Uchaguzi ulivyohitimishwa Samia akiapishwa muhula wa pili

Dar es Salaam. Siku saba baada ya Uchaguzi Mkuu Oktoba 29, kufanyika, Rais Samia Suluhu Hassan ameanza safari ya uongozi kwa muhula wake wa pili wa miaka mitano, baada ya kuapishwa kufuatia ushindi alioupata kwenye uchaguzi huo 2025 uliohitimishwa kwa vurugu.

Samia alikuwa miongoni mwa wagombea 17 walioshindana kwenye uchaguzi huo na baada ya uchaguzi, Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) ilimtangaza kuwa mshindi wa uchaguzi huo, akiwaacha mbali wapinzani wake.

Uchaguzi huo ulihitimisha siku 62 za kampeni ambapo vyama vya siasa vilipata fursa ya kunadi ilani zao za uchaguzi kwa wananchi na wagombea urais wakatoa ahadi lukuki kuwashawishi kuwapigia kura.

Wagombea urais walioshiriki uchaguzi huo na vyama vyao ni Samia (CCM), Salum Mwalimu (Chaumma), Gombo Samandito Gombo (CUF), Saum Rashid (UDP), Haji Ambar Khamis  (NCCR Mageuzi), Yustas Rwamugira (TLP) na Abdul Mluya (DP).

Wengine ni Mwajuma Mirambo (UMD), Twalib Kadege (UPDP), Hassan Almas (NRA), Coaster Kibonde (Makini), Doyo Hassan Doyo (NLD), Majalio Kyara (SAU), David Mwaijojele (CCK), Kunje Ngombare Mwiru (AAFP), Georges Bussungu (Ada-Tadea) na Wilson Elias (ADC).

Uchaguzi huo ulighubikwa na maandamano ya vijana (Gen Z) ambao walikabiliana na vyombo vya ulinzi na usalama ambavyo vilitumia silaha kali kuyadhibiti maandamano yao, jambo ambalo limesababisha vifo vya baadhi yao.

Licha ya kasoro zilizojitokeza baadhi ya maeneo, kama INEC ilivyobainisha wakati ikitangaza matokeo, kasoro hizo hazikuzuia uchaguzi huo kukamilika, hivyo Tume ikamtangaza Samia kuwa mshindi kupitia kura zilizopigwa.

Novemba mosi, 2025, Tume ya Uchaguzi iliandaa hafla maalumu ya kumkabidhi Samia cheti baada ya kupata ushindi huo kwa asilimia 97.66 ya kura zote zilizopigwa, na hivyo kuibuka kidedea dhidi ya wenzake.

Katika hafla hiyo, Mwenyekiti wa INEC, Jaji Jacobs Mwambegele alisema ibara ya 41(6) na (7) ya Katiba inafafanua kuwa mgombea wa kiti cha Rais atatangazwa kuwa amechaguliwa kuwa Rais iwapo akiwa amepata kura nyingi zaidi kuliko mgombea mwingine yeyote.

Jaji Mwambegele alimtangaza mgombea aliyeshinda uchaguzi wa kiti cha Rais, Samia, kwa kupata idadi ya kura 31,913,866 sawa na asilimia 97.66 ya kura 32,678,844 halali zilizopigwa.

Kura walizopata wagombea wengine ni kama ifuatavyo:

“Ibara hiyo inafafanua zaidi kwamba, mgombea wa kiti cha Rais, akitangazwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi kuwa amechaguliwa kuwa Rais hakuna mahakama yoyote itakayokuwa na mamlaka ya kuchunguza kuchaguliwa kwake,” alisema Mwambegele wakati wa hafla hiyo.

Mwambegele alitoa shukrani kwa wananchi, wapigakura, wagombea na vyama vyote vya siasa vilivyoshiriki katika uchaguzi huo kwa  kuiwezesha Tume kukamilisha majukumu yake “kwa ufanisi mkubwa.”

“Shukrani za pekee nizitoe kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wadau wa uchaguzi ambao kwa namna moja au nyingine, wameiwezesha Tume kuratibu, kuendesha, kusimamia na kukamilisha mchakato wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 kwa salama na amani,” alisema.

