JKT Queens yaenda Misri kwa mafungu

WAWAKILISHI pekee wa Cecafa kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa wanawake, JKT Queens wameanza safari kwenda Misri inakofanyika michuano hiyo huku kundi la kwanza limeondoka leo Jumatano Novemba 5, 2025 na lingine la watu 11 litaondoka kesho Alhamisi.

JKT ilikata tiketi ya kushiriki michuano hiyo Septemba 2025, iliponyakua ubingwa wa Cecafa mbele ya Rayon Sports ya Rwanda iliyoichapa kwa bao 1-0 katika Uwanja wa Moi Kasarani jijini Nairobi Kenya.

Ubingwa huo ukaifanya kuwa moja kati ya timu nane zitakazoumana kuwania ubingwa wa Afrika kwa wanawake ikianzia makundi ambapo imepangwa kundi B na TP Mazembe (DRC Congo), Asec Mimosas (Ivory Coast) na Gaborone United (Botswana) huku kundi A likiwa na FC Masar (Misri), AS Far (Morocco), 15 de Agosto (Guinea ya Ikweta) na US FAS Bamako (Mali).

Akizungumza na Mwanaspoti, Kocha Mkuu wa JKT Queens, Abdallah Kessy amesema wachezaji 11 wameondoka leo, huku akiongeza kwamba watakuwa na siku tatu za maandalizi nchini Misri kabla ya kuivaa Gaborone United Novemba 9, 2025.

“Tulipata mechi za maandalizi Dar es Salaam hasa kwenye mechi ngumu za Simba Queens na Yanga Princess kwenye mashindano ya Ngao ya Jamii, ingawa sio kwa ukubwa lakini yalitupa nafasi ya kurekebisha mazoezini penye upungufu,” amesema.

“Tunaamini mashindano hayatakuwa rahisi kwa sababu ukiangalia makundi yote kila timu ilikuwa bingwa kwenye ukanda wake kasoro Mazembe ambao waliingia kama bingwa mtetezi hivyo tunayachukulia kwa uzito na tunaamini tutafanya vizuri.”

Hii ni mara ya pili kwa JKT Queens kushiriki kwani mara ya kwanza ilikuwa 2023 nchini Ivory Coast ambako iliishia hatua ya makundi. JKT Queens ndio timu pekee iliyocheza mashindano hayo mara nyingi Cecafa tangu Ligi ya Mabingwa ianzishwe 2021. Kwa ukanda huo Simba pekee ndio ilifika nusu fainali.