BAADA ya Shirikisho la Mpira wa Migu Afrika (CAF) kuchezesha droo ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho Afrika, kuna kazi kubwa ya kufanya kwa wawakilishi wetu Simba na Yanga zinazoshiriki Ligi ya Mabingwa, huku Singida Black Stars na Azam zikiwa Kombe ka Shirikisho.
Kwa Simba na Yanga, hii si mara ya kwanza kucheza hatua ya makundi, zimefanya hivyo zaidi ya mara tano, lakini Azam na Singida Black Stars kwao ni mara ya kwanza, ingawa makocha wa timu hizo sio mara ya kwanza kwao.
Miguel Gamondi kabla ya kutua Singida Black Stars aliiongoza Yanga kucheza makundi ya Ligi ya Mabingwa mara mbili mfululizo, 2023-2024 ambapo aliifikisha timu hadi robo fainali, kisha 2024-2025 alipofuzu makundi tu, akaondolewa.
Florent Ibenge, ni kocha mwenye rekodi kubwa Afrika akiwa tayari ameshinda ubingwa wa Kombe la Shirikisho akiwa na RS Berkane, ametua Azam na tayari ameweka rekodi ndani ya kikosi hicho akiifikisha makundi ya CAF kwa mara ya kwanza.
Hata hivyo, upande wa Ligi ya Mabingwa, mbali na Yanga na Simba kuwa na vibarua vya kuvuka kwenda robo fainali, kuna wachezaji watano wa kuchungwa zaidi wanaotazamwa kuwa ni hatari kunako hatua hii.
Pamoja na klabu kubwa kama Al Ahly, Mamelodi Sundowns, Espérance de Tunis na Pyramids FC ubora wa vikosi vyao unaweza kuwa silaha muhimu kuelekea kuwania taji la Ligi ya Mabingwa, lakini huwezi kuwaweka kando nyota hawa katika mafanikio binafsi.
1. Fiston Mayele – Pyramids FC
Ni wachache waliokuwa na mwaka mzuri kama Fiston Mayele. Straika huyu kutoka DR Congo aliongoza orodha ya wafungaji bora katika Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliopita na kuendeleza moto huo hadi Kombe la Dunia la Klabu (FIFA Intercontinental Cup), alipofunga hat-trick dhidi ya Al Ahli Saudi na kuvutia ulimwengu mzima.
Akiwa na kasi, nguvu, na umakini wa hali ya juu, Mayele pia alifunga bao la ushindi katika ubingwa wa Super Cup ya CAF dhidi ya RS Berkane, hiyo ni katika kuthibitisha nafasi yake kama mchezaji wa mechi kubwa.
Tayari amefunga mabao matatu kwenye hatua za awali msimu huu huku akiendelea kuwa miongoni mwa wanaowania tuzo za Mchezaji Bora wa CAF na Mchezaji Bora wa Klabu Afrika.
Mayele ana kazi ya kuonyesha ubora wake katika Kundi A ambapo Pyramids imepangwa na timu za RS Berkane (Morocco), Rivers United (Nigeria) na Power Dynamos (Zambia).
2. Oussama Lamlioui – RS Berkane
Oussama Lamlioui, mshambuliaji wa RS Berkane, anaendelea kung’ara kama mmoja wa washambuliaji wenye kiwango bora Afrika.
Baada ya kuongoza kwa mabao kwenye Kombe la Shirikisho msimu uliopita na CHAN 2024, Lamlioui amejidhihirisha kuwa mtaalamu wa utulivu na ufanisi katika dakika muhimu.
Berkane sasa wanataka kutafsiri ubabe wao wa Kombe la Shirikisho kuwa mafanikio kwenye Ligi ya Mabingwa, na ukali wa Lamlioui mbele ya goli utakuwa kiini cha safari hiyo.
Akiwa tayari na mabao matatu katika hatua za awali na akiwania tuzo za CAF, anazidi kuwa mmoja wa washambuliaji wanaoogopwa zaidi nchini Morocco.
3. Florian Danho – Espérance de Tunis
Usajili wa Florian Danho kutoka Randers FC ya Denmark, umeipa nguvu mpya safu ya ushambuliaji ya Espérance de Tunis.
Mfaransa huyu mwenye asili ya Ivory Coast, anajulikana kwa kasi, ujanja, na uwezo wa kumiliki mpira.
Katika mechi chache tu, amefunga mabao mawili kwenye ligi na mawili zaidi kwenye hatua za awali za Ligi ya Mabingwa, hii ni ishara kwamba amejibadilisha haraka.
Akiwa na thamani ya takriban Dola za Marekani 1.2 milioni (Sh2.9 bilioni za Tanzania), Danho anaonekana kama nyota ambaye anaweza kuwa mshambuliaji hatari msimu huu ikiwa ataendelea na kiwango chake cha sasa.
Espérance iliyopo Kundi D, wapinzani wake ikiwemo Simba inapaswa kumchunga zaidi mshambuliaji huyu. Timu zingine ni Petro de Luanda (Angola) na Stade Malien (Mali).
4. Nuno Miguel Santos – Mamelodi Sundowns
Kuwasili kwa Nuno Miguel Santos kutoka Vitória Guimarães ya Ureno kunaonesha dhamira ya Mamelodi Sundowns kutawala kila ngazi ya ushindani.
Mchezaji huyu wa zamani wa timu ya vijana ya Ureno, analeta nidhamu ya kimbinu, uzoefu wa Ulaya, na ubunifu katika timu ambayo tayari imejaa vipaji.
Uwezo wake wa kudhibiti kasi ya mchezo na kuvunja ngome imara unampa kocha Rhulani Mokwena silaha mpya ya kushambulia katika safari yao ya kutafuta taji jingine la bara.
Kundi C ndipo ipo Mamelodi Sundowns sambamba na timu za Al Hilal (Sudan), MC Alger (Algeria) na St Éloi Lupopo (DR Congo).
5. Emam Ashour – Al Ahly
Emam Ashour ni kiungo mwenye akili, ustadi, na ubunifu wa hali ya juu, kwa sasa anachukuliwa kama mmoja wa viungo kamili zaidi barani Afrika.
Baada ya msimu wa 2024-2025 ambapo alifunga mabao matano na kutoa pasi mbili za mabao kwenye Ligi ya Mabingwa, Ashour amekuwa mchezaji muhimu wa eneo la kiungo ndani ya Al Ahly.
Nguvu ya kupambana aliyonayo na uwezo wa kufunga katika mechi muhimu humfanya kuwa tegemeo kubwa katika harakati za Al Ahly kutafuta taji lingine la CAF.
Kuteuliwa kwake kuwania Tuzo ya Mchezaji Bora wa Klabu Barani Afrika ni uthibitisho zaidi wa ubora alionao.
Nyota huyu yupo na Al Ahly katika Kundi B ambalo pia kuna Yanga. Zingine ni AS FAR (Morocco) na JS Kabylie (Algeria).