Tanzania ipo katika kipindi kisicho na mfano katika historia yake ya kisiasa. Tunapotazama nyuma uchaguzi wa mwaka 2025, matukio yaliyotokea na maisha yaliyobadilika, tunajikuta tukitafakari ukurasa mgumu uliogeuka sehemu muhimu ya simulizi la taifa letu.
Katika kila kipindi cha uchaguzi, vyombo vya habari vimekuwa mstari wa mbele vikielimisha wananchi, vikihakikisha kuna uwiano wa madaraka, vikidumisha uwajibikaji na vikikumbusha kila raia wajibu wake katika kuimarisha demokrasia.
Lakini safari hii, matukio yaliyofuatana na ukakasi wake yameacha wengi wakiwa na majonzi, mshangao na swali lisilopotea masikioni mwa wengi linauliza: “Vyombo vya habari vilikuwa wapi?”
Siku ya kupiga kura na vurugu zilizofuatia zilisababisha vifo vya watu wakiwemo wasio na hatia na uharibifu wa mali za umma na watu binafasi. Katika nyakati za namna hiyo, wananchi wana haki ya kutarajia taarifa sahihi kwa wakati, pamoja na mwelekeo wa hatua za kuchukua kujilinda.
Hata hivyo, wakati huo wa taharuki, vyombo vya habari vya ndani ikiwemo Mwananchi vilishindwa kutekeleza wajibu wao wa msingi kuwa chanzo cha taarifa kwa taifa katika muda ambao taifa lilihitaji zaidi taarifa sahihi na kwa wakati.
Kwa miaka mingi, Mwananchi Communications Limited kupitia magazeti yake ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti imejijengea heshima kama nguzo ya habari za kuaminika. Watazamaji na wasomaji wetu hututegemea kupata ufafanuzi, ukweli na mwanga wa mambo. Ilipofika wakati ambapo hawakuweza kutupata, wengi walihisi kutotendewa haki, wakaachwa na sintofahamu na hisia za kutengwa. Tunazitambua hisia hizo.
Hata hivyo, ni muhimu kuelewa mazingira ambayo vyombo vya habari hufanya kazi. Uandishi wa habari ni taaluma iliyo chini ya mwongozo wa sheria, taratibu na kanuni zinazolenga kuhakikisha uwajibikaji, weledi na uhalali wa kazi zetu.
Oktoba 29, 2025, na katika siku chache zilizofuata, taifa lilijikuta likikabiliwa na kuzimwa kwa mtandao wa intaneti kote nchini. Hatua hiyo ilifanya vyombo vya habari vya ndani kutoweka katika mtandao wa kidijitali. Mfumo muhimu wa mawasiliano ulidorora kabisa, upatikanaji wa taarifa ukavurugika, na kama ilivyokuwa kwa mamilioni ya Watanzania na taasisi mbalimbali nchini, nasi tulijikuta tukiwa tumeondolewa kutoka kwenye zana muhimu za utendaji wetu wa kila siku.
Hatukugeuka nyuma. Hatukuiacha nchi yetu. Tulikosa tu njia ya kuwafikia kama ilivyo kwa Watanzania wengine. Hali waliyopitia wananchi nasi na waandishi wetu tumeipitia vivyo hivyo.
Dhamira yetu ya kuhudumia umma haijayumba. Tutaendelea kushikilia misingi ya juu ya uandishi wa habari, tukiwatumikia Watanzania kwa uadilifu, ujasiri na kwa heshima kubwa kwa misingi ya kisheria inayotuongoza.
Sasa, ni wakati wa kuponya majeraha. Kujenga upya. Na kusonga mbele kwa umoja kama taifa moja lenye matumaini mapya.
Tunaahidi kurejea upya kwa nguvu zaidi kuendeleza utamaduni wetu wa kuwapa wasomaji wetu taarifa sahihi zenye kuwajengea uwezo kama ilivyo kauli mbiu yetu: Tunaliwezesha Taifa.
Mwananchi Communications Limited