Zungu kumvaa Dk Tulia uspika, wapinzani wajipanga

Dodoma. Joto la kuwania kiti cha Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania linazidi kupamba moto ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) huku mchuano mkali ukiwa ni kati ya viongozi wanaomaliza muda wao, Spika, Dk Tulia Ackson na Naibu Spika, Mussa Zungu.

Wakati mchuano huo ukiwa ndani ya CCM, baadhi ya vyama vya upinzani navyo vinaendelea na vikao vya uteuzi wa wagombea wake huku chama cha ACT Wazalendo kikieleza bayana kwamba hakitasimasha mgombea. Spika wa Bunge huchaguliwa na wabunge kwenye kikao cha kwanza cha mkutano wa kwanza wa wa uhai wa Bunge.

Hadi pazia linafungwa kwa CCM jana Jumanne Novemba 4, 2025, Spika aliyemaliza muda wake, Dk Tulia na Zungu walikuwa wameshachukua fomu za kuwania ya kiti hicho katika ofisi za chama hichi jijini Dodoma.

Wengine waliochukua fomu kwa nafasi hiyo ni mbunge wa zamani wa Shinyanga, Stephen Masele na Peter Frank (Mr Black).

Jana, Mwenyekiti wa CCM, Rais Samia Suluhu Hassan aliongoza kikao maalumu cha kamati kuu ambacho pamoja na mambo mengine, kilifanya uteuzi wa wagombea wa nafasi za Spika na Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Spika na Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar.

Chanzo kimoja ndani ya chama hicho kinaeleza kwamba kamati kuu iliteua majina matatu kuwania nafasi ya uspika ambayo ni Dk Tulia, Zungu na Masele ambayo yatapigiwa kura na wabunge wa CCM kumpata mmoja.

Dk Tulia anatetea nafasi hiyo ambayo aliipata baada ya kujiuzulu Job Ndugai, wakati huo yeye akiwa Naibu Spika. Kwa upande wa Zungu, kabla ya kuwa Naibu Spika, amehudumu kwa muda mrefu kama mwenyekiti wa Bunge.

Uchaguzi wa Spika wa Bunge ni hatua ya kukamilisha mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa Rais, wabunge na madiwani uliofanyika Oktoba 29, 2025 na tayari Rais Samia Suluhu Hassan ameitisha Bunge la 13 kuanza vikao vyake, vitakavyoanza kwa kumchagua Spika.

Kwa mujibu wa Katiba ya nchi Ibara ya 86(1) na Kanuni za Kudumu za Bunge Toleo la Februari 2023, 9(1) na (2), chama cha siasa kitakuwa na haki ya kupendekeza jina moja la mbunge ambaye atakuwa mgombea wa kiti cha Spika kwa mujibu wa Katiba.

Kwa wagombea wasiokuwa wabunge, majina yao yatawasilishwa na vyama husika kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi siku tano kabla ya tarehe ya uchaguzi wa Spika na Tume itayachambua na kuyawasilisha kwa Katibu wa Bunge siku mbili kabla ya siku ya uchaguzi.

Kwa upande wa Naibu Spika, waliochukua fomu na kupitishwa ni watatu kati yao walishahudumu kama wenyeviti wa Bunge –Najma Giga na Daniel Sillo wakati sura mpya kwenye nafasi hiyo ikiwa ya  mbunge wa Korogwe Vijijini, Timotheo Mzava.

Ukiacha mchuano ndani ya CCM, baadhi ya vyama vya upinzani, pia vimethibitisha kujipanga kushiriki uchaguzi wa Spika na Naibu Spika.

Akizungumza na Mwananchi, Mwenyekiti wa chama cha Alliance for Democratic Change (ADC), Shabani Itutu amethibitisha kwamba chama hicho kimeteua makada kuwania nafasi hizo.

Chama kingine kinachojipanga kukiwania kiti hicho ni National Reconstruction Alliance (NRA) ambacho kimeeleza kwamba kiko kwenye vikao vya uteuzi.

“Sisi NRA hatujawahi kuacha nafasi ya uwakilishi wa wananchi. Tunajipanga, tupo katika vikao vya uteuzi wa wagombea ili wabebe ajenda yetu ya kuleta mageuzi makubwa katika chombo hicho kikuu cha uwakilishi wa wananchi,” amesema Hassan Almas, Katibu Mkuu wa NRA ambaye pia alikuwa mgombea urais kupitia chama hicho.

Kwa upande wake, Msemaji wa chama cha Tanzania Labour Party (TLP), Bakari Makame amesema chama hicho kinaendela na michakato ya ndani kupata jina la mgombea wa kiti cha Spika wa Bunge la 13.

“TLP tupo vizuri, tunamalizia michakato yetu ya ndani na tukikamilisha tutawasilisha jina la mgombea wetu bora kabisa ambaye ataenda kuwania kiti cha Spika ili kuongoza Bunge kwa masilahi ya wananchi,” amesema.

Katibu Mkuu wa chama cha Democratic Party (DP), Felix Makuwa amethibitisha kuwa chama hicho ni miongoni mwa vyama vinavyowania uongozi wa Bunge hilo.

“DP tunashiriki, tumepokea barua ya Tume, tupo katika maandalizi ya ndani na punde tutakapokamilisha tutawasilisha majina ya wagombea wetu,” amesema.

Wakati vyama hivyo vikijiandaa, Msemaji wa chama cha ACT Wazalendo, Shangwe Ayo amesema chama hicho hakiweki mgombea wa kiti cha Spika kwani kinaamini hakiwezi kushinda na hakitaki kufanya maagizo.

Shangwe licha ya kupata wabunge wanne kwa upande wa Bara na wengine Zanzibar, idadi yao haiwezi kuwashawishi wapiga kura kuwachagua, hivyo wamejipanga kuanza na mikakati ya kuwatumikia wananchi badala ya kuwaza kitu ambacho ni vigumu kukipata.

Akitoa maoni juu ya nani anaweza kuwa Spika kwa masilahi ya Bunge, Katibu Mkuu wa Chama cha Kutetea Haki na Maslahi ya Walimu Tanzania (Chakamwata), Meshack Kapange amesema hakutakuwa na jipya katika sura za wabunge kutoka chama kimoja.

Kapange amesema kuwa hata akiingia Spika mzuri lakini mfumo ulivyo kwa Bunge la walio wengi kutoka chama kimoja, itakuwa ni sawa na kazi bure.

Mchungaji wa Kanisa la EAGT Gairo, Egbert Lyoka amesema Watanzania wasitegemee kuwa na mabadiliko makubwa kutokana na aina ya watu walioomba na jinsi Bunge la 12 lilivyokuwa, kwani ni walewale na mambo ni yaleyale, hakuna mabadiliko.