Azam FC yanogewa mapema CAF, Bosi atoa kauli ya kibabe

WAWAKILISHI wa Tanzania katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, Azam FC wameanza kunogewa mapema baada ya timu hiyo kufuzu makundi kwa mara ya kwanza hatua ya makundina mmoja wa vigogo ametamba msimu huu hadi kieleweke CAF.

Azam iliyoasisiwa 2004 ilitinga makundi CAF ikipangwa Kundi B sambamba na Wydad AC ya Morocco, Nairobi United ya Kenya na AS Maniema ya DR Congo, huku jina la kocha Florent Ibenge likiendelea kutajwa midomoni mwa vigogo wa timu hiyo.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mwenyekiti wa klabu hiyo, Nassor Idrissa ‘Father’ amesema Azam msimu huu ina mipango mingi mizuri ikiwemo kufanya vyema katika michuano ya kimataifa.

“Kama umeiangalia vizuri Azam unaona kabisa ina mabadiliko makubwa na hata inavyocheza wachezaji na klabu kwa ujumla inataka kufanya makubwa msimu huu. Ni furaha kubwa kwetu kama viongozi wa timu kutinga makundi. Sasa sio ndoto tena na imani yetu bado ni kubwa kwani uwezo wa kuendelea kufanya vizuri upo mkubwa,” amesema Father na kuongeza:

“Kundi ambalo tumepangwa nalo (CAF) si jepesi, lakini hakuna kinachoshindikana ni kujipanga tu, jambo ambalo tayari tumeshalifanya na tuna imani kubwa ya kufika mbali zaidi na hapo tulipofika kwa mara ya kwanza.”

Idrissa alisema kama kiongozi na klabu kwa ujumla wanajivunia kuwa na kocha mwenye uwezo mkubwa kama Ibenge.

“Tutafanya vikao na benchi la ufundi kuanza mipango na kubwa kabisa tunajivunia kuwa na Ibenge, ambaye ana uzoefu mkubwa wa mechi za hatua hii. Mungu atusaidie tutimize malengo tu maana kila kitu kipo sawa na wachezaji wote wako vizuri kwa ajili ya hatua inayofuata,” amesema Father.

Kabla ya Azam kuanza kucheza mechi hizo za kimataifa, itakuwa na mechi za ligi, ikijipanga kukutana na Namungo ugenini mjini Ruangwa Lindi mechi itakayopigwa Jumapili kwenye Uwanja wa Majaliwa.