Akizungumza baada ya kukabidhiwa cheti na Mwenyekiti wa Tume, Samia alieleza kwamba ushindi alioupata si wake pekee, bali ni wa Watanzania wote na kwamba uchaguzi huo ulikuwa “kipimo cha ukomavu wa demokrasia nchini”.

“Uchaguzi huu haukuwa tu kipimo cha uungwaji mkono wa sera na maendeleo ya vyama vya siasa, bali pia ulikuwa kipimo cha ukomavu wa demokrasia nchini. Hivyo, ushindi huu si wa mgombea mmoja au chama kimoja, ni ushindi wetu sote Watanzania kama taifa,” alisema.

Samia ambaye alikuwa mgombea wa Chama cha Mapinduzi (CCM), alivishukuru vyombo vya ulinzi na usalama kwa kuhakikisha kwamba vurugu zilizotokea siku ya uchaguzi “hazikuathiri au kusimamisha uchaguzi”.

“Matukio yale yaliyofanywa kwenye maeneo, hasa kwenye miji ya Dar es Salaam, Arusha, Mwanza, Mbeya na Songwe, kwa vyovyote vile, hayakuwa ya kiungwana na ya kizalendo. Mzalendo hujenga nchi na siyo kubomoa nchi iliyojengwa kwa nguvu na jasho la wananchi.

“Serikali inalaani na kukemea vikali matukio yale…kwenye suala la usalama wa nchi na Taifa la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hakuna mbadala, bali ni kutumia mbinu zote za kiulinzi na kulibakisha taifa likiwa salama,” alisema Rais Samia.

Novemba 3, 2025, Rais Samia, aliapishwa kuwa Rais kwa miaka mitano ijayo, akiwa wa kwanza mwanamke kuapishwa baada ya uchaguzi mkuu, tofauti na alipoapishwa Machi 19, 2021 baada ya kifo cha mtangulizi wake.

Hafla ya uapisho wa kiongozi huyo iliyofanyika kwenye viwanja vya kamisheni , Ikulu Chamwino, ilihudhuriwa na wageni mbalimbali akiwamo Rais wa Zambia, Hakainde Hichilema, Rais wa Burundi, Evariste Ndayishimiye, Rais wa Somalia, Hassan Sheikh Mohamud, Rais wa Msumbiji, Daniel Chapo na Naibu Rais wa Kenya, Kithure Kindiki.

Kwenye shughuli hiyo Rais Samia aliingia uwanjani akapigiwa mizinga 21 na kukagua gwaride la heshima kama kiongozi anayemaliza muda wake huku bendera ya Rais ikishushwa.

Baada ya kula kiapo, Rais Samia alikagua gwaride kwa mara nyingine lililokuwa katika umbo la Alpha kuashiria mwanzo wa utawala wake huku bendera ya Rais ikipandishwa tena na kupigiwa tena mizinga 21.

Akizungumza baada ya kuapishwa, Rais Samia pamoja na mambo mengine alizungumzia vurugu zilizotokea na umuhimu wa kurejesha amani.

Alisema vurugu na uvunjifu wa amani huishia kupimana nguvu na uwezo wa kujihami, lakini mazungumzo huzaa mshikamano.

Sambamba na hilo, aliwaonya wote waliochochea uvunjifu wa amani, huku akiweka msisitizo kwenye umuhimu wa njia ya mazungumzo badala ya vurugu.

Kauli hiyo ya Samia inakuja siku chache baada ya kutokea vurugu zilizohusisha wananchi walioandamana na kuharibu baadhi ya miundombinu ya umma, wakishinikiza uchaguzi usifanyike.

Miongoni mwa vilivyoharibiwa ni vituo vya mabasi yaendayo haraka baadhi vikichomwa moto na vingine kupasuliwa vioo, kuchomwa moto kwa magari binafsi ya wananchi na maduka.

Hatua hiyo, ilisababisha Serikali itangaze marufuku ya wananchi kutotembea mitaani baada ya saa 12 jioni. Vikosi vya ulinzi na usalama pekee ndivyo vilivyopewa ruhusa ya kuzunguka kulinda amani nyakati hizo.

