BAADA ya kuchangia mabao mawili ya Ligi Kuu Bara akiwa na kikosi cha Fountain Gate, mshambuliaji wa timu hiyo, Mudrik Abdi Shehe ‘Gonda’, amesema taratibu anaanza kuzoea mazingira na ushindani, baada ya kutofanya vizuri msimu uliopita.
Mudrik alijiunga na timu hiyo Januari 2025, akitokea JKU SC ya Zanzibar ili kuzipa pengo la aliyekuwa nyota mshambuliaji mwenzake, Seleman Mwalimu ‘Gomez’, aliyejiunga na Wydad Casabalanca ya Morocco, kisha kutolewa kwa mkopo kwenda Simba.
“Huu ni msimu ambao napaswa kufanya vitu bora zaidi ili kuweka imani kwa benchi la ufundi na viongozi walionileta hapa, nashukuru nimeanza vizuri kwa kushirikiana na wenzangu, jambo ambalo kwetu kikosini linaongeza motisha,” amesema Mudrik.
Mshambuliaji huyo amesema baada ya timu hiyo kuanza vibaya kwa sasa kuna mwanga unaonekana kutokana na matokeo mazuri ambao wanayapata, huku akiwaomba mashabiki wa kikosi hicho kuendelea kuwaunga mkono na wachezaji wenzake wote msimu huu.
“Kila mmoja wetu anajua tumeanza msimu kwa changamoto mbalimbali ambazo hata hivyo, tunashukuru sana benchi la ufundi na viongozi kwa kutuweka katika mazingira mazuri ya kutujenga kiakili na kimwili hadi hapa tulipofikia muda huu,” amesema.
Bao alilofunga nyota huyo ni la ushindi wa timu hiyo wa 1-0, dhidi ya Dodoma Jiji la dakika ya 90, Oktoba 17, 2025, huku alilochangia ‘Assisti’, ni la Ismail Aziz Kader, wakati kikosi hicho kikishinda tena 1-0, mbele ya KMC, Oktoba 25, 2025.
Akiwa na JKU SC, Gonda, alifunga mabao manane katika Ligi ya Zanzibar msimu wa 2024-2025, akiungana na nyota wengine wa hivi karibuni walioibukia Bara, baada ya Seleman Mwalimu, Maabad Maulid wa Coastal Union na Yassin Mgaza wa Dodoma Jiji.