Dar es Salaam. Watuamiaji wa vyombo vitumiavyo petroli watendelea kutumia bei ileile kwa mwezi Novemba baada ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) kutangaza bei ya kikomo ambayo haijafanyiwa marekebisho yoyote ikilinganisha na mwezi ulioishia Oktoba 31, 2025.
Bei hiyo iliyotangazwa itahusu mafuta yote yanayopita katika bandari za Dar es Salaam, Tanga na Mtwara.
Taarifa ya Ewura iliyotolewa inaonyesha kuwa sasa wakazi wa Dar es Salaam watanunua lita moja ya petroli kwa Sh2,752 sawa na iliyokuwa ikitumika Oktoba mwaka huu.
Kwa watumiaji wa dizeli wataendelea kutumia Sh2,704 kwa lita moja ya mafuta kama ilivyokuwa Oktoba na mafuta ya taa wakiendelea kutumia Sh2,774 kwa lita.
Kwa wanunuaji wa rejareja kwa mafuta yanayopita Bandari ya Tanga sasa watanunua petroli lita moja kwa Sh2,813, dizeli Sh2,766 huku mafuta ya taa yakisalia Sh2,835.
Kwa Bandari ya Mtwara, petroli itaendelea kununuliwa kwa Sh2,844, dizeli kwa Sh2,797 na mafuta ya taa yakiendelea kusalia kwa Sh2,866 kama ilivyokuwa Oktoba mwaka huu.
Taarifa hii iliyosainiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Ewura, Dk James Mwainyekule eendelea kuvitaka vituo vyote vya mafuta kuchapisha bei za bidhaa za mafuta katika mabango yanayoonekana bayana yakionesha bei za mafuta, punguzo, vivutio vya kibiashara vinavyotolewa na kituo husika.
“Pale ambapo inawezekana kuchagua, wateja wanashauriwa kununua bidhaa za mafuta katika vituo vinavyouza mafuta kwa bei nafuu zaidi ili kushamirisha ushindani. Ni kosa kuuza mafuta bila kuweka mabango ya bei inayoonekana vizuri kwa wateja,” imesema taarifa hiyo.
Pia imewataka wauzaji wa mafuta Wauzaji wa bidhaa za mafuta ya petroli wanatakiwa kutoa stakabadhi za mauzo kutoka kwenye Electronic Fiscal Pump Printers (EFPP) na wanunuzi wahakikishe wanapata stakabadhi hizo za malipo zinazoonyesha jina la kituo, tarehe, aina ya mafuta yaliyonunuliwa na bei kwa lita.