Katika hotuba yake hiyo, Samia alisema wote wanaoitakia mema nchi wamesikitishwa na kuhuzunishwa na matukio ya uvunjifu wa amani, upotevu wa maisha na uharibifu wa mali za umma na zile za watu binafsi.

Alieleza kilichotokea hakiendani na taswira na sifa za Kitanzania na sio Utanzania.

“Haikutushangaza kuona kuwa baadhi wa vijana waliokamatwa kutokana na kadhia hiyo wametoka nje ya Tanzania. Vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vinaendelea kufuatilia na kuchunguza kwa undani kilichotokea,” alisema Samia.

Alizisihi kamati za ulinzi na usalama za kitaifa, mikoa na wilaya kuirudisha nchi katika hali iliyozoeleka na kwamba kuanzia Novemba 3, 2025 maisha ya wananchi yarejee mara moja.

Alitoa onyo kwa wote waliochochea uvunjifu wa amani na aliwataka watambue kuwa vurugu na uvunjifu wa amani huishia kupimana nguvu na uwezo wa kujihami, ila mazungumzo huzaa mshikamano.

“Tuchague lenye manufaa kwetu, kwani usalama wa Taifa lolote hulindwa na wote kwa nguvu na gharama zozote,” alisisitiza.

Alitumia jukwaa hilo kueleza kuwa kipindi cha kampeni Taifa liligawika kiitikadi na kishabiki, lakini baada ya mchakato huo anayechaguliwa na wengi huwa ndio chaguo la nchi na anapaswa kuwa mtumishi wa waliomchagua, waliochagua wagombea wengine na hata ambao hawakushiriki uchaguzi.

“Kwa sisi tuliochaguliwa, ahadi yetu ni kulitumikia Taifa hili kwa nguvu zetu zote, vipawa vyetu vyote na maarifa yetu yote. Niwasihi tuendelee kuilinda itikadi yetu ya umoja na mshikamano,” alisema.

Samia alitumia jukwaa hilo kuwashukuru watazamaji wa uchaguzi wakiwemo kutoka Umoja wa Afrika (AU), Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc) na waangalizi wa kimataifa huku akisema ushauri wao ameupokea lakini maagizo ya nini cha kufanya hawatayapokea.

Katika hilo, alimnukuu Rais wa awamu ya tatu, hayati Benjamin Mkapa akisema: “nawashukuru watazamaji wa kimataifa kuja kushuhudia uchaguzi wetu ulivyofanyika, walipotusifia tumepokea sifa hizo kwa unyenyekevu. Tumesikia pia waliyodhani hayakwenda sawa na mengine hata sisi tumeyaona. Maagizo yao tumeyakataa, ushauri wao tutauzingatia ili tufanye vizuri zaidi siku zijazo.”

Alisema sifa moja ya mwanadamu ni kutokukamilika, aliyekamilika bila kasoro yoyote ni Mungu pekee. Ndio maana, katika shughuli au harakati za wanadamu wanaunganishwa na mawasiliano, mazungumzo na maelewano.

Alisema demokrasia haipimwi kwa nani kashinda uchaguzi, bali kwa jinsi tunavyoendesha mambo yetu baada ya uchaguzi.

“Tutakuwa na nguvu zaidi pale kila sauti, chanya na hasi, zinaposikilizwa, kuheshimiwa na kuthaminiwa, na vilevile, tunapoweza kuponya penye maumivu. Hii si kazi ya upande mmoja wa Serikali peke yake, bali ni kwa kila jumuiya za wananchi, chama cha siasa, dini zetu na kila mwananchi.

“Na hapa, nitumie fursa hii, kuwashukuru kwa dhati ya moyo wangu viongozi wa dini waliohimiza amani na upendo katika kipindi chote cha uchaguzi,” alieleza.

Rais Samia alisema uchaguzi huo ulikuwa na wagombea 17 kutoka vyama mbalimbali vya siasa wote wakiwania nafasi ya urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Napenda kuwashukuru wenzangu 17 ambao kwa hakika mmeonyesha ukomavu wa kidemokrasia kwa kuendesha kampeni ambazo tulishindana kwa hoja, na sote tulionyesha, kuwa siasa sio vita. Tumemaliza vyema uchaguzi na kumpongeza aliyeshinda,” alisema.

Awali, akizungumza katika hafla hiyo, Rais wa Zambia, Hainde Hichilema alisema amewahi kuwa mpinzani nchini mwake na kushindwa uchaguzi mara kadhaa lakini alitumia njia ya majadilino hadi akaingia ikulu.

Pamoja na kushawishika kuingia barabarani, alisema hakufanya hivyo na alikuwa wa kwanza kupingana na hilo, akisema kuandamana si suluhu ya matatizo, bali mazungumzo ndiyo suluhu.

Kwa upande wake Rais wa Burundi, Everist Ndayishimiye alitumia jukwaa hilo kumpongeza Rais Samia kwa ushindi katika uchaguzi, huku akiahidi kuendelea kushirikiana na Tanzania kama ilivyo historia ya mataifa hayo.

Katika hafla hiyo pia, Mwenyekiti wa Makanisa ya Kipentekoste Tanzania (CPCT), Askofu Vernon Fernandes alisema Taifa limegawanyika na mioyo ya watu imejeruhiwa kwa namna mbalimbali.

Alimwomba Rais Samia kulileta Taifa pamoja na kuiponya mioyo hiyo na kwamba alifanye hilo kuwa kipaumbele chake.

“Umepokea jukumu kubwa la kihistoria. Taifa limegawanyika na mioyo ya watu imejeruhiwa kwa namna mbalimbali. Ombi langu kwako kwa niaba ya umma wa Tanzania ulilete Taifa pamoja na kuiponya mioyo hii, hili likiwa kipaumbele chako,” alisema.

Mufti wa Tanzania, Sheikh Aboubakar Bin Zubeir alitumia jukwaa hilo kumshukuru Mungu kwa hatua ya kumfanya Rais Samia kuwa mkuu wa nchi kwa kipindi cha pili.

Alisema kwa kuwa uamuzi huo unamhusisha Mungu, basi binadamu hawana sababu ya kuwa radhi na hicho kilichotokea.

“Tumepokea na kukubali bila kigegezi, uchaguzi wako wewe Mungu na uamuzi wako na kwa ihklasi tunakiri kuwa tuko radhi, ilimradi wewe Mungu uko radhi naye,” alisema.

Kwa upande wa ubunge, tayari matokeo ya uchaguzi huo yametangazwa ambapo Mwananchi limefanikiwa kupata majina ya washindi wa uchaguzi huo katika baadhi ya majimbo, licha ya changamoto ya mtandao.

Katika Mkoa wa Songwe, wagombea wote wa CCM wameshinda kwenye majimbo yote, wagombea hao na majimbo yao ni Philipo Mulugo (Songwe), Japhet Hasunga (Vwawa) na Onesmo Mkondya (Mbozi). Wengine ni Kondesta Sichalwe (Momba), Godfrey Kasekenya (Ileje) na David Silinde (Tunduma).

Katika Mkoa wa Mbeya, Washindi wote pia ni wa CCM, ambao ni Dk Tulia Ackson (Uyole), Patrick Mwalunenge (Mbeya Mjini), Baraka Mwamengo (Kyela), Lutengano Mwalwiba (Busokelo), Anthony Mwantona (Rungwe), Bahati Ndingo (Mbarali) na Patali patali (Mbeya Vijijini).

CCM, pia kimenyakua majimbo yote katika Mkoa wa Njombe, wagombea waliochaguliwa ni Joseph Kamonga (Ludewa), Deo Mwanyika (Njombe mjini), Daniel Chongolo (Makambako), Festo Dugange (Wanging’ombe), Edwin Swalle (Lupembe) na Festo Sanga (Makete).

Huko Arusha, wagombea wa CCM wameshinda ambao ni Isack Joseph (Monduli), Daniel Awakii (Karatu), Paul Makonda (Arusha Mjini), Yannick Ndonyo (Ngorongoro) na Dk Steven Kiruswa (Longido).

Huko Manyara, walioshinda ni James Ole Millya (Simanjiro), Asia Halamga (Hanang), Emmanuel Nuwas (Mbulu Vijijini), Zacharia Isaay (Mbulu Mjini)