KLABU ya Yanga imetangaza kuwa, mechi zake za nyumbani katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu itatumia Uwanja wa New Amaan Complex uliopo Zanzibar.
Yanga imepangwa Kundi B pamoja na timu za Afrika Kaskazini ambazo ni Al Ahly ya Misri, JS Kabylie ya Algeria na AS FAR ya Morocco, imehamishia mechi hizo Zanzibar ikiachana na Uwanja wa Benjamin Mkapa uliopo Dar ilioutumia kwa mechi za hatua ya awali ilipocheza dhidi ya Wiliete ya Angola na Silver Strikers kutoka Malawi.
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga, Ally Kamwe, amesema: “Baada ya kufanyika tathmini ya kina na kwa maslahi mapana ya klabu yetu, napenda kuwatangazia kwamba mechi za Yanga katika hatua ya makundi zitafanyika katika kisiwa cha Unguja kwenye Uwanja wa New Amaan Complex.
“Nichukue fursa hii kuwaomba sasa mashabiki na wanachama wa Yanga katika visiwa vya Pemba na Unguja kuanza maandalizi ya haraka kuhakikisha tunafanya vizuri.”
Wakati mechi hizo za CAF ikihamishia Zanzibar, Yanga itautumia Uwanja wa KMC Complex kwa Ligi Kuu Bara na mashindano mengine ya ndani.
Kitendo cha Yanga kuhamia Zanzibar, inaifanya kuwa timu ya tatu ya Tanzania Bara kuutumia uwanja huo kwa mechi za CAF msimu huu baada ya Singida Black Stars na Azam zinazoshiriki Kombe la Shirikisho Afrika.
CAF imetangaza tarehe za mechi za hatua ya makundi ambapo Yanga itaanzia nyumbani kuikaribisha AS FAR kati ya Novemba 21 na 23, 2025, kisha itaifuata JS Kabylie kati ya Novemba 28 na 30, 2025.
Baada ya hapo, kutakuwa na kipindi cha kupisha michuano ya AFCON 2025, kisha hatua ya makundi itaendelea kati ya Januari 23 na 25, 2025, Yanga ikiwa tena ugenini kukabiliana na Al Ahly.
Kati ya Januari 30 na Februari 1, 2025, Yanga itarudiana na Al Ahly nyumbani, kisha itatoka kwenda kwa AS FAR kati ya Februari 6 na 8, 2025, itahitimisha hatua ya makundi kati ya Februari 13 na 15, 2025 ikiikaribisha JS Kabylie.