Unguja. Mkutano wa kwanza wa Baraza la 11 la Wawakilishi (BLW) Zanzibar unatarajiwa kuanza kesho Alhamisi, Novemba 6, 2025, ambapo wagombea wanne kutoka vyama vya CCM, UDP, ADC na NLD wanatarajiwa kuchuana kuwania nafasi ya Spika wa Baraza hilo atakayeliendesha kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.
Baraza limepokea majina manne kutoka Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) ambao wanatarajia kupigiwa kura.
Wagombea hao na vyama vyao kwenye mabano ni pamoja na anayetetea nafasi yake, Zubeir Ali Maulid (CCM), Naima Salum Hamad (UDP), Suleiman Ali Khamis (ADC) na Chausiku Khatib Mohamed (NLD).
Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za baraza hilo leo Novemba 5, 2025 Katibu wa BLW, Raya Issa Msellem ametaja shughuli zingine zitakazofanyika kesho ni pamoja na kiapo cha uaminifu cha spika na kiapo cha uaminifu cha wajumbe wote.
“Pia, atachaguliwa Naibu Spika ambayo ni miongoni mwa shughuli za mkutano wa kwanza zilizoelekezwa na kifungu cha 74 (2) cha Katiba ya Zanzibar na kanuni ya 19 (1) ya kanuni za kudumu za baraza la wawakilishi, toleo la 2024,” amesema.
Raya amesema mkutano huo wa baraza unaofanyika kwa mujibu wa kifungu cha 90 (1) cha Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 kinachoweka masharti ya kuitisha baraza jipya baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu sio zaidi ya siku 90 tangu kuvunjwa kwa baraza.
Kifungu cha 89 (1) kinaeleza kwamba mkutano wa baraza utakuwa sehemu yoyote visiwani Zanzibar na utafanyika wakati wowote ambapo Rais ataamuru.
Amesema kufuatia masharti ya Katiba na kanuni za kudumu za Baraza la Wawakilishi, Rais amepeleka taarifa ya kuliita baraza kesho.
Akielezea sifa za mgombea uspika, Mkurugenzi wa Shughuli za Bunge, Othman Ali Haji, amesema awe anatokana na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi au mtu mwingine mwenye sifa za kuwa Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi.
“Kwa mujibu wa kifungu cha 68 cha Katiba ya Zanzibar, pia anatakiwa awe Mzanzibari, umri wake usiwe chini ya miaka 21 na awe anatokana na chama cha siasa,” amesema Othman Ali Haji.