Dar es Salaam. Wizara ya Maliasili na Utalii, imewataka watalii waliokuwa wamepanga kutembelea Tanzania kuendelea na mipango ili waweze kufurahia vivutio vilivyopo bila ya kuwa na hofu yoyote.
Imetoa wito huo baada ya hali ya amani na utulivu kurejea, huku shughuli mbalimbali za kijamii zikifunguliwa na watu kuendelea na majukumu yao ya kila siku kama kawaida katika maeneo yote nchini.
Shughuli za kiuchumi nchini zilirejea rasmi Novemba 4 ikiwa ni utekelezaji wa maagizo yaliyotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan alilolitoa Novemba 3 mwaka huu wakati akiapishwa kuongoza nchi kwa miaka mitano ijayo.
Samia aliapishwa baada ya kushinda katika uchaguzi uliofanyika Oktoba 29 mwaka huu kwa asilimia 97.66 licha ya baadhi ya Watanzania kuandamana kupinga uchaguzi huo hali iliyosababisha uharibifu wa mali na vifo.
Taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini wa Wizara ya Utalii na Maliasili, Nteghenjwa Hosseah imeeleza kuwa Tanzania kama Mwanachama wa Shirika la Utalii Duniani (UN Tourism), inatekeleza na kusimamia Mwongozo wa Utalii Kimataifa unaoelekeza nchi kuhakikisha usalama wa wageni, ikiwemo wasafiri na watalii wanaotembelea maeneo mbalimbali wawapo nchini.
“Kufuatia hilo, vituo vyote vya kuingia na kutoka nchini kupitia usafiri wa anga, barabara, maji, reli, sambamba na usafiri wa umma vinaendelea kutoa huduma kwa utaratibu wa kawaida. Aidha, shughuli za utalii na huduma kwa wageni zinaendelea kutolewa katika maeneo yote nchini kwa kushirikiana na sekta binafsi,” amesema.
Amesema Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaendelea kuwa nchi salama, yenye utulivu na mazingira rafiki kwa shughuli zote za usafiri, uwekezaji kibiashara na utalii na wanaendelea kuwakaribisha wageni wote nchini.
Takwimu zilizopo zinaeleza kuwa zinaeleza kuwa jumla ya watalii 1,285,876 walitembelea hifadhi za Taifa kati ya Julai 2024 hadi Aprili 2025 na kuwezesha Tanzania kukusanya Sh433.612 bilioni sawa na asilimia 100.64 ya lengo la makusanyo ya Sh430.864 bilioni kwa mwaka wa fedha 2024/2025.
Pia, idadi ya watalii waliotembelea maeneo yanayosimamiwa na mamlaka kwa ajili ya shughuli za utalii imeongezeka na kufikia watalii wa picha 209,522 ikilinganishwa na watalii 155,037 mwaka 2023/24 sawa na ongezeko la asilimia 35.14.
Wakati huo pia idadi ya wawindaji imeongezeka kufikia 530 ikilinganishwa na wawindaji 484 mwaka 2023/24 sawa na ongezeko la asilimia 9.5.