Dar es Salaam. Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) limeisihi Serikali kuanzisha mchakato wa maridhiano haraka, ili kuponya majeraha kwa pande zote, huku likiwapa pole Watanzania walioguswa na maandamano yaliyozaa vurugu, kadhia mbalimbali na mauaji.
Maandamano hayo yalitokea wakati na baada ya uchaguzi mkuu Oktoba 29, 2025 katika mikoa mbalimbali ikiwemo Dar es Salaam, Dodoma, Mbeya, Mwanza, Mara na Arusha.
Taarifa iliyotolewa leo Alhamisi Novemba 6, 2025 na Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile imeeleza wanafuatilia kwa karibu na wamepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za vifo vya Watanzania, wakiwamo wanahabari na wengine waliojeruhiwa.
Amesema jukwaa linatoa mwito kwa mamlaka kufanya uchunguzi wa kina na kuhakikisha haki inatendeka.
“Tunaisihi Serikali kuanzisha mchakato wa maridhiano haraka, ili kuponya majeraha kwa pande zote. Tunaomba kila upande mchakato ukianza uwe tayari kushiriki kama nchi tumalize kadhia hii milele,” amesisitiza.
Balile amesema, “Jukwaa limerejea utamaduni wa Taifa letu wa amani na utulivu na kuakisi yaliyotokea yakazaa maafa haya. Tunafahamu yapo maumivu makubwa kila upande, ila tunaomba sasa tusimame pamoja kama Taifa, tuzungumze na kujisahihisha, ili kamwe haya yasitokee tena katika ardhi ya Tanzania.”
Balile amesema siku ya tukio jukwaa lilipokea taarifa za vifo vya vijana na askari polisi. “Baadhi ya wananchi waliwasiliana nasi wahariri, kuomba msaada wa kuulizia walipo ndugu zao.”
Amesema jukwaa linatoa pole kwa Watanzania waliopoteza ndugu, jamaa na marafiki katika vurugu zilizotokea katika kilichoanza kama maandamano ya amani, lakini kuishia kwenye uchomaji wa magari, vituo vya mafuta, nyumba, kadhia zingine za kiafya kwa waliopiga kura na hatimaye mauaji ya raia na askari.
“TEF inawakumbuka kwa heshima wanahabari na Watanzania waliouawa katika vurugu hizi, kwani wameacha pengo kubwa katika tasnia ya habari, kazini na familia zao. Pia tunawapa pole wote waliojeruhiwa katika matukio hayo,” amesema.
Amesema Taifa limeshuhudia madhara ya amani kupotea na tulikofika, hivyo tujizuie kama nchi isitokee tena.
“Mungu awape uponyaji wa haraka walioumia, azilaze mahali pema peponi roho za waliopoteza uhai, na atupe nguvu ya kusimama kama nchi tujisahihishe. Mungu ibariki Tanzania,” amehitimisha.