26,093 wakacha mtihani darasa la saba, asilimia 81.8 wakifaulu

Dar es Salaam. Wakati Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) likitangaza matokeo ya mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi yanayoonesha ufaulu kuongezeka kwa asilimia 0.93 ikilinganishwa na matokeo ya mwaka 2024, jumla ya wanafunzi 26,093 hawakufanya mtihani huo licha ya kusajiliwa.

Idadi  ya wanafunzi ambao hawakufanya mtihani ni ongezeko kidogo ikilinganishwa na wanafunzi 25,875 wa mwaka uliopita.

Hata hivyo, wanafunzi hao ni upungufu wa asilimia 57 ikilinganishwa na 40,901 ambao hawakufanya mtihani, mwaka 2023.

Baraza hilo pia limefuta matokeo yote ya watahiniwa 38 wakiwamo 31 waliobainika kufanya udanganyifu katika mtihani na wengine saba walioandika lugha ya matusi katika skripti zao.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu mtendaji wa baraza hilo, Dk Said Mohamed jumla ya watahiniwa 1,172,324 walisajiliwa kufanya mtihani huo, lakini 26,093 sawa na asilimia 2.23 hawakufanya, wavulana wakiwa 15,078 na wasichana 11,015.

Taarifa hiyo imewashtua wadau wa elimu ambao wameeleza kuwa, ipo haja kwa Taifa kufanyia tathmini ya ufanisi wa mfumo wa elimu kubaini kinachowafanya wanafunzi kukatisha masomo yao.

Akizungumza na Mwananchi mtaalamu wa masuala ya elimu, Dk Wilberfoce Meena amesema idadi hiyo ni kubwa na haipaswi kuangaliwa kwa kwa jicho la kawaida kwa sababu inatengeneza kundi kubwa la watu wasio na maarifa.

“Tumekuwa tukilalamikia hili suala la wanafunzi kukatisha masomo yao na ilikuwa tatizo kubwa kwa shule za sekondari, miaka ya karibuni linazidi kuongezeka na sasa linashuka kwa kasi katika shule za msingi idadi hii ya wanafunzi ambao hawajafanya mtihani.

“Hii inaonesha ufanisi wa mfumo wa elimu uko chini, mfumo bora wa elimu ni ule ambao idadi ya walioandikishwa na wanaohitimu inalingana lakini ukifuatilia hawa unaweza kukuta wakati wanaandikishwa darasa la kwanza walikuwa wengi, lakini wapo walioshia njiani hata kabla ya kufikia hatua ya kusajiliwa kufanya mtihani wa darasa la saba,” amesema.

“Maana yake tunakwenda kuongeza idadi ya watu wasiokuwa na maarifa na hii inatuondoa kwenye dhamira yetu ya kutengeneza jamii iliyoelimika kama ambavyo dira 2025 inavyotuelekeza.”

Kufuatia hali hiyo, Dk Meena ameshauri mamlaka na taasisi zinazohusika na mfumo wa elimu kueleza kwa kina wanakoelekea wanafunzi wanaokatisha masomo bila kujali uchache wao.

“Hiyo namba ukiiangalia kwa asilimia unaweza kusema ni kidogo, lakini uhalisia ni kwamba hata mtoto mmoja ana maana na muhimu kwa Taifa, baada ya Necta kutoa taarifa hii nafikiri ifike wakati mamlaka zinazohusika ikiwamo wizara itupe maelezo kuhusu kundi hili la watoto linakwenda wapi,”amesema Dk Meena.

Amesema kuna ushahidi wa wazazi kuwazuia watoto wasifanye vizuri kwenye mitihani yao ili wasifaulu, hivyo upo uwezekano sasa wanawazuia wasiende kabisa kufanya mitihani hiyo.

Kwa upande wake Mkuu wa Shule ya Moga, Leonard Ntimba amesema tatizo limeanza kuota mizizi huku waathirika wakubwa wakiwa ni watoto kutoka katika shule za umma.

Amesema hilo ni matokeo ya kupungua kwa msukumo kwa wazazi kupeleka watoto shuleni licha ya Serikali kutekeleza mpango wa elimu bila ada.

“Msukumo wa kuwapeleka watoto shule umepungua kwa kiasi kikubwa tofauti na ilivyokuwa hapo awali, nafikiri kuna haja ya kuwa na sheria itakayosimamia vikali suala hili na wazazi wachukuliwe hatua.  Serikali isiishie kusema elimu bure ichukue hatua kwa wazazi wanaoshindwa kuwafuatilia watoto kupata elimu.

“Nasema hivi kwa sababu, siku hizi imekuwa si kitu cha ajabu kukuta watoto wenye umri wa kuwa shuleni wanazurura tu mitaani, wazazi hawana muda wa kufuatilia; na naona hili suala la watoto kulelewa na mzazi mmoja linazidi kuongeza tatizo hakuna kabisa ufuatiliaji,” amesema Ntimba.

Katika mtihani huo uliofanyika Septemba 10 na 11, 2025 jumla ya watahiniwa 1,146,231 sawa na asilimia 97.77 walifanya mtihani wakiwamo wasichana 626,147 (asilimia 98.27) na wavulana 520,084 (asilimia 97.18).

Matokeo yanaonesha jumla ya watahiniwa 937,581 sawa na asilimia 81.80 ya watahiniwa 1,146,164 kwenye matokeo ya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi mwaka 2025 wamefaulu kwa kupata madaraja ya A, B na C.

Kuhusu ubora wa ufaulu, watahiniwa 422,923 sawa na asilimia 36.90 wamepata madaraja ya A na B ikiwa ni ongezeko la asilimia 1.07 ikilinganishwa na mwaka 2024.

Ubora wa ufaulu kwa wasichana umeongezeka kwa asilimia 0.70, mwaka 2025 umefikia asilimia 33.71 ikilinganishwa na asilimia 33.01 mwaka 2024.

Ongezeko hilo limechangiwa na kuimarika kwa ufaulu katika madaraja ya juu, daraja la A limeongezeka kwa asilimia 0.39 na daraja la B kwa asilimia 0.31 ikilinganishwa na mwaka 2024.

Kwa upande wa wavulana, ubora wa ufaulu nao umeongezeka kwa asilimia 1.52 hadi asilimia 40.73 ikilinganishwa na asilimia 39.21 mwaka 2024.

Ongezeko la ubora wa ufaulu limechangiwa na kuimarika kwa ufaulu katika daraja la A kwa asilimia 0.78 na daraja la B kwa asilimia 0.74 ikilinganishwa na mwaka 2024.

Necta pia imezuia kutoa matokeo ya watahiniwa 245 waliopata changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuugua, hivyo kushindwa kufanya mtihani kwa idadi kubwa ya masomo au masomo yote.

Hata hivyo, Dk Mohamed amebainisha kuwa watahiniwa husika wamepewa fursa ya kurudia kufanya Mtihani wa Kumaliza Elimu ya Msingi (PSLE) mwaka 2026 kwa mujibu wa Kifungu cha 32(1) cha Kanuni za Mitihani.