FS San Pedro (Côte d’Ivoire

Kundi B: Wydad AC (Morocco), AS Maniema Union (DR Congo), Azam FC (Tanzania), Nairobi United FC (Kenya)

Kundi C: CR Belouizdad (Algeria), Stellenbosch FC (Afrika Kusini), AS Otoho (Congo Brazzaville), Singida Black Stars FC (Tanzania)

Kundi D: Zamalek FC (Misri), Al Masry (Misri), Kaizer Chiefs FC (Afrika Kusini), Zesco United FC (Zambia)