ACT –Wazalendo wawatuliza wanachama | Mwananchi

Unguja. Baada ya kushindwa katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 29, 2025, aliyekuwa mgombea wa ACT-Wazalendo, Othman Masoud amewataka wanachama wa chama hicho kutulia wakati viongozi wakiendelea kutafakari.

Uchaguzi huo ulioshirikisha vyama 11 vya siasa, Dk Hussein Mwinyi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) aliibuka kidedea kwa kupata asilimia 74.8 ya kura zote zilizopigwa huku Othman akipata asilimia 23.22.

Akizungunza na viongozi na baadhi ya wanachama katika ofisi za chama hicho Vuga, Oktoba 31, 2025, Othman amesema licha ya kutokubaliana na matokeo hayo, lakini hawana budi kuwa na utulivu.

“Ndugu wanachama, tunaona yaliyotokea lakini niwaombe tutulie wakati viongozi tukiendelea kushughulikia jambo hili,” amesema.

Othman amesema jambo lolote litakalofanyika lazima watawashirikisha wanachama na hakuna uamuzi watakaoamua bila kupata baraka za wanachama.

“Kama ambavyo kila kinachofanyika tunakuwa kwenu kuomba ridhaa, hata hili hakuna uamuzi utakaotolewa na sisi viongozi, lazima tutakuja kwenu na ninyi mtakachokiamia ndio tutakachotekeleza,” amesema Othman akiwapoza wanachama na wafuasi wa chama hicho.

Wakati ACT – Wazalendo wakisema hayo, CCM imewashukuru na kuwapongeza wananchi wote kwa kuchagua viongozi wao kwa kura nyingi na kuendelea kuiweka madarakani.

Katibu wa Kamati Maalumu, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama hicho Zanzibar, Khamis Mbeto amesema chama hicho kinavikaribisha vyama vingine washirikiane kujenga uchumi wa Zanzibar.

“Tumeshinda kwa kishindo, hii ni kuonesha kwamba, mgombea wetu alikuwa anakubalika, lakini inaonesha jinsi ambavyo CCM imetekeleza ilani yake kwa asilimia kubwa, hivyo ikajenga imani kwa wananchi, uchaguzi umeisha sasa ni wakati wa kuendelea kuijenga nchi,” amesema Mbeto.

Majimbo waliyopoteza CCM na kuchukuliwa na ACT – Wazalendo ni  Mtambile, Shumba, Ole, Wete, Gando, Mtambwe, Pandani, Wingwi na Tumbe na Ziwani.