KOCHA wa zamani wa Yanga, Mzambia Noel Mwandila ameteuliwa na Shirikisho la Soka la Zambia (FAZ) kuwa Mkufunzi wa washambuliaji wa timu ya taifa ya nchi hiyo, Chipolopolo kwa ajili ya Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) zitakazofanyika Morocco.
Mwandila aliyewahi kuifundisha Yanga katika kipindi cha George Lwandamina ambaye pia ni Mzambia kuanzia mwaka 2016 hadi 2018 na amepata shavu hilo jipya akishirikiana na kocha Moses Sichone aliyemrithi Avram Grant aliyeinoa tangu Desemba 22, 2022.
Sichone, ambaye awali alikuwa msaidizi wa Avram Grant, amekabidhiwa jukumu la kuongoza benchi la ufundi la timu ya taifa hilo, akipewa nafasi ya kufanya vizuri katika mashindano ya AFCON yatakayoanza, Desemba 21, 2025, hadi Januari 18, 2026.
Kocha msaidizi katika kikosi hicho ni Andrew Sinkala mwenye leseni ya UEFA B Plus, ambaye muda mrefu anaishi Ujerumani, huku akiwahi kuchezea timu mbalimbali za Ligi ya Bundesliga, zikiwemo, Bayern Munich, FC Koln, Augsburg na SC Paderborn.
Msaidizi namba mbili ni Perry Mutapa anayeifundisha Green Eagles, akiwa ni miongoni mwa kizazi cha mwaka 1999 cha timu ya vijana cha miaka 20 (U-20), kilichoonyesha ubora katika Kombe la Dunia la Vijana, chini ya Kocha Mkuu, Patrick Phiri.
Kennedy Mweene, aliyekuwa kipa wa timu ya taifa na mshindi wa Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka 2012, ameteuliwa kocha wa makipa kutokana na uzoefu wake na kwa sasa anafanya kazi akiwa na Mamelodi Sundowns ya Afrika ya Kusini.
Kwa upande wa aliyekuwa beki mkongwe wa timu hiyo, Joseph Musonda, ameteuliwa kocha wa mazoezi ya viungo, huku Katibu Mkuu wa FAZ, Machacha Shepande, akiweka wazi anaamini benchi hilo jipya la ufundi litaleta chachu ndani ya kikosi hicho.