Baba wa Mtanzania aliyefia Israel aibuka kupatikana kwa mwili mwanaye

Simanjiro. Baba mzazi wa kijana Joshua Mollel (21) aliyetekwa na kuhofiwa kuuawa kwenye mapigano ya Israel na Palestine, Loitu Mollel amesema bado hajapata taarifa rasmi ya kupatikana kwa mwili wa mtoto wake.

Joshua alikuwa miongoni mwa vijana 260 wa Kitanzania waliokwenda Israel kwenye mafunzo ya kilimo cha kisasa kwa vitendo chini ya mpango wa ushirikiano wa Tanzania na Israel mwaka 2023.

Joshua alitekwa wakati akifanya mazoezi ya kilimo kusini mwa Israel wakati wapiganaji wa Hamas walipowavamia na mwili wake kuchukuliwa na wapiganaji hao.

Joshua na Mtanzania mwingine Clemence Mtega ambaye mwili wake ulipatikana na kurejeshwa Tanzania wakiwa na raia wengine wa mataifa mbalimbali walitekwa kwenye mapigano hayo katika eneo la Gaza.

Serikali ya Israel hivi karibuni imeeleza kwamba imepokea mabaki ya Joshua aliyetekwa Oktoba 7 2023 kwenye vita ya Israel na Palestina.

Akizungumza kwa njia ya simu leo ijumaa Novemba 7, 2025 akiwa mji mdogo wa Orkesumet wilayani Simanjiro mkoani Manyara, Mollel amesema bado hajapata taarifa rasmi ya kupatikana kwa mabaki ya mwili wa mtoto wake.

Amesema bado hajapata taarifa rasmi juu ya suala hilo hivyo hana chochote cha kuzungumza juu ya tukio hilo.

Hata hivyo, mmoja kati ya wakazi wa mji mdogo wa Orkesumet, Richard Seuri ameeleza kwamba Joshua alikuwa miongoni mwa vijana wastaarabu waliokuwa na maono ambao ndoto zao zimemalizwa bila kutimizwa.

Seuri amesema Joshua ni kijana ambaye hakupitia hata jeshi la mgambo ila akakutwa na mauti na maharamia waliokuwa wanapigana nje ya nchi huko Israel ila anashukuru Mungu hata mabaki ya mwili wake yamepatikana ili azikwe kwa heshima.

Amesema suala la mzazi kuambiwa kuwa mtoto wako amefariki dunia na wewe hukuona hata mwili wake inaumiza sana kwani ni bora upate hata mwili ufahamu kubwa umezika kuliko awali.

Desemba 17 hadi 31 mwaka 2023 familia ya Joshua iliweka msiba baada ya kuona mtandaoni kipande video iliyowahakikishia kuwa Joshua ameuawa.

Mollel baba wa marehemu Joshua, alienda Israel kwa wito wa Serikali ya Israel na kurejea nchini Desemba 29 mwaka 2023 na baada ya kurejea aliwaeleza waandishi wa habari kwamba safari hiyo ilikuwa ya huzuni isiyo na matumaini.

“Serikali ya Israel walinieleza hali halisi namna ilivyokuwa hao maharamia walivyoingia na kuwaua watu bila kuwa na huruma,” amesema Mollel.

Joshua ni mtoto wa kwanza kati ya watoto wanne wa Mollel ambaye alikwenda Israel kwa mafunzo ya kilimo cha kisasa kwa muda wa miezi 11.