Dar es Salaam. Vurugu zilizotokea kwenye baadhi ya maeneo nchini wakati wa uchaguzi mkuu, ziliathiri uendeshaji wa Mahakama ya Tanzania kwa kuwa ilishindwa kutekeleza majukumu yake na kuvuruga ratiba yake.
Vurugu hizo ambazo zimeacha kumbukumbu mbaya ziliambatana na matukio mengine ikiwamo kuzimwa kwa mtandao nchini kote kwa muda wa siku sita tangu siku ya kupiga kura Oktoba 29 mpaka Novemba 3, 2025 ulipoanza kurejeshwa kwa kiasi fulani.
Mbali na kuzimwa kwa mtandao, siku ya kupiga kura pia makundi ya vijana katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam, Mbeya, Mwanza na baadhi ya mikoa, yaliingia mitaani kwa madai ya kudai haki kwenye uchaguzi.
Kuzimwa kwa mtandao kualiathiri mhimili huo kwa kuwa ni mojawapo ya taasisi zilizopiga hatua kubwa katika matumizi ya teknolojia katika utendaji kazi zake, ikiwa ni pamoja na uendesheaji wa kesi.
Mara nyingi, Mahakama imekuwa ikiendesha kesi kwa kutumia teknolojia ya mtandao inayoiunganisha na wadau wake, wakiwemo wadaawa (pande husika katika kesi) pamoja na mawakili, kutoka maeneo tofauti pale mazingira yanapokuwa hayaruhusu kukutana ana kwa ana mahakamani au kunapokuwepo sababu za msingi.
Kesi zote zilizokuwa zimepangwa kuendelea siku moja baada ya uchaguzi ambayo ilikuwa ni siku maalumu ya mapumziko kwa ajili hiyo, siku iliyofuata, Alhamisi Oktoba 30 na kuendelea, zilikwama.
Katika utaratibu wa Mahakama, kila kesi inapangiwa tarehe maalumu kutegemeana na nafasi iliyopo. Kuna majaji na mahakimu ambao ratiba zao huwa zimejaa hata kwa kipindi cha miezi miwili au zaidi.
Kesi mpya au iliyopangwa kusikilizwa kwa usikilizwaji kamili (ushahidi au hoja za kisheria), ikikosa nafasi hiyo kwa tarehe iliyopangiwa, inaweza kupangiwa baada ya muda mrefu.
Hivyo, kesi hiyo inaweza kupangiwa tena baada ya mwezi mmoja, miwili au zaidi, kulingana na nafasi iliyopo, isipokuwa zile za dharura, hasa za jinai ambazo upelelezi wake haujakamilika, kwani kisheria zinapaswa kutajwa kila baada ya siku 14 kuangalia mwenendo wa upelelezi huo.
Wadaawa ambao kesi zao zilipangwa kusikilizwa kwa tarehe zilizokwama kutokana na athari za uchaguzi huo, watalazimika kusubiri kwa muda zaidi kulingana na tarehe mpya watakazopangiwa.
Miongoni mwa kesi hizo zilizokwama kuendelea kutokana na athari za uchaguzi huo ni kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu.
Kesi hiyo, ambayo inaendelea kusikilizwa na Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Dar es Salaam katika hatua ya ushahidi wa upande wa mashtaka, ilisimama kwa muda kupisha uchaguzi na ilipaswa kuendelea kuanzia Novemba 3.
Lakini kutokana na athari hizo za uchaguzi huo, ilikwama, hivyo sasa inasubiri kupangiwa tarehe nyingine ya kuendelea kusikilizwa, ratiba ambayo inaweza kutoka muda wowote kuanzia sasa.
Wasemavyo wadau wa sheria
Deogratias Butawantemi, wakili wa Mahakama Kuu, amesema suala la uchaguzi liliambatana na kuzimwa kwa mtandao wa intaneti ambao uliathiri shughuli za kimahakama na mahabusu
Butawantemi amesema kwa mujibu wa Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai(CPA), inaeleza mshtakiwa aliyepo mahabusu ambaye hana dhamana au ameshindwa kupata dhamana kwa sababu mbalimbali anatakiwa kila baada ya siku 14 apelekwe mahakamani ili apate taarifa mpya kuhusiana na kesi yake.
Hivyo, kitendo cha watuhumiwa kushindwa kupelekwa mahakamani kipindi hicho, kisheria ilikuwa ni athari kubwa.
“Kitendo cha washtakiwa kushindwa kupelekwa mahakamani katika tarehe husika ambazo zinaangukia kuanzia Oktoba 30, Oktoba 31, Novemba 3, 2025 na hadi Novemba 4, 2025, watuhumiwa hao wanakuwa wanakaa rumande kwa amri ya nani? Ikiwa sheria inaelekeza kila baada ya siku 14 washtakiwa wanatakiwa kupelekwa mahakamani,” amesema Butawantemi na kuongeza:
“Mfano mimi nilikuwa na kesi Novemba 3, 2025, mteja wangu alitakiwa apelekwe mahakamani akitokea mahabusu kwa ajili ya kesi yake kutajwa na kujua upelelezi umefikia hatua gani, lakini siku hiyo hakuletwa, sasa hiyo dharura ya kisheria tunaiweka kwenye amri gani? Na inatolewa na kwa amri ya nani? Kwa sababu mtuhumiwa anaendelea kukaa mahabusu bila kuwa na utaratibu wa Mahakama wala Jeshi la Magereza, hivyo unaweza kuona athari ilivyo.”
Amebainisha athari nyingine ni usumbufu katika mfumo wa mahakama kutokana na kukosekana kwa intaneti.
“Nilitakiwa kusajili kesi Tabora kwa njia ya mtandao na nilipewa muda maalumu wa kusajili kesi hiyo, lakini kutokana na kukoseka kwa intaneti nimeshindwa, hivyo natakiwa kurudi tena mahakama ili nipewe tarehe nyingi kwa ajili ya kusajili. Hali hii inafanya kuwepo na mlundikano wa kesi na usumbufu kwa mteja,” amesema Butawantemi.
Amefafanua kuwa Mahakama ya Tanzania inatumia mfumo wa Tehama kusikiliza mashauri mbalimbali kwa njia ya mtandano, hivyo kuzimwa kwa intaneti kumsababishia kesi hizo zishindwe kuendelea ua kutolewa uamuzi.
“Mahakama kwa sasa imepiga hatua katika teknolojia na sasa inatumia mtandao kuendesha baadhi ya kesi zake, sasa suala la mtandao wa intaneti kuwa chini na kusuasua unaweza ukaona hali hiyo imeathiri kesi nyingi ambazo zingesikilizwa na kutolewa uamuzi,” amesema Wakili Butawantemi.
Kwa upande wake, Wakili wa Mahakama Kuu, Edson Kilatu ameungana na Butawantemi na kueleza kuwa sintofahamu hiyo katika kipindi cha uchaguzi imesababisha athari kubwa, huku akianisha sababu tano.
Kilatu amezitaja athari hizo kwanza ni suala la kiusalama, akisema huduma za kimahakama zinahitaji usalama, kwani bila hivyo hazitafanyika.
“Lazima kuwepo kwa usalama, watu wapate utulivu wa kutosha, lakini vyombo vya ulinzi na usalama lazima wajihakikishie usalama ndipo hata mahabusu wapelekwe mahakamani,” amesema na kuongeza:
“Hali hii sio tu imeathiri Mahakama, hata mawakili tumeathiriwa na, kwa mfano mimi nilikuwa na kesi Jumatatu Novemba 3, 2025 mkoani Morogoro nimeshindwa kwenda, leo (jana) nilikuwa na kesi Dodoma nimeshindwa kwenda kutokana na kutokuwepo kwa usafiri wa uhakika, hivyo unaweza kuona mazingira ya kimiundo mbinu ya usafiri bado yamekuwa ni changamoto.”
Akizungumzia suala la mtandano kusuasua na wakati mwingine kutokuwa na nguvu, Kilatu amesema kukosekana kwa intaneti imara kumekwamisha baadhi ya nyaraka muhimu kushindwa kusajiliwa katika mfumo wa mahakama.
“Mpaka sasa mtandao wa intaneti haujawa imara, bado unasuasua na hali hii imesababisha baadhi ya nyaraka za wateja nimeshindwa kutuma na kuzisajili katika mfumo wa Mahakama,” amesema Kilatu.
Kutokana na vurugu zilizotokea wakati wa uchaguzi, nyanja mbalimbali ziliathirika ikiwemo ya uchumi, kutokana na kusimama kwa shughuli za uzalishaji mali na utoaji huduma katika sekta za umma na binafsi, kulikosababishwa na kukosekana kwa huduma wezeshi.
Mbali na kuzimwa kwa mtandao, siku ya kupiga kura pia makundi ya vijana katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam, Mbeya, Mwanza na baadhi ya mikoa, yaliingia mitaani kwa madai ya kudai haki kwenye uchaguzi.
Katika baadhi ya maeneo, vijana hao waliharibu miundombinu na mali za umma na binafsi, hivyo kusababisha sintofahamu baina yao na vyombo vya dola vilivyokuwa vikiwadhibiti, hatua iliyohatarisha usalama na hata uhai wa watu katika baadhi ya maeneo.
Kutokana na hali hiyo iliyoashiria uvunjifu wa amani, Jeshi la Polisi lilitoa tangazo la zuio la wakazi wa Dar es Salaam kutotembea baada ya saa 12 jioni. Serikali, kupitia Katibu Mkuu Kiongozi, iliwaelekeza watumishi wa umma kufanyia kazi nyumbani, isipokuwa wale ambao kwa asili ya kazi zao wanalazimika kuwepo ofisini.
Pia, iliwashauri waajiri katika sekta binafsi kuwaelekeza wafanyakazi wao kufanyia shughuli zao nyumbani.