Dar es Salaam. Waangalizi wa uchaguzi wa Tanzania uliofanyika Oktoba 29, 2025, wametoa mapendekezo ya kuboresha chaguzi zijazo, ikiwemo kufanya mageuzi ya mfumo wa uchaguzi ili kutoa haki na kukuza demokrasia nchini.
Ujumbe wa Waangalizi wa Uchaguzi (SEOM) unaowakilisha Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Umoja wa Ulaya (EU) ni miongoni mwa waangalizi wa kimataifa waliotoa taarifa zao za awali kufuatia uchaguzi huo.
Katika taarifa zao, waangalizi hao wameeleza kuguswa na uchaguzi huo kutokana na mambo mbalimbali waliyoyaona, huku wakipendekeza masuala mbalimbali yakiwemo mabadiliko ya mfumo wa uchaguzi.
Hata hivyo, Serikali imeeleza kwamba uchaguzi mkuu ulifanyika kwa uwazi wa hali ya juu na kwa kufuata kikamilifu misingi ya kidemokrasia. Imesisitiza kuwa wananchi wa Tanzania walitumia haki yao ya kikatiba kwa kupiga kura kwa amani.
Wakati Serikali, kupitia taarifa ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mahmoud Thabit Kombo, ikieleza hayo, Rais Samia Suluhu Hassan alipozungumza baada ya kuapishwa Novemba 3, alitumia maneno ya hayati Benjamin Mkapa (Rais Mstaafu) akisema:
“Nawashukuru watazamaji wa kimataifa kuja kushuhudia uchaguzi wetu ulivyofanyika. Walipotusifia, tumepokea sifa hizo kwa unyenyekevu. Tumesikia pia waliyodhani hayakwenda sawa, na mengine hata sisi tumeyaona… Maagizo yao tumeyakataa, ushauri wao tutauzingatia ili tufanye vizuri zaidi siku zijazo.”
Katika taarifa yao ya awali, SEOM imeeleza haja ya kufanya mageuzi ya mfumo wa uchaguzi. Inabainisha kuwa Ibara ya 41(7) ya Katiba, inayohusu taratibu za uchaguzi wa Rais, inasema kwamba:
“Iwapo mgombea atatangazwa na Tume ya Uchaguzi kuwa amechaguliwa ipasavyo kwa mujibu wa ibara hii, basi hakuna mahakama yoyote itakayokuwa na mamlaka ya kuchunguza uchaguzi wa mgombea huyo.”
SEOM imebainisha kwamba kifungu hicho kinaondoa mamlaka ya mahakama yoyote kusikiliza pingamizi lolote dhidi ya matokeo ya uchaguzi wa urais, jambo ambalo ni kinyume na matarajio ya haki ya uchaguzi kama ilivyowekwa katika Ibara ya 4.1.5 ya kanuni na miongozo ya SADC inayoongoza uchaguzi wa kidemokrasia.
Wakati huohuo, waangalizi hao wameeleza kwamba wadau wengine waliokutana nao walionesha mashaka yao kuhusu uhuru wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), kwa kuwa wajumbe wake huteuliwa na Rais, ambaye pia ni mwenyekiti wa chama tawala na mgombea wa urais.
SEOM imebainisha pia kwamba wapo wadau waliokuwa na wasiwasi kuhusu upigaji kura wa mapema kwa maofisa wa usalama, unaofanyika Zanzibar pekee. Wadau hao walihisi utaratibu huo unaweza kuwa tishio kwa uadilifu wa uchaguzi na ukawa chanzo cha udanganyifu.
“Kwa kuzingatia hayo, Serikali na Bunge zinahimizwa kutoa kipaumbele kwa mchakato jumuishi wa mapitio ya Katiba ya nchi ili kupata maoni ya umma kuhusu njia bora za sasa na zijazo,” imeeleza taarifa hiyo ya awali iliyowekwa kwenye tovuti rasmi ya SADC.
Njia bora zilizopendekezwa na waangalizi hao ni pamoja na kuruhusu wagombea binafsi (wasio wanachama wa vyama vya siasa), kuruhusu uwasilishaji wa mashauri ya uchaguzi yanayohusu uchaguzi wa urais na kuruhusu ukaguzi wa kimahakama wa baadhi ya maamuzi ya taasisi za usimamizi wa uchaguzi.
Kutokana na mazingira magumu waliyokumbana nayo wakati wa kutekeleza majukumu yao, SEOM imehimiza INEC na maofisa wa usalama kuchukua hatua kuhakikisha kwamba waangalizi wa kimataifa wa uchaguzi wanapewa vibali kwa wakati.
Kwa upande wao, EU imeeleza wasiwasi wake kutokana na matukio yaliyotokea katika kipindi chote cha siku ya uchaguzi na yanayoendelea, yakiwemo matukio ya vurugu, kuzimwa kwa mtandao wa intaneti, pamoja na taarifa za dosari katika mchakato wa uchaguzi katika maeneo kadhaa.
Katika taarifa yake ya Novemba mosi, 2025, Waziri Kombo alisema uadilifu wa uchaguzi wa mwaka huu unahusishwa na mageuzi yaliyotambuliwa na kutekelezwa na wadau wote, vikiwemo vyama vya siasa na asasi za kiraia.
Amesema miongoni mwa mageuzi muhimu ni kuanzishwa kwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) na mapitio ya mifumo ya kisheria ya uchaguzi iliyokuwepo.
“Katika tukio la kusikitisha lililotokea mwishoni mwa mchakato wa upigaji kura, kuliripotiwa matukio machache ya uvunjifu wa amani na sheria katika baadhi ya maeneo ya nchi.
“Ili kudumisha utulivu, vyombo vyetu vya usalama vilichukua hatua za haraka, kitaalamu na kwa ufanisi kukabiliana na hali hizo, kuhakikisha kwamba matukio hayo ya hapa na pale hayakuenea wala kuvuruga mchakato mzima wa uchaguzi,” amesema katika taarifa hiyo.