Mikoani. Ikiwa imepita wiki moja tangu uchaguzi umefanyika, matokeo yaliyotangazwa na wasimamizi wa uchaguzi baada ya wananchi kupiga kura Oktoba 29, 2025, sasa yako hadharani ambapo Chama cha Mapinduzi (CCM) kikiibuka na ushindi katika majimbo mengi nchini.
Matokeo hayo hayakupatikana mapema kutokana na changamoto ya kukatwa kwa mtandao wa intaneti, jambo ambalo lilitatiza utumaji wa taarifa zikiwemo za matokeo ya uchaguzi kwa wakati na kuchapishwa.
Mwananchi limefuatilia matokeo hayo kwa wasimamizi wa uchaguzi katika majimbo mbalimbali nchini na kubaini washindi katika uchaguzi huo kwa nafasi ya ubunge huku wabunge wateule hao wakitarajiwa kuripoti bungeni Novemba 8, 2025.
Mbali na CCM kunyakua majimbo mengi, vyama vya upinzani hasa ACT Wazalendo na Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), vimejipatia ushindi katika majimbo machache, hivyo vitawakilisha maeneo hayo na vyama vyao bungeni.
Katika Mkoa wa Mara, CCM kimepata ushindi katika majimbo yote 10. Katika jimbo la Musoma Mjini, Mgore Miraji ameshinda kwa kupata kura 14,555 dhidi ya wapinzani wake tisa ambao ni pamoja na Angela Lima wa Chaumma (3,762), Omar Mohamed wa CUF (119) na Julius Matto wa DP (50).
Wengine ni Salome Alex wa UDP (33), Hassan Ogolla wa Makini (32), Christina Ndego wa Sau (112), Michael Gabriel wa UMD (23), Geneviva Mechele wa AAFP (141) na John Kaseleka wa ACT Wazalendo (343).
Katika jimbo la Serengeti lililokuwa na wagombea wawili, mgombea wa CCM, Mary Daniel ameshinda kwa kura 182,562 dhidi ya Catherine Ruge wa Chaumma aliyepata kura 5,711.
Jimbo la Bunda Mjini, Ester Bulaya ameshinda baada ya kupata kura 83,908 huku Jeremiah Lameck (AAFP) akipata kura 1,233, Edward Saramba (CUF) akipata kura 1,367 na Manga Wanjala (NLD) akipata kura 919.
Jimbo la Rorya lilikuwa na wagombea watatu ambapo Jafari Chege wa CCM ameshinda kwa kura 165,660 dhidi ya Dady Midumbi (ACT Wazalendo) aliyepata kura 3,177 na Sospeter Rutaga (AAFP) aliyepata kura 1,282.
Katika jimbo la Musoma Vijijini, Profesa Sospeter Muhongo ameongoza kwa kupata kura 50,847, akifuatiwa na Magina Ng’aranga (ACT Wazalendo) akipata kura 12,171, Barnabas Mafuru ( CCK) akipata kura 458 na Kuleba Bwire (CUF) akipa kura 428 na Lukresia Girimba (UPDP) akipata kura 349.
Katika Jimbo la Tarime Vijijini, mbunge aliyemaliza muda wake, Mwita Waitara ameshinda kwa kura 165,341 huku mpinzani wake, Charles Mwera (ACT Wazalendo) akipata kura 8,519.
Jimbo la Mwibara, mbunge na waziri wa zamani, Kangi Lugola ameshinda kwa kura 30,646 huku mwandishi wa habari, Cyprian Musiba (ACT) akipata kura 7,723, John Magafu (CUF) akipata kura 211,4, Day Kalyanyama (DP) akipata kura 08 na Thomas Mgaywa (NCCR) akipata kura 192.
Katika Jimbo la Bunda, mbunge aliyemaliza muda wake, Boniphace Getere ameshinda kwa kura 22,393, Maxmilian Madoro (ADC) akipata kura 7,237 na Kastam Chagonga (Chaumma) akipata kura 366.
Katika Jimbo la Butiama, Dk Wilson Mahera (CCM) ameshinda kwa kura 112,876 huku Verena Charles (Chaumma) akipata kura 1,632.
Ester Matiko ameshinda nafasi ya ubunge katika Jimbo la Tarime baada ya kupata kura 52,369 na Mzarifu Ryoba (Chaumma) akipata kura 4,831.
Katika mikoa ya Songwe na Mbeya, CCM kimeshinda majimbo yote ya uchaguzi. Wagombea walioshinda ni pamoja na Philipo Mulugo (Songwe) akipata kura 116,735, Japhet Hasunga (Vwawa) akipata kura 126,945 na Onesmo Mkondya (Mbozi) akipata kura 124,204.
Wengine ni David Silinde (Tunduma) aliyepata kura 116, 258, Kondesta Sichalwe (Momba) akipata kura 117,521, Godfrey Kasekenya (Ileje) akipata kura 71,150.
Katika Mkoa wa Mbeya, Washindi wote pia ni wa CCM, ambao ni Dk Tulia Ackson (Uyole), Patrick Mwalunenge (Mbeya Mjini), Baraka Mwamengo (Kyela), Lutengano Mwalwiba (Busokelo), Anthony Mwantona (Rungwe), Bahati Ndingo (Mbarali) na Patali Patali (Mbeya Vijijini).
CCM, pia, kimenyakua majimbo yote katika Mkoa wa Njombe, wagombea waliochaguliwa ni Joseph Kamonga (Ludewa) aliyepata kura 80,419, Deo Mwanyika (Njombe mjini) kura 77,617 na Daniel Chongolo (Makambako) aliyepata kura 72,894.
Wengine katika mkoa huo ni Festo Dugange (Wanging’ombe) aliyepata kura 107,491, Edwin Swalle (Lupembe) akipata kura 50,637 na Festo Sanga (Makete) aliyepata kura 66,717.
Mwanza, Kahama, Kilimanjaro
Mkoani Mwanza, CCM kimeshinda majimbo yote ambapo katika Jimbo la Nyamagana, John Nzilanyingi ameshinda kwa kura 381, 295, Kafiti William ameshinda Ilemela wakati Buchosa ameshinda Eric Shigongo kwa kura 215,720.
Jimbo la Sengerema mshindi ni Hamis Tabasam aliyepata kura 198,830 wakati Ukerewe Dk Sweetbert Mkama ameshinda kwa kupata kura 186,879 na Magu ameshinda Boniventura Kiswaga.
Wengine walioshinda ni Moses Bujaga (Sumve) akipata kura 87,648 wakati Cosmas Bulala (Kwimba) akipata kura 117,724 na Silvery Luboja aliyeshinda katika jimbo la Misungwi.
Katika majimbo matatu ya yaliyopo katika Wilaya ya Kahama (Ushetu, Msalala na Kahama Mjini), CCM kimeongoza katika matokeo ya ubunge ambapo Kahama Mjini, Ngaiwa Benjamin ameshinda kwa kupata kura 253,112.
Katika Jimbo la Msalala, Magangila Mabula ameshinda akipata kura 186,316 wakati katika Jimbo la Ushetu, mshindi ni Emmanuel Charahani aliyepata jumla ya kura 200,349.
Katika Jimbo la Rombo, msimamizi wa uchaguzi, Cornelia Bitegeko amemtangaza, Profesa Adolf Mkenda (CCM) kuwa kuwa mshindi wa ubunge akipata kura 96,815.
Saashisha Mafuwe (CCM) ameibuka mshindi katikaa Jimbo la Hai akipata kura 106,774 wakati katika Jimbo la Vunjo Vijijini, Enock Koola (CCM) akishinda kwa kura 108,083. Moris Makoi (CCM) naye ameibuka mshindi katika Jimbo la Moshi Vijijini akipata kura 82,160.
Katika Jimbo la Mwanga, Dk Ngwaru Maghembe (CCM) ametangazwa mshindi akipata kura 70,037 wakati Dk Mathayo David Mathayo (CCM) akishinda katika Jimbo la Same Magharibi kwa kura 85,960 na Same Mashariki, Anne Kilango akishinda kwa kura 68,630.
Katika mikoa ya Manyara na Arusha, CCM kimeibuka na ushindi katika majimbo yote huku baadhi ya majimbo yaliyokuwa na mgombea mmoja wakishinda kwa kupigiwa kura nyingi za “Ndiyo”.
Katika Jimbo la Kiteto, Edward Ole Lekaita ametangazwa mshindi akipata kura 186,283 wakati Babati Mjini, Emmanuel Khambay akishinda kwa kura 37,520 na Mbulu vijijini, Emmanuel Nuwas akishinda kwa kura za “Ndiyo” 118,665 na kura za “Hapana” zikiwa 162.
Kwa upande wa Jimbo la Hanang, Asia Halamga ameshinda kwa jumla ya kura za “Ndiyo” 173,333 huku kura za “Hapana” zikiwa 1,106. Katika Jimbo la Simanjiro, James Ole Millya ameshinda kwa kura 150,665.
Huko Arusha, wagombea wa CCM wameshinda ubunge ambao ni Isack Joseph (Monduli), Daniel Awakii (Karatu), Paul Makonda (Arusha Mjini), Yannick Ndonyo (Ngorongoro) na Dk Steven Kiruswa (Longido).
Katika mkoa wa Ruvuma, upinzani umeshinda katika jimbo moja la Tunduru kaskazini ambako Ado Shaibu wa ACT Wazalendo ameshinda kwa kupata kura 80,282 huku CCM kikishinda katika majimbo mengine yaliyosalia.
Katika Jimbo la Tunduru Kusini, Fadhili Chilombe (CCM) ametangazwa mshindi akipata kura 63,417, sawa na asilimia 99 ya kura zilizopigwa huku Omary Msigwa (CCM) akitangazwa mshindi katika Jimbo la madaba akipata kura 43,689.