KIKOSI cha Singida Black Stars kinaondoka jijini Dar es Salaam kesho Alhamisi ili kuwahi pambano lijalo la Ligi Kuu Bara dhidi ya Pamba Jiji, huku kocha msaidizi wa timu hiyo, David Ouma akisema watakuwa na dakika 90 bora kusaka pointi tatu ugenini.
Singida ilikuwa jijini Dar es Salaam na kuweka kambi ya muda ikijiandaa na mechi dhidi ya Azam FC iliyokuwa ipigwe kupigwa Oktoba 30 kabla ya kuahirishwa na safari hii itakuwa CCM Kirumba, Mwanza dhidi ya Pamba iliyotoka kupewa ushindi wa mezani mbele ya Dodoma Jiji.
Akizungumza na Mwanaspoti, Ouma amesema kikosi hicho kilirejea mazoezini Jumanne kikifanya mazoezi kwa siku mbili kwenye Uwanja wa KMC Complez kabla ya leo kuanza safari kuifuata Pamba Jiji ikiwa ni mechi ya tatu kwa timu hiyo.
“Timu imerudi na wachezaji wapo katika hali nzuri maandalizi yaendelea vizuri na tumefanya mazoezi ya mwisho kabla ya safari ya kesho (leo) kwenda Mwanza tayari kwa mechi ya tatu wa ligi tukiwa na matarajio ya kuendelea tulipoishia,” amesema Ouma na kuongeza:
“Kila mchezaji anatambua umuhimu wa mchezo ulio mbele yetu na hatutarajii mchezo rahisi kutokana na rekodi nzuri kwenye mechi mbili za kwanza za ligi hivyo matarajio ni kuwa na dakika 90 za ubora kwa timu zote mbili.”
Ouma alisema malengo yao kama klabu ni kuwa na muendelezo mzuri wa kupata matokeo kwenye kila mchezo ili kuiweka timu kwenye ushindani ndani na kimataifa.
Akizungumzia droo ya michuano ya kimataifa, Ouma raia wa Kenya amesema hakuna kundi rahisi wameona timu walizopangwa nazo na wataendelea na mipango kuhakikisha wanakuwa na timu bora shindani bila kujali wanakutana na mpinzani wa aina gani.
“Huwezi kusema tuna kundi dhaifu au gumu kila timu iliyofika hatua hiyo ni bora na ndio maana imefika hapo ilipo hivyo mipango mikakati bora ndiyo itakayoamua ubora wa mpinzani tumejipanga kushindana na sio kushiriki.”