Dar es Salaam. Ni mtikisiko kwenye sekta ya elimu, hivi ndivyo inavyoweza kuelezwa kufuatia vurugu zilizotokea siku ya uchaguzi Oktoba 29, 2025 kusababisha mabadiliko ya ratiba mbalimbali muhimu zinazohusu sekta hiyo.
Miongoni kwa ratiba zilizobadilishwa ni ile ya Baraza la Taifa la Mitihani (Necta) iliyohusisha mtihani ya upimaji wa kidato cha pili na mtihani wa Taifa wa kidato cha nne.
Mabadiliko hayo yamefanya mtihani wa kidato cha Pili uliopaswa kufanyika kuanzia Novemba 3, 2025 kusogezwa mbele hadi Novemba 10, 2025.
Ratiba nyingine iliyosogezwa mbele ni ya mtihani wa Taifa wa kuhitimu kidato cha nne uliopaswa kuanza Novemba 17 sasa utafanyika kuanzia Novemba 24.
Panga pangua hiyo haikuishia kuathiri elimu ya sekondari pekee, imegusa pia taasisi za elimu ya juu ikihusisha vyuo vikuu na vya kati ambavyo vilipaswa kufunguliwa kuanzia Novemba 1, 2025.
Tangazo lililotolewa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia limewataka wanafunzi wanaoendelea na masomo katika vyuo mbalimbali waliopaswa kuripoti vyuoni Novemba 3, 2025 kutofanya hivyo hadi pale itakapotangazwa tena.
Tangazo hilo limewahusu pia wanafunzi wa mwaka wa kwanza ambao walitakiwa kuripoti vyuoni kuanzia Novemba 1, 2025 kwa ajili ya kuanza masomo yao ya elimu ya juu na kati.
Mabadiliko ya ratiba yameigusa pia Bodi ya Wahasibu ambapo mitihani ya NBAA ya uhasibu kwa ngazi ya utunzaji vitabu (ATEC) na CPA nayo imesogezwa mbele.
Kwa mujibu wa ratiba ya awali mitihani hiyo ilipaswa kufanyika kuanzia Novemba 4 hadi 7 mwaka huu, lakini imesogezwa mbele na sasa itafanyika kuanzia Novemba 25 hadi 28.
Akizungumzia hali hiyo, mdau wa elimu Ochola Wayoga amesema mabadiliko hayo yanaweza yasiwe na athari kubwa endapo hali itatulia na mitihani itafanyika ndani ya muda mfupi baada ya kuhairishwa.
“Hili tulilishuhudia wakati wa janga la Uviko 19 shule zilifungwa na mitihani ikasogezwa mbele, hivyo si kitu kipya sana na madhara yake kwa upande mmoja yanaweza yasiwe makubwa sana, endapo itasogezwa kwa wiki moja kama ilivyoelezwa.
“Kwa upande mwingine hatuwezi kupingana na ukweli kwamba katika kipindi hiki ambacho watoto wamekaa nyumbani inawezekana wamekutana na vitendo vya ukatili na hata mimba ambazo zimepatikana kutokana na kuchangamana na watu wengi nyumbani, amesema.
Wayoga amesema katika kipindi hiki ambacho shughuli za kiuchumi zimesimama, upo uwezekano wapo watoto wakachelewa kurudi shuleni au hata kushindwa kwenda kufanya mtihani kwa kukosa mahitaji, muhimu zikiwemo fedha za usafiri.
Mbali na hilo Wayoga amesema mbali na hayo, upo uwezekano wa athari kubwa kujitokeza zaidi kutoka kwa wadau wa maendeleo wanaochangia kwenye sekta ya elimu.
“Hizi vurugu tunaweza kuzichukulia kawaida ila wenzetu wakaona kwa jicho lingine, ikionekana tumeshindwa kusimamia misingi ya utawala bora kama nchi wadau wa maendeleo, wanaweza kutuwekea vikwazo vitakavyoathiri sekta ya elimu moja kwa moja, ikizingatiwa bado tunategemea fedha za wahisani,”amesema Wayoga.
Kwa upande wake mshauri wa masuala ya elimu Dk Wilberfroce Meena amesema mabadiliko ya ratiba ya mtihani yanaweza kuwa na athari za kisaikolojia kwa walimu na wanafunzi.
“Kwa mtu aliyejiandaa kufanya mtihani siku fulani halafu muda ukasogezwa, kuna namna inaweza kuathiri ile kasi ya maandalizi na athari yake iko kisaikolojia zaidi, hili linaweza kutokea kwa wanafunzi wenyewe au hata walimu waliowandaa ila naamini mambo yatakaa sawa,” amesema.
Dk Meena amesema mabadiliko hayo ni kipimo cha uhimilivu wa mfumo wa elimu katika kuhakikisha uko tayari kukabiliana na majanga.
“Inaweza kuwa kipimo cha kuangalia namna wanafunzi walivyoandaliwa kukabiliana na changamoto zinapojitokeza. Je, waliandaliwa kisaikolojia kwamba majanga yanaweza kutokea, maana hili tunaweza kusema ni janga,” amesema.
Mkazi wa Kisemvule, Engebert Mwami ambaye ni mzazi, amesema hatua hiyo ya kusogeza ratiba ya mitihani hasa kwa wanafunzi wa sekondari imefanyika kwa usahihi.
“Kiukweli hakuna mzazi ambaye angekuwa na amani mtoto wake kuwa katika chumba cha mtihani katika hali hii, mimi mwanangu yupo kidato cha pili kwa hiki kilichofanyika naona ni busara ya hali ya juu, usalama kwanza hayo mambo mengine yanafuata.
“Kwa sababu hizi ratiba wanapanga wenyewe, sioni kama kuna kitu kitaharibika kwa sababu wote tunajua hali ilivyokuwa. Hivyo ni imani yangu mambo yatakwenda kwa utaratibu mzuri bila kuharibu ratiba ambazo zinapaswa kuanza Januari,” amesema Mwami.
Kwa upande wake Asha Sefu ambaye ni mwalimu wa shule ya sekondari, amesema ingawa suala la kusogeza ratiba halikutarajiwa lakini itasaidia kuondoa hofu kwa wanafunzi.
“Hatujawahi kuwa na hali hii, tuliwaandaa watoto wetu kwa ajili ya mitihani lakini tatizo kama hili limetokea, isingekuwa busara kuendelea na ratiba maana wapo ambao wangeingia chumba cha mtihani wakiwa na hofu na wengine wasingekuja kabisa.
“Hii ingesababisha hata ufaulu usiwe mzuri, lakini kwa hii wiki moja wanaweza kukaa sawa na sisi walimu na wazazi tukitumia kipindi hiki kuwajenga kisaikolojia na kuwaondolea hofu ili wafanye mitihani yao kwa utulivu,” amesema Asha.