Dar es Salaam. Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limetangaza nafasi za ajira katika kada tofauti likiwaalika Watanzania wenye sifa stahiki kutuma maombi yao.
Lengo ni kuongeza nguvu kazi na kuboresha utendaji wa sekretarieti ya Bunge.
Kwa mujibu wa tangazo lililotolewa jana Jumatano, Novemba 5, 2025 na Katibu wa Bunge, nafasi hizo zimeundwa kwa mujibu wa Ibara ya 62(1) na 88(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, ambazo zinalipa Bunge mamlaka ya kuwa na sekretarieti yake yenye jukumu la kuliwezesha kutekeleza majukumu yake ipasavyo.
Nafasi zilizotangazwa ni pamoja na Mkutubi Daraja la II (nafasi 2), Fundi Sanifu Mifumo ya Maji Daraja la II (2), Mtakwimu Daraja la II (2), Ofisa Ugavi Daraja la II (1), Ofisa Sheria Daraja la II (3), na Ofisa Habari Daraja la II (3).
Nyingine ni Ofisa Tehama (System Administrator) (1), Ofisa Utafiti Daraja la II (3), Mpokezi Daraja la II (4), Ofisa Tehama ( Network Administrator) (1) na Mwandishi Taarifa Rasmi za Bunge (Isimu ya Lugha) (1),
Nafasi zingine ni Mwandishi Taarifa Rasmi za Bunge (Uhazili) (2), Mhasibu Daraja la II (2), na Ofisa Usimamizi wa Fedha Daraja la II (1).
Aidha, tangazo hilo limeeleza waombaji wote wanatakiwa kuwa Raia wa Tanzania wenye umri usiozidi miaka 45, isipokuwa wale walioajiriwa tayari serikalini.
Pia, waombaji wenye ulemavu wamehimizwa kuomba na kutaja aina ya ulemavu walionao kwenye mfumo wa maombi.
Katibu wa Bunge amesisitiza waombaji wote wanapaswa kuambatanisha barua ya maombi iliyoandikwa kwa mkono na kusainiwa, pamoja na vyeti vya taaluma vilivyothibitishwa na Mwanasheria au Wakili, ikiwemo cheti cha kuzaliwa, vyeti vya kidato cha nne na sita (kwa waliofikia kiwango hicho), vyeti vya kitaaluma na kompyuta, kulingana na sifa za nafasi husika.
Vilevile, hati za matokeo (testimonials, provisional results, au statement of results) hazitakubalika, na waombaji waliosoma nje ya nchi wanapaswa kuhakikisha vyeti vyao vimehakikiwa na kuthibitishwa na mamlaka husika kama TCU, NECTA au NACTE.
Tangazo hilo pia limeonya utoaji wa taarifa au vyeti vya kughushi ni kosa la kisheria litakalosababisha hatua kali kuchukuliwa dhidi ya watakaobainika.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mwisho wa kutuma maombi ya kazi ni tarehe 18 Novemba, 2025, na barua za maombi zinapaswa kupelekwa kwa Katibu wa Bunge, Ofisi ya Bunge Dodoma.