Wabunge wateule waitwa Dodoma, kumpata Spika mpya moto

Dodoma. Rais Samia Suluhu Hassan kwa mamlaka aliyopewa na Katiba ya nchi, amewaita wabunge wateule wote jijini Dodoma kuanzia Novemba 8,2025.

Taarifa iliyotolewa kwa umma na Katibu wa Bunge Barala Leonard, Tangazo la Rais la kuitisha Bunge lililotolewa kwenye Gazeti la Serikali toleo maalumu Na. 11 (Special Supplement) la tarehe 4 Novemba, 2025.

Bunge la 13 litaanza rasmi baada ya kukamilika kwa Uchaguzi Mkuu wa Rais, wabunge na madiwani uliofanyika Oktoba 29, 2025 ambao kwa nafasi ya Rais Samia Suluhu Hassan aliibuka mshindi.

“Tangazo Na. 647A wabunge wateule wote wanafahamishwa kwamba shughuli za usajili na taratibu nyingine za kiutawala zitafanyika Ofisi ya Bunge Dodoma kuanzia tarehe 8 hadi 10 Novemba, 2025,” inasema sehemu ya barua iliyosainiwa na Katibu wa Bunge.

Kwa mujibu wa barua hiyo, kikao cha kwanza cha mkutano wa kwanza wa Bunge la 13 kitafanyika tarehe 11 Novemba, 2025 kama ilivyotamkwa kwenye Tangazo la Rais; ambapo shughuli zitakazofanyika katika Mkutano huo zimetajwa.

Miongoni mwa shughuli hizo ni kusomwa tangazo la Rais la kuitisha Bunge, uchaguzi wa Spika, kiapo cha uaminifu kwa wabunge wote na kuthibitisha uteuzi wa Waziri Mkuu.

Shughuli nyingine zitakuwa, uchaguzi wa naibu Spika; na ufunguzi rasmi wa Bunge jipya utakaofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Leonard amewata wabunge wateule kufika viwanja vya Bunge Dodoma wakiwa wamevaa mavazi rasmi kwa ajli ya zoezi la usaili na upigaji picha na wabebe nyaraka ikiwemo hati ya kuchaguliwa/kuteuliwa kwa mbunge, Kitambulisho cha Taifa na nakala yake, kadi ya benki yenye namba ya akaunti ya mbunge, cheti halisi cha ndoa kinachotambuliwa na Serikali (kwa wenye ndoa) na nakala yake.

Nyaraka zingine ni vyeti halisi vya kuzaliwa vya watoto wenye umri chini ya miaka 21 (kwa wenye watoto/wasiozidi wanne) na nakala vyeti halisi vya elimu/taaluma vyenye ithibati ya taasisi husika na nakala zake lakini wawe na wasifu wa mbunge (Curriculum Vitae).