Unguja. Zubeir Ali Maulid amechaguliwa tena kuwa Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar kwa kipindi cha tatu.
Zubeir amechaguliwa leo Alhamisi Novemba 6, 2025 katika mkutano wa kwanza wa Baraza la 11 la Wawakilishi Zanzibar, ambapo hiki kitakuwa kipindi cha tatu tangu alipochaguliwa kwa mara ya kwanza mwaka 2015.
Spika Zubeir ambaye anatoka kwenye Chama cha Mapinduzi (CCM), amechaguliwa kwa kupata kura 53 sawa na asilimia 94.6 na kuwabwaga aliokuwa akichuana nao ambao ni
Chausiku Khatib Mohamed wa NLD aliyepata kura 3, Naima Salum Hamad wa UDP na Suleiman Ali Khamis wa ADC ambao wote hawakupata kura hata moja.
Kabla ya kupigwa kura, shughuli iliyoongozwa na Katibu wa Baraza la Wawakilishi, Raya Issa Msellem amewapa wagombea wote wanne dakika tano kujieleza na kuomba kura.
Akitangaza matokeo ya kura hizo Raya amesema waliopiga kura ni 68 waliokuwa wamefika ndani ya baraza hilo wakati shughuli ya kuomba na kupiga kura inaanza.
“Kati ya kura zilizopigwa, 12 zimeharibika, kwa hiyo namtangaza Zubeir Ali Maulid amechaguliwa kuwa Spika wa Baraza la Wawakilishi,” amesema Raya.
Baada ya kutangazwa, Zubeir ameapishwa na Katibu wa Baraza la Wawakilishi kushika rasmi madaraka hayo. Akiwashukuru wajumbe kwa kumchagua kwa kipindi kingine na kuomba ushirikiano ili atimize majukumu yake ipasavyo.
Jukumu la kwanza aliloanza nalo baada ya kuapishwa ni kuwaapisha wajumbe wa Baraza la Wawakilishi.
Kwa mujibu wa taarifa ya Baraza la Wawakilishi, walioapa ni wajumbe 71. Kati ya hao wa majimbo ni 50, viti maalumu 20 na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dk Mwinyi Talib Haji.
Kutokana na ratiba ya Baraza la Wawakilishi, uchaguzi wa Naibu Spika inatarajiwa kufanyika kesho Ijumaa Novemba 7, 2025 huku ikisubiriwa kuzinduliwa rasmi kwa Baraza hilo na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi.