Madaktari wataja hatua 10 za kuondokana na kiwewe

Dar es Salaam. Kujiweka mbali na mitandao ya kijamii, simu janja na taarifa zinazoamsha hisia kali na kufanya maandalizi mazuri nusu saa kabla ya kulala, kunaweza kumsaidia mtu kuondokana na kiwewe hasa katika kipindi cha majanga na vurugu.

Kwa sababu inelezwa kwamba kiwewe au trauma kama inavyoelezwa na wataalamu, mara nyingi haitokani na kuumizwa kimwili pekee, bali pia na kile unachokishuhudia kwa macho au kukisikia.

Wataalamu wa saikolojia wanaeleza kuwa ni asilimia 30 tu ya watu waliopata majanga, ndio wanaweza kupata changamoto zinazohusiana na trauma, hivyo jamii inapaswa kutambua kuwa, kadiri muda unavyokwenda, hali hiyo inaweza kuisha kabisa.

Wakati muda ukitajwa kuwa ni tiba kubwa, wataalamu wengine wa masuala ya afya ya akili na saikolojia, wametaja mambo 10 yanayoweza kumsaidia mtu mwenye tatizo kiwewe.

Akizungumza na Mwananchi baada ya kutokea vurugu kwenye maandamano katika maeneo mbalimbali nchini, Mtaalamu wa saikolojia tiba, Saldin Kimangale amesema ili watu wapate nafuu, wanapaswa wapate nafasi ya kuzungumza na kuweka zuio la kutoshirikishana  ambako kutawafanya waendelee kupata maumivu yanayoweza kuchochea visasi.

Amesema ni muhimu kujizuia kutoshorikishana picha na video zinazoonyesha matukio ya kuumiza, kwa sababu baadhi ya watu wapo kwenye hatari ya kupata changamoto zaidi za trauma.

Kimangale ameshauri kuanzishwa kwa vituo vya dharura vya ushauri kwa njia ya simu ili kutoa msaada wa kisaikolojia kwa waathirika wa matukio ya vurugu.

Amesema wapo watu ambao hawakuhusika moja kwa moja na matukio hayo, lakini wameathiriwa kisaikolojia kutokana na milio ya risasi na milipuko ya mabomu wakiwa majumbani mwao.

Kwa mujibu wa Kimangale, ni muhimu viongozi wa dini, kijamii na Serikali kuzungumzia masuala ya uponyaji wa kiakili na hisia badala ya kutoa matamko yanayochochea hasira au makatazo ya kihisia, akisisitiza kuwa hatua hizo zinasaidia kujenga utulivu wa jamii baada ya misukosuko.

Amefafanua kuwa kila mtu anao wajibu wa kujipa muda wa utulivu na kutafakari akiwa peke yake katika mazingira ya asili, ili kupunguza mchanganyiko wa taarifa na msongo wa mawazo.

Amewashauri wananchi kujiepusha na matumizi makubwa ya simu na mitandao ya kijamii, hasa inapokaribia jioni, kwani taarifa nyingi zinazopatikana mtandaoni huamsha hisia kali.

Badala yake, amewahimiza kutumia muda huo kuzungumza na watoto, kushiriki michezo ya mwili na kufanya shughuli ndogo ndogo za nyumbani kama sehemu ya kujenga afya ya akili.

Aidha, ametoa ushauri kuhusu maandalizi ya kulala kwa amani kwa kuhakikisha mtu amefunga siku yake vizuri, amesali, hana njaa wala kushiba kupita kiasi na kuepuka matumizi ya visisimuzi kama kahawa, vinywaji vyenye sukari na vinavyoongeza nguvu.

Kimangale amesisitiza umuhimu wa mawasiliano ya kirafiki, akieleza kuwa kuzungumza na mtu unayemwamini na kumpenda kuhusu hisia zako, husaidia kupunguza homoni za msongo wa mawazo.

Ameongeza kuwa endapo mtu ataendelea kupata dalili kama uchungu, hasira kali, fikra za kujidhuru au kudhuru wengine na kukosa usingizi kwa zaidi ya siku tatu, anapaswa kufika kituo cha afya kilicho karibu au kupiga namba za dharura 110, 111, 115, 116 au 119 kwa msaada wa haraka.

Ameeleza kuwa katika nyakati za vurugu, milio ya risasi na milipuko ya mabomu haileti athari kwa waliojeruhiwa pekee, bali hata mashuhuda hubeba majeraha ya ndani yasiyoonekana kwa macho.

“Wengi huendelea na maisha wakidhani wamepona, kumbe bado wanabeba maumivu ya kiakili yanayoweza kuathiri afya ya akili na mwili kwa muda mrefu,” amesema mtaalamu huyo.

Wataalamu wengine wa afya ya akili wanabainisha kuwa hali kama hiyo ni ya kawaida kwa watu waliopitia matukio ya kutisha, wengine hupata usingizi kwa shida, ndoto mbaya, au kuona kama tukio limejirudia. Hali hiyo inajulikana kitaalamu kama trauma ya baada ya tukio.

Wanasema dalili zake ni pamoja na kumbukumbu zinazorudia za tukio, wasiwasi, hofu, hasira, kukosa usingizi, au kujitenga na watu na mazingira fulani.

Daktari wa Afya ya Akili kutoka Hospitali ya Kanda Mbeya, Dk Raymond Mgeni amesema janga ambalo hutokea wakati usiotarajiwa, huleta madhara ya kimwili, kiakili hadi kihisia.

Amesema matukio kama kusikiliza milio mikubwa ya vitu kama mabomu, kushuhudia tukio la kutisha husababisha msongo wa mawazo wakati huo na hata baada ya tukio husika.

“Hii husababisha wengine kuendelea kulikumbuka tukio, kushindwa kulala, kujawa na woga au wasiwasi au hata kuota ndoto za kutisha. Kisaikolojia matukio haya huweza kusababisha mtu kupata mahangaiko ya kiakili juu ya kukabiliana na tukio lilokwishatokea na hivyo huhitaji msaada ili hali isizidi kuwa mbaya zaidi,” ameshauri.

Dk Mgeni ametaja njia zinazoshauriwa kutumika kwa mtu ambaye kapitia janga na anapata hali ngumu kuvuka, moja ni kukubali kuwa janga kweli limetokea. Hii ni hatua ya awali kabisa ya kuruhusu kupona.

“Akili ikikataa kuwa hakukuwa na janga, huzidi kuteseka zaidi. Pili epuka kuendelea kuwa katika mazingira ya kuchochea kumbukumbu za janga husika, ili kuepusha hali mbaya zaidi ya mahangaiko katika akili,” amesema.

Pia, ni muhimu kuzungumza kile unachopitia kwa kuandika na hili hupunguza maumivu na uchungu unaoweza kuwepo kwa wakati huo.

Pia, jaribu karibu na watu wengine wanaoweza kutoa mazingira ya kukutia moyo na matumaini juu ya hatua za kufuata baada ya mshtuko wa janga. Pia, muone mtaalamu wa afya ya akili endapo bado dalili za kushindwa kuvuka dhidi ya janga zitaendelea.

“Epuka matumizi ya vilevi kama pombe, bangi au sigara kama njia ya kusahau maumivu au uchungu. Hili litaongeza madhara mengine mapya kama uraibu wa vilevi kwa siku za baadaye,” amesema Dk Mgeni.

Daktari bingwa wa magonjwa ya akili Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dk Said Kuganda ameshauri kuwa ni muhimu waliopata trauma ya kisaikolojia wawe na watu wao wa karibu, ndugu wa kuwafariji na wa kuwasaidia, huku wakiepuka kukaa peke yao.

Amesema kwa kawaida mtu yeyote anaposikia sauti ya risasi au bomu lazima apate mshtuko, ni mwitikio wa kawaida na mara nyingi huendelea kupata mshtuko kwa kipindi cha mwezi mmoja.

Kwa mujibu wa Dk Kuganda mshtuko utaondoka kwa wengi, iwapo mahitaji yao ya kila siku yatarudi ikiwemo vyakula, usafiri, ibada, kazi, shule na mahitaji mengine muhimu ambayo humfanya mtu aliyeshtuka kurudi kuwa sawa.

 “Kisaikolojia waliopitia majanga kama haya huchukua hata mwezi mzima kukaa sawa, mwingine ataogopa hata kutoka nje.”

Amesema itahesabia kuwa mtu amepata trauma iwapo hali ya kushtuka na woga itaendelea kumzonga hata baada ya mwezi mmoja kupita.

“Baada ya mwezi kupita wakawa bado hawako sawa, tutasema kuna tatizo watahitaji msaada wa tiba,” amesema.

Dk Kuganda pia amesema ni muhimu kutoangalia picha mbaya, ziwe za kweli au za kutengenezwa na akili mnemba, hiyo itawasaidia kurudi sawa kwa haraka.

Kwa mujibu wa Dk Kuganda, walio katika hatari ya kupata trauma ni wale waliopoteza wapendwa wao, na kwamba wanahitaji faraja zaidi wakati huu kwa kuwa kundi hilo linaweza kukaa na hali ya huzuni hata miezi sita.

“Wanatakiwa kuwa na watu wa karibu wanaomfariji, msiba huu si wa kawaida, tuongeze kuwafariji ili wawe na matumaini,” amesema.