Pedro ashtukia jambo Yanga, aliamsha fasta kambini

YANGA iko kambini ikiendelea kujifua kwa ajili ya mechi inazotarajia kuzicheza katika Ligi Kuu Bara na michuano ya kimataifa, lakini kuna jambo zito ambalo kocha mpya Pedro Goncalves amelishtukia na fasta ameliamsha akitaka lirekebishwe mapema.

Jambo hilo limeanza kuonekana kuwatesa mastaa wa klabu hiyo wanaoendelea kupigishwa tizi la maana ambapo wikiendi hii watashuka kwenye Uwanja wa KMC Complex, kumalizana na KMC katika mechi ya Ligi Kuu Bara.

Ipo hivi. Kocha Goncalves raia wa Ureno, ameukataa utimamu wa mwili wa wachezaji wa kikosi hicho, haustahili kuwepo katika kikosi hicho kinachotaka kuchukua mataji akianza hesabu mpya haraka za kubadilisha mambo.

YANG 01


Kuanzia hapo kwanza kocha huyo akawazuia mabosi wa klabu hiyo, kumtoa kocha wa mazoezi ya viungo Tshephang Mokaila na anataka kumwangalia ubora wake.

Mokaila ni yule raia wa Botswana, aliyekuja wakati wa Kocha Romain Folz ambaye alishaachana na kikosi hicho, akiwa mtu pekee aliyesalia baada ya Mfaransa huyo kusitishiwa mkataba baada ya kufungwa mechi ya kwanza ya raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi Silver Straiker ya Malawi iliyopigwa ugenini na kuletwa Mreno.

Huko kambini, kazi ya kuwaongezea ufiti wachezaji wa Yanga imeshaanza kwa dozi kidogo kidogo ikiwapa wakati mgumu mastaa wa timu hiyo bahati yao ikiwa ni mechi za mashindano hususan Ligi Kuu Bara.

YANG 04


Kocha Goncalves hataki kupandisha kwa nguvu utimamu wa mwili akihofia anaweza kuwachosha wachezaji na kushindwa kufanya vizuri katika mechi za ligi kabla ya kuanza kibarua cha mechi za makundi ya CAF dhidi ya waarabu Far Rabat na JS Kabylie.

Yanga imepangwa Kundi B la Ligi ya Mabingwa Afrika ikiwa na vigogo kutoka Afrika Kaskazini, AS FAR Rabat ya Morocco, JS Kabylie ya Algeria na Al Ahly ya Misri.

Goncalves ameonekana akiwa na Mokaila wakipandisha utimamu wa mwili kwa mazoezi makali ya mbio za tofauti kisha baadaye kurudi kuuchezea mpira taratibu katika mazoezi hayo hayo.

YANG 02


Yanga itakutana na KMC katika mechi ya Ligi Kuu Jumapili Novemba 9, 2025, ukiwa ni wa pili kwa Goncalves akitangulia na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Mtibwa Sugar mara tu alipoteuliwa kuchukua nafasi ya Folz.

Akiwa mazoezini, Goncalves ameonekana kuwa mkali akitaka umakini kwa wachezaji wake akifuatilia kwa makini kazi ya Mokaila akiwapa dozi wachezaji wa timu hiyo.

Mazoezi hayo yamewaacha hoi wachezaji wa kikosi hicho ikithibitisha mastaa hao hawakuwa sawasawa kama walivyoshtukiwa na Mreno huyo mwenye kibarua cha kuiwezesha Yanga kutetea mataji ya Ligi Kuu Bara, Kombe la Muungano na Kombe la Shirikisho (FA) iliyotwaa msimu uliopita mbali na kufika mbali CAF.

YANG 03


Msimu uliopita, Yanga iliishia makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya nyuma yake kutinga robo fainali, lakini ilifika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika 2022-2023 ikiwa chini ya kocha Nasreddine Nabi na kushindwa kutwaa taji kwa kanuni ya bao la ugenini kwa USM Alger ya Algeria baada ya matokeo ya jumla kuwa sare ya 2-2.