Hoja ya kumkamata Mange Kimambi yazua mjadala

 Dar es Salaam. Wakati Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza Johari akieleza kuwa Serikali inaangalia uwezekano wa kumchukulia hatua Mange Kimambi kwa tuhuma za kuhamasisha Watanzania kuandamana, baadhi ya wanasheria wamesema suala hilo si rahisi kisheria.

Wataalamu hao wamesema ni vigumu kwa nchi kama Marekani kumkabidhi mtu kwa nchi nyingine, hususan pale anapokabiliwa na tuhuma zenye mwelekeo wa kisiasa, hata kama kuna mikataba ya ushirikiano au makubaliano ya kiuhamisho kati ya mataifa hayo.

Johari alitoa kauli hiyo alipowasili katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali jijini Dodoma, ambako pia alifanya mazungumzo na wafanyakazi wa ofisi hiyo, jana muda mfupi baada ya kuapishwa kushika wadhifa huo.

Johari aliapishwa jana Jumatano, Novemba 5, 20254, Ikulu ya Chamwino, jijini Dodoma na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Makamu wa Rais, Dk Emmanuel Nchimbi.

Akizungumza baada ya kuwasili ofisini kwake, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Johari, alisema kuwa ofisi yake inaendelea kuangalia uwezekano wa kumkamata mwanadada aliyeko nje ya nchi, akimaanisha Mange Kimambi, ikiwa ni pamoja na kutumia mikataba maalumu ya ushirikiano iliyopo kati ya Tanzania na Marekani.

“Haiwezekani mtu amekaa nje ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, dada tu hata ukimuangalia muonekano anawaambia watu wakafanye hivi wanaenda kufanya kweli halafu imetokea anaanza kutamba anasema bado nitakuja kivingine, lazima tumkamate.

“Nakuambia DPP (Mkurugenzi wa Mashitaka nchini) huyu lazima tumkamate tuangalie kama kuna makubaliano na Marekani, tuangalie tu, tutafikiri tu, lakini hawezi kututambia kwa kiasi hicho yani anakubali kuwa hicho alipanga kukifanya na bado atafanya zaidi sasa tunamuachaje,” amesema Johari.

Amesema ameanza kushughulikia suala hilo kwa sababu ni moja ya majukumu aliyopewa, na anaamini kuwa ofisi yake ina watu wenye ujuzi na akili, ambao wanahitaji usimamizi bora pamoja na motisha ya kutimiza majukumu yao ipasavyo.

“Hivyo suluhisho litapatikana kisheria na hata kidiplomasia. Tumeona mali za watu zimeharibiwa, mali za umma hadi gari ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu linachomwa moto haliwezekani, gari letu limechomwa moto na dereva wetu kakimbia, lakini wanasheria tuko mahiri na tutakuja na suluhisho zuri tunakwenda kufikiri ili tuweze kuishauri Serikali vizuri,” amesema.

Amesema kuwa katika kushughulikia suala hilo, watu wa vyombo vya ulinzi na usalama wana nafasi yao na watatekeleza majukumu yao kwa upande wao.

Hata hivyo, hawa hawawezi kuachia kila kitu kwa upande wa sheria; badala yake, watasimama kisheria, kwa kuwa sheria zilipuuzwa na kuvunjwa.

Johari anakalia kiti cha Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa mara ya pili. Aliteuliwa kushika nafasi hiyo kwa mara ya kwanza Agosti 14 mwaka jana, akijaza pengo lililoachwa wazi na Jaji Eliezer Feleshi, aliyeteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani.

Kabla ya uteuzi huo, Johari alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA).

Baada ya tamko hilo, Mange Kimambi kupitia ukurasa wake wa Instagram alimjibu kuwa kuna siku atarudi Tanzania mwenyewe, lakini haiwezekani kurudishwa kinguvu ili akamatwe.

Mange amedai Serikali ya Marekani haiwezi kumrudisha Tanzania.

Wakili Jebra Kambole amesema jambo la msingi amblao mwanasheria alipaswa kuumiza kichwa si kuangalia namna ya kumkamata Mange, bali kwa nini watu wanamsikiliza wakati si kiongozi na hana cheo chochote nchiini.

“Hili ndiyo linapaswa kumuumiza kichwa kwa nini watu wanamsikiliza akiwa nje na watu wanamtii kuliko viongozi wao, nasikitika sana kusikia kauli hii. Halafu kumtoa mtu katika nchi nyingine kama anatuhumiwa kwa kosa la kisiasa hakuna nchi inayoweza kumtoa mtu kumpeleka hata kama mna makubaliano,” amesema.

Amesema ili kumkamata mtu unahitaji kibali cha mahakama husika na ili atolewe ni lazima kosa hilo lihesabiwe kama kosa kwa pande zote mbili, lakini lisihusiane na siasa na hasa kama anakopelekwa kuna uwezekano wa kunyongwa.

“Katika mazingira kama hayo haiwezekani. Nadhani afanye utafiti aone wanasheria waliopopita waliishia wapi, kabla ya kutoa kauli ambayo ni kama vile haitekelezi kwani maandamano katika nchi aliyopo (Marekani) na Tanzania si kosa hivyo, haiwezekani kuchukuliwa kuletwa Tanzania,” amesema Kambole.

Wakili Dk Onesmo Kyauke amesema kama kuna mkataba jambo hilo linaweza kufanyika, lakini kwa sheria za Marekani inakuwa ngumu kwani wanatambua uhuru wa kujieleza na maandamano si kosa.

“Hata kama wangeomba bado itakuwa ngumu kwa sababu akisema kama akiletwa huku hatatendewa haki hawatamtoa. Wao wanatambua sana uhuru wa kujieleza ndiyo maana hata mitandao ya kijamii hawamfungii kwa sababu si kosa.

“Ni jambo linalowezekana ingekuwa ni nchi za kiafrika ambazo sera zetu zinafanana kama Rwanda, Uganda ingekuwa rahisi. Hata kama Serikali ya Marekani itakuwa tayari kumleta mahakama yao ikitoa zuio hawezi kuletwa kwa sababu mahakama zao zinanguvu sana,” amesema.

Amesema kitendo cha kudhani kama anaweza kurudishwa Tanzania na Serikali ya Marekani ni kama kujidanganya. “Lakini mtu huyo makazi yake huko Marekani yakoje, kama ni raia inakuwa ni ngumu kwani ana haki zake huko katika nchi yake hususani kama ana watoto.

Kama hakuna Mkataba wa moja kwa moja (Extradition Treaty) uliotiwa saini na kutekelezwa kikamilifu mahususi wa kubadilishana watuhumiwa kati ya Tanzania na Marekani, kuna namna Tanzania inaweza kufanya kati yake na Marekani.

Kwa mujibu wa taarifa mbalimbali, bado inaweza kufanyika kati ya nchi hizo mbili kulingana na sheria za kimataifa na miongozo ya uhusiano.

Mfano, njia zinazowezekana za kubadilishana watuhumiwa ni sheria za ndani ya nchi.

Tanzania inaweza kutegemea Sheria ya Kubadilishana Watuhumiwa ya Tanzania, ambayo inaweza kuruhusu ushirikiano na nchi ambazo hazina mkataba wa moja kwa moja, kwa masharti ya kurudishiana fadhila (reciprocity).

Pia, Marekani ina sheria zake zinazoruhusu mashirikiano ya aina hii hata bila mkataba maalumu, kulingana na sheria za Marekani na misingi ya kimataifa.

 Mikataba mipana ya kimataifa

Nchi zote mbili zinaweza kuwa zimetia saini na kuridhia Mikataba ya Kimataifa ya Umoja wa Mataifa inayohusu uhalifu fulani (kama vile uhalifu wa dawa za kulevya, ugaidi, au rushwa) ambayo inajumuisha vifungu vya kubadilishana watuhumiwa (Extradition) kama sehemu ya ushirikiano wa kupambana na uhalifu.

Ushirikiano wa Kimahakama (Judicial Cooperation) na Kidiplomasia

Ubadilishanaji wa watuhumiwa unaweza kutokea kupitia maombi rasmi ya Serikali moja kwenda nyingine, ikitegemea ushirikiano mzuri wa kidiplomasia na mamlaka za kimahakama za nchi hizo mbili. Hii mara nyingi hujulikana kama Msaada wa Sheria wa Mutual Legal Assistance (MLA).

Kanuni ya Kufanana kwa Kosa (Dual Criminality): Kosa ambalo mtuhumiwa anasakwa lazima liwe ni kosa la jinai katika nchi zote mbili (Tanzania na Marekani).

Kawaida, hakuna mabadilishano yanayofanyika kwa makosa ya asili ya kisiasa.

Masuala ya hukumu ya kifo yanaweza kuwa kizuizi, kwani nchi inayopokea ombi inaweza kuhitaji uhakikisho kwamba hukumu ya kifo haitatolewa au haitatekelezwa kabla ya kukubali kumrudisha mtuhumiwa.

Taratibu zote lazima zizingatie haki za msingi za mtuhumiwa.