Pamba yazitaka pointi tatu kwa Singida, watatu kukosekana

KESHO Jumamosi Novemba 8, 2025, Pamba Jiji itaikaribisha Singida Black Stars katika mechi ya Ligi Kuu Bara itakayochezwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza kuanzia saa 10:00 jioni, huku wenyeji wakizitaka alama tatu za nyumbani.

Hii itakuwa mechi ya sita kwa Pamba Jiji msimu huu, ambapo tano zilizopita imeshinda mbili, sare mbili na kupoteza moja, huku ikifunga mabao sita na kuruhusu matano, inakamata nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi ikiwa na point nane.

Singida BS inakamata nafasi ya nane ikiwa na alama sita baada ya kucheza mechi mbili na kushinda zote dhidi ya Mashujaa FC na KMC.

Mechi ya kesho ni ya tatu kwa timu hizo kukutana kwenye Ligi Kuu Bara, ambapo msimu uliopita Singida BS ilishinda 1-0 CCM Kirumba na kutoa sare ya mabao 2-2 Uwanja wa Liti, Singida.

Akizungumzia maandalizi ya mechi hiyo, Kocha Mkuu wa Pamba Jiji, Francis Baraza, amesema vijana wake wako tayari kwa kwani wamefanya maandalizi ya kutosha ya kupata alama tatu nyumbani.

Amesema hana wasiwasi na ukubwa wa Singida Black Stars kwani Pamba Jiji ina historia kubwa kuliko wapinzani wao, hivyo wachezaji wakitimiza kile alichowapa mazoezini watapata ushindi.

“Tunaelewa ni mechi ngumu japo naamini wachezaji wangu wakiwa kwenye ubora wao itakuwa ni mechi nzuri. Tumeangalia michezo yao ni timu nzuri, wanakuja hapa wakiwa na ujasiri wa kuchukua alama tatu, lakini nawaambia mashabiki watarajie utakuwa mchezo mzuri,” amesema Baraza.

Kocha huyo amesema nyota wake watatu akiwemo beki Abdallah Sebo ambaye ana matatizo ya kifamilia, Amosi Kadikilo na kiungo Salehe Masoud wenye majeraha watakosekana katika mechi hiyo, lakini anaamini ana kikosi kipana kitakachompa matokeo mazuri.

‎“Sina hofu yoyote kama wachezaji wangu watabeba yale ambayo tumeelekazana mazoezini nina imani tutabeba pointi tatu. Vijana wangu wako tayari, nina kikosi ambacho hakinipi uoga wowote, tunajua tunacheza na timu gani, dakika 90 naamini zitaamua,” amesema.

‎Naye, nahodha wa timu hiyo, Yona Amosi amesema wachezaji wako tayari kwa mechi hiyo bila kujali mpinzani wanayekutana naye huku lengo likiwa ni kuwapa furaha mashabiki wao.

‎”Kwetu hakuna mechi ndogo, sisi tumejipanga, niwaondoe mashaka mashabiki wa Pamba Jiji waje uwanjani, hatutawaangusha. Maelekezo tunayopewa na benchi la ufundi tunayafanyia kazi kuhakikisha tunafanya vizuri,” amesema Amosi.