Mabaki ya mwili wa Mtanzania mwingine aliyetekwa Israel wapatikana

Dar es Salaam. Serikali ya Israel imesema, imepokea mabaki ya mwili wa kijana wa Kitanzania, Joshua Mollel (21), aliyetekwa Oktoba 7, 2023 wakati wa vita ya Israeli na Palestina.

Joshua alikuwa miongoni mwa Watanzania wawili na raia wengine wa mataifa mbalimbali waliotekwa Oktoba 7, 2023, nchini Israel na katika maeneo ya Wapalestina hususani Gaza.

Mbali na Joshua, mwili wa Clemence Mtega  ulipatikana mwezi mmoja baadaye (Novemba 17, 2023) na kurejeshwa Tanzania kwa taratibu za mazishi.

Joshua na Clemence ni miongoni mwa vijana wa Kitanzania wapatao 260 waliokwenda Israel kushiriki mafunzo ya kilimo cha kisasa kwa vitendo chini ya Mpango wa Ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Israel.

Wakati wanaotekwa walikuwa wakifanya mafunzo ya kilimo kusini mwa Israel wakati wapiganaji wa Hamas walipovamia eneo hilo Oktoba 7, 2023. Aliuawa katika Kibbutz Nahal Oz, na mwili wake kuchukuliwa na wapiganaji wa Hamas.

Tangu mwaka 2023, mwili wa Joshua pamoja na miili ya mateka sita waliouawa, Waisraeli watano ilikuwa chini ya wanamgambo hao wa Hamas na sasa imebaki sita ambayo haijarejeshwa.

Shirika la Habari la Uingereza (BBC) limenukuu Ofisi ya Waziri Mkuu wa Israel ikieleza baada ya kukamilika kwa vipimo vya kitabibu katika Kituo cha Kitaifa cha Tiba ya Uchunguzi wa Vifo, wizara ya mambo ya nje iliijulisha familia ya Joshua.

Taarifa hiyo imeeleza, Serikali ya Israel inashirikiana na familia ya Joshua katika kipindi hiki kigumu pamoja na familia zote za mateka waliopoteza maisha.

Pia, ilisisitiza Hamas inapaswa kurudisha miili yote ya mateka waliouawa chini ya makubaliano ya kusitisha mapigano, ikiongeza kuwa mamlaka za Israel hazitaacha jitihada hadi tuwarejeshe mateka wote waliopoteza maisha, kila mmoja wao.”

“Katikati ya huzuni yao na ufahamu kwamba mioyo yao haitapona kikamilifu, kurejeshwa kwa Joshua kunatoa faraja fulani kwa familia iliyoteseka kwa mashaka yasiyovumilika kwa zaidi ya miaka miwili.”

Kabla ya kukabidhi mabaki ya Joshua kwa Msalaba Mwekundu huko Gaza Jumatano jioni, wanajeshi wengi wa Hamas walidai wameupata mwili wa mateka katika mtaa wa Shejaiya, mashariki mwa mji wa Gaza.

Katika siku za hivi karibuni, Israel imewaruhusu wanachama wa Hamas na wafanyakazi wa Msalaba Mwekundu kutafuta mabaki ya miili katika eneo hilo, ambalo bado lipo chini ya udhibiti wa wanajeshi wa Israel.