Ahueni bei ya mafuta ikisalia ilivyokuwa Oktoba

Dar es Salaam. Watuamiaji wa vyombo vya moto nchini wataendelea kupata ahueni kwani bei za mafuta zitakazotumika Novemba, 2025 zitaendelea kusalia kama zilivyokuwa Oktoba mwaka huu, isipokuwa kwa petroli jijini Dar es Salaam.

Wanunuzi wa rejareja katika jiji la Dar es Salaam wataongeza Sh32 katika kila lita ya mafuta watakayonunua Novemba mwaka huu ikilinganishwa na mwaka uliotangulia.

Taarifa ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), iliyotolewa inaonyesha kuwa sasa wakazi wa Dar es Salaam watanunua lita moja ya petroli kwa Sh2,752 kutoka Sh2,720 iliyokuwa ikitumika Oktoba mwaka huu.

Kwa watumiaji wa dizeli wataendelea kutumia Sh2,704 kwa lita moja ya mafuta kama ilivyokuwa Oktoba na mafuta ya taa wakiendelea kutumia Sh2,774 kwa lita.

Kwa wanunuaji wa rejareja kwa mafuta yanayopita Bandari ya Tanga sasa watanunua petroli lita moja kwa Sh2,813 kutoka Sh2,868 iliyokuwapo Septemba mwaka huu, dizeli Sh2,766 huku mafuta ya taa yakisalia Sh2,835.

Kwa Bandari ya Mtwara, petroli itaendelea kununuliwa kwa Sh2,844, dizeli kwa Sh2,797 na mafuta ya taa yakiendelea kusalia kwa Sh2,866 kama ilivyokuwa Oktoba mwaka huu.

 Taarifa hii iliyosainiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Ewura, Dk James Mwainyekule imevitaka vituo vyote vya mafuta kuchapisha bei za bidhaa za mafuta katika mabango yanayoonekana bayana yakionyesha bei za mafuta, punguzo, vivutio vya kibiashara vinavyotolewa na kituo husika.

“Pale ambapo inawezekana kuchagua, wateja wanashauriwa kununua bidhaa za mafuta katika vituo vinavyouza kwa bei nafuu zaidi ili kushamirisha ushindani. Ni kosa kuuza mafuta bila kuweka mabango ya bei inayoonekana vizuri kwa wateja,” imeeleza taarifa hiyo.

Pia imewataka wauzaji wa bidhaa za mafuta ya petroli wanatakiwa kutoa stakabadhi za mauzo kutoka kwenye Electronic Fiscal Pump Printers (EFPP) na wanunuzi wahakikishe wanapata stakabadhi hizo za malipo zinazoonyesha jina la kituo, tarehe, aina ya mafuta yaliyonunuliwa na bei kwa lita.