MSHAMBULIAJI wa Yanga, Clement Mzize amefanyiwa upasuaji wa goti na anatarajia kuwa nje ya uwanja kwa wiki nane hadi kumi.
Mzize ambaye alikuwa kinara wa mabao kwa wachezaji wazawa ndani ya Ligi Kuu Bara msimu uliopita akifunga mabao 14, huku akimaliza wa pili nyuma ya Jean Charles Ahoua wa Simba aliyefunga mabao 16, alipata majeraha wakati Yanga ikiichapa Wiliete SC ya Angola mabao 3-0 kwenye mechi ya awali Ligi ya Mabingwa Afrika.
Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Yanga kimeliambia Mwanaspoti kuwa baada ya mshambuliaji huyo kutonyesha jeraha ambalo lilimuweka nje kwa wiki tatu uongozi ulifanya uamuzi wa kumfanyia upasuaji na tayari jambo hilo limefanyika.
“Ni kweli Mzize amefanyiwa upasuaji wa goti ambalo kwa mujibu wa daktari atakaa nje ya uwanja kwa wiki nane hadi kumi hivyo hatutakuwa na huduma ya mchezaji huyo kwa muda huo,” alisema mtoa taarifa huyo na kuongeza;
“Upasuaji huo umezingatia vipimo vikubwa alivyofanyiwa haikuwa rahisi mchezaji kukubaliana na hilo, lakini msaada mkubwa wa wanasaikolojia na namna alivyojengwa na madaktari bingwa imechukua siku tatu kufanikisha jambo hilo baada ya mchezaji kukubali.”
Mtoa taarifa huyo alisema wanatambua umuhimu wa mchezaji huyo kwenye kikosi chake na hata timu ya taifa hivyo wanaamini baada ya upasuaji huo kama atafuata taratibu zote mara baada ya wiki nane hadi kumi atarejea uwanjani na kuendelea na majukumu yake kama kawaida.
Wakati hayo yakitokea kwa upande wa Mzize kikosi cha timu hiyo kimerudi kambini tayari kwa maandalizi ya mechi dhidi ya KMC inayotarajiwa kuchezwa Septemba 9 mwaka huu.