Dar es Salaam. Matukio yaliyotokea wakati na baada ya uchaguzi mkuu yameshuhudiwa na kila mmoja wetu. Wapo waliopoteza miasha, kupata ulemavu wa kudumu, waliopoteza mali na baadhi ya miundombonu kuharibiwa. Swali linalobaki sasa tunatokaje?
Umuhimu wa jawabu la swali hili unatokana na ukweli kwamba, hakuna uwezekano wa kurudisha siku nyuma ili kuzuia kilichotokea. Hivyo, tufanyeje tutoke tulikofika?
Oktoba 29, 2025, ni siku ambayo haitasahaulika kwa Watanzania kwa sababu matukio hayo yalihusisha vurugu, uvunjifu wa amani na kubadili mtindo wa maisha.
Matukio hayo yalihusisha kuchoma moto baadhi ya miundombinu ikiwemo vituo vya polisi, ofisi za Serikali za mitaa, vituo vya mabasi yaendayo haraka, ofisi za CCM, vituo vya mafuta, maduka, magari na nyumba za viongozi wa kisiasa.
Ili tutoke tulipofika, ni muhimu kama Taifa tuanze kwa kujibu swali: tupo tayari kutoka hapo? Kama inavyoelezwa na wanazuoni, wachambuzi wa siasa, wanahabari wakongwe na viongozi wa dini waliozungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti.
Mwanazuoni wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Conrad Masabo, amesema swali la tunatokaje linapaswa kujibiwa na kila Mtanzania, kuanzia viongozi wa juu wa Serikali hadi raia wa kawaida.
“Wajibu wa kutoka tulipo ni wa kila Mtanzania, lakini kiwango cha uwajibikaji kitapishana kulingana na dhamana aliyonayo mtu kwenye nchi,” amesema.
Mwanazuoni huyo amesema mkulima hawezi kuwa na dhamana sawa na mwanasiasa, polisi au kiongozi wa dini, kwani kila mmoja ana dhamana yake.
Ikishajulikana kuna utayari, amesema ni muhimu kukubali kilichotokea, tukiri tumekosea, na katika hilo asinyooshewe kidole yeyote, makosa yabebwe na kila Mtanzania.
“Nimeona tumeanza kufanya siasa za kunyoosheana vidole kutafuta nani alikosea. Lazima wote tukubali kwamba hilo ni kosa letu. Tukubali zilitokea vurugu, uharibifu wa mali na upoteaji wa maisha, tusikwepe chochote kati ya hayo,” amesisitiza.
Ameongeza kuwa hatua hiyo ifuatiwe na kupita mitaani, kuchukua rekodi ya waliopoteza maisha na kuhakikisha watu wahifadhiwa kwa mujibu wa imani na tamaduni zao.
“Hicho kitatoa cultural healing (uponyaji wa kiutamaduni). Kwa sababu kwetu mtu kufa ni tatizo, lakini litakuwa tatizo zaidi iwapo hatazikwa kwa utaratibu wa kiimani au kitamaduni,” amesema.
Mwanazuoni huyo ameeleza kuwa, hatua itakayopaswa kufuata ni kuandaa mpango wa angalau kufuta machozi familia za wafiwa na waliopoteza mali, ingawa haina thamani sawa na uhai wa mtu, lakini inaonesha kuthamini na kujali.
Kisha, amesema waliohusika kwa namna yoyote, kuanzia kuhamasisha, kubeza hadi kutekeleza kilichotokea wawajibishwe bila kujali ni raia au kiongozi.
Mwanahabari mkongwe, Absalom Kibanda, amesema kuna haja kwa Rais Samia Suluhu Hassan kutimiza ahadi yake ya kuunda Tume ya Ukweli na Maridhiano sambamba na kufuta kesi zote za kisiasa.
“Kwa mara nyingine Rais Samia akubali kurudi alipoanzia (mwaka 2021). Binafsi naona Samia aliyeingia madarakani ni tofauti na yule aliyemaliza muhula wa kwanza mwaka 2025, ni Samia wawili tofauti. Lazima Rais Samia arudi katika msingi alioanza nao,” amesema.
Kibanda, aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), amesema: “Kingine, Rais Samia akubali kujiweka kando na watu au mambo yote ambayo kwa namna moja au nyingine yalimrudisha kule ilikokuwa Serikali ya awamu ya tano. Lazima Serikali ikomeshe vitendo vya watu kukamatwa kinyume cha sheria, kupotea na kutekwa.”
Ameongeza kuwa ni wakati mwafaka kwa Serikali kujitafakari na kuhakikisha inaachia uhuru wa watu kutoa maoni bila hofu, na vyombo vya habari kufanya kazi kwa uhuru.
Aidha, Kibanda amesema Serikali ihakikishe inazitambua familia za watu walioumia, kujeruhiwa au kupoteza maisha wakati wa vurugu zilizoanza Oktoba 29, na kuweka utaratibu wa kuwafidia ili kuwafuta machozi.
Novemba 3, 2025, katika hotuba yake ya kwanza baada ya kuapishwa, Rais Samia aliahidi kuendeleza falsafa ya 4R, za kujenga upya (Rebuild), maridhiano (Reconciliation), mageuzi (Reform) na ustahimilivu (Resilience).
“Kama mnavyofahamu, katika kuliunganisha Taifa, Serikali ya awamu ya sita tulianza na falsafa ya 4R’s inayosimamia misingi ya kuzungumza na kuelewana, kuvumiliana, kujenga Taifa letu na kubadilisha mwelekeo baada ya maelewano.
“Tunapoendelea mbele, hatutachoka wala kurudi nyuma katika kusimamia yote yanayohusu kujenga umoja na mshikamano wa Taifa letu,” alisema Rais Samia.
Mwanahabari mwingine, Jesse Kwayu amesema kabla ya kuwaza kuhusu Taifa linavyoweza kutoka hapa lilipofikia, ni lazima Watanzania wafahamu nini kilisababisha kufikia hali hiyo.
Katika maelezo yake. Kwayu amedai kuwa huenda kuna mambo au maoni na ushauri uliotolewa na wadau mbalimbali kuhusu mwenendo wa uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, lakini yakapuuzwa.
Hata hivyo, amesema ili Taifa litoke hapo lilipofikia lazima kurudi katika meza ya mazungumzo ili kupata mwafaka wa pamoja kwa maslahi ya Taifa.
“Asikwambie mtu jambo la kwanza turudi mezani ili hayo yanayolalamikiwa yafanyiwe kazi, yakifanyiwe kazi watu watatoka na mioyo iliyonyooka na watakwenda sawasawa na waliokubaliana.
“Hakuna kitu kinachozidi mazungumzo katika dunia ya leo, mazungumzo ni muhimu tena yenye nia ya kweli ili mioyo ifunguke. Tunatokaje hapo, lazima turejee kwenye meza wadau wote wazungumze,” ameeleza Kwayu.
Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa), Dk Rose Reuben, amesema chama hicho kinaendelea kusisitiza umuhimu wa kulinda utu wa binadamu, kuheshimu haki za kila mmoja na kudumisha mazungumzo ya amani kama nguzo muhimu ya Taifa.
Amesisitiza, kulinda amani na mshikamano ni jukumu la kila Mtanzania, ili kuondoa hofu na kuimarisha mshikamano wa kijamii.
“Tunaendelea kusisitiza umuhimu wa kulinda utu, kuheshimu haki za binadamu na kudumisha mazungumzo ya amani kama nguzo ya Taifa letu,” amesema Dk Reuben.
‘Hatua gani zinachukuliwa’
Mchambuzi wa siasa na jamii, Kiama Mwaimu, amesema kilichotokea si kizuri kwa sababu kilitishia usalama wa raia na nchi, lakini ili Taifa litoke hapo, Serikali inapaswa kueleza hali halisi na hatua zilizochukuliwa.
“Pia Serikali inapaswa kukaa pamoja tena na wadau wa vyama vya siasa, asasi za kiraia, viongozi wa madhehebu ya dini na makundi ya vijana ya pande zote. Wajadili kwa kina ilikuaje Taifa likafikia hatua hii, tatizo ni nini?” amesema.
“Lengo la vikao hivi ni kutoka na mtizamo mmoja kwa maslahi ya Taifa ili tufike mahali tuwe na uelewa wa pamoja. Tanzania tuna bahati ya kutokuwa chembe chembe za ukabila wala udini, kilichotokea siku zilizopita kiliwajumuisha wote,” amesema Mwaimu.
Mwaimu ametaadhalisha endapo suala hilo, lisiposhughulikiwa kwa ufanisi, huenda siku zijazo matendo hayo yakajitokeza na kuchukua mkondo wa kidini na kikabila, jambo ambalo ni hatari zaidi wa Taifa.
“Lilitokea linapaswa kufanyiwa kazi kikamilifu ili tuwe na ajenda moja ya kitaifa,” amesisitiza Mwaimu.
Wakati Mwaimu akieleza hayo, mchambuzi mwingine wa siasa, Said Miraji, amesema Serikali inapaswa kurudisha umoja wa kitaifa na usalama wa raia ili kila mmoja amuone mwenzake ana thamani.
“Tusifike mahali Watanzania tukagawanywa, kwamba mtu anayeshabikia CCM na kupiga kura anaonekana mbaya au asiyekwenda kupiga kura akachukuliwa yeye ni Chadema na anapinga uchaguzi.
“Wapo watu ni CCM, lakini wana mitizamo tofauti na yanayofanyika au wengine ni wapinzani lakini pia wana mitizamo tofauti pia. Tufike mahali kila mmoja ajione ana haki na wajibu na usalama na mwenzake,” amesema Miraji.
Ameongeza kuwa usalama si jukumu la vyombo vya dola pekee bali ni wajibu wa kila Mtanzania.
Miraji pia ameeleza kuwa Serikali inapaswa kutambua kiini cha matatizo ya vijana na kushughulikia si ajira pekee bali pia fursa nyingine zilizopo.
Katika mazungumzo yake, Miraji ameungana na Mwaimu, akisema maridhiano ya kitaifa yanahitajika kwa Serikali kukaa na kuzungumza na makundi tofauti ikiwemo vyama vya siasa, asasi za kiraia, mashirika yasiyokuwa ya kiserikali na viongozi wa dini na kimila, wanazuoni ili kuwa mjadala wa kitaifa.
“Hii si kazi ya CCM pekee, wala Serikali au wale wengine… bali kila mmoja ana umuhimu wa kushirikishwa ili ajione ana wajibu. Asilimia 90 ya Watanzania ni waumini wa dini wakisikia viongozi wao wanavyosema kwenye madhabauni au msikitini wanafuata,” amesema Miraji.
Profesa Ali Makame amesema vyombo vinavyohusika vinapaswa kufanya tathmini ya mambo yaliyotokea na kuchukua hatua stahiki.
“Jambo lingine tunapaswa kujifunza siasa sio njia pekee ya kuleta mabadiliko na mageuzi, mageuzi ya maendeleo hayaletwi na demokrasia ya vyama, ukiangalia vyama ina waumini wachache kuliko idadi ya raia waliopo nchini,” amesema.
Profesa Makame amesema japo siasa inatumika kwa nafasi yake katika demokrasia kupata viongozi, lakini viongozi hao huongozwa na mipango, mikakati kuwaletea wananchi mabadiliko wanayohitaji.
Amesisitiza viongozi hawapaswi kuona changamoto zilizopo nchini suluhisho ni kuondoa kwa vyama vya siasa bali ujumuishaji wa sekta mbalimbali.
“Tusitumie siasa kuathiri maendeleo ya nchi, kuhujumu au kuharibu haisaidii hata maendeleo tunayoyataka hatutayapata kwa njia hiyo. Tuangalie ni kipi kinaweza kututoa kwenye manunguniko, malalamiko na tuende kwenye mazingira ya kidemokrasia,” amesema.
Walichosema viongozi wa dini
Rais wa Mitume na Manabii Tanzania, Joshua Mwantyala, amesema watawala wanapaswa kuzifanyia kazi changamoto zilizotokea kwa kushirikisha wadau wote.
“Tunapaswa kufanya utafiti kwanini hizi changamoto zimetokea, kama Taifa tunapaswa kushirikisha makundi yote kwenye jamii bila kuchagua makundi fulani, waliothirika ni watu wa chini. Hivyo lazima wapewe nafasi ya kuzungumza,” amesema.
Katika ushauri wake wa nini kifanyike, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT), Sheikh Alhad Mussa Salum, amesema Tanzania imeingia kwenye mtihani mkubwa, hivyo inapaswa kusimama imara kuukabili.
“Changamoto imetokea, tuone namna ya kurejesha hali tuliyoizoea. Sio jambo la busara kuharibu nchi. Ni busara viongozi wa dini na Serikali kukaa kwa lengo moja la kuijenga Tanzania,” amesema.
Sheikh Alhad amewataka viongozi kuwa na sikio la usikivu kuangalia malalamiko ya wananchi na wananchi kujifunza kufuata utaratibu na kutii mamlaka zilizopo.
“Kwa pamoja kila mtu akishika ncha yake, Tanzania itarudi mahali ambapo tulitarajia, haya tuliyopitia tupokee kama tulipitia,” amesema.
“Tulidhani haiwezekani kwenye nchi yetu lakini Mungu akatuonyesha inawezekana kwahiyo tusidharau haya yanayotokea. Tuyafanyie kazi kwa kufuata utaratibu ili tuwe salama wote,” amesema.
Katibu Mkuu wa CCT, Mchungaji Moses Matonya, amesema meza ya mazungumzo ni muhimu kwa sababu watu wamepoteza maisha, wengine kujeruhiwa na mali nyingi kuharibiwa.
“Tunatoa pole kwa yaliyotokea. Baada ya pole, ndipo tuseme tunafanya nini. Sasa hivi kuna hali ya kulaumiana na kunyoosheana vidole. Inapaswa tukae chini na tuangalie kilichotokea kupitia meza ya mazungumzo,” amesema.
Amesema viongozi wa dini wako tayari kuratibu mazungumzo baina ya Serikali, viongozi wa kisiasa na vijana ili kupata suluhisho la pamoja.
Amesema kama ilivyofanyika kupitia kikosi kazi ni muhimu kuangalia matakwa ya kundi la vijana ambao kwa kiasi kikubwa wapo mtaani baada ya kuhitimu vyuo, wengi wao wakilalamikia ukosefu wa ajira.
Katibu Mkuu wa Baraza la Waislam Tanzania (Bakwata), Sheikh Nuhu Mruma, amesema jambo la muhimu ni Watanzania kutambua kuwa uchaguzi umeshapita na viongozi wameshapewa dhamana.
“Sasa ni jukumu la viongozi waliopatikana kuongoza Watanzania na kurejesha yale yaliyokwenda vibaya. Wenye malalamiko wasikilizwe, lakini watoe hoja kwa busara na si kwa vurugu,” amesema Sheikh Mruma.
Mbali na hilo, Sheikh Mruma amewaomba Watanzania kuendelea kumuomba Mungu ili Taifa lirejee katika hali ya kawaida na amani idumu